Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Udanganyifu watawala mitihani darasa la saba
Udanganyifu watawala mitihani darasa la saba
By Habari Tanzania | Published  12/14/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Midraji Ibrahim

UDANGANYIFU katika mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba mwaka huu, umeishtua Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kulazimika kusitisha kutangaza viwango vya ubora na ufaulu wa kila mkoa.

Kutokana na udanganyifu huo uliogundulika wakati wa usahishaji wa mitihani, wanafunzi 294, wakiwamo watatu wasioona, wamefutiwa matokeo baada ya kubainika kuwa walihusika na vitendo vya udanganyifu, huku matokeo ya wanafunzi 2,677 yakishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, alisema matokeo ya watahiniwa hao yamesitishwa kutokana na kuwepo kwa dalili za udanganyifu katika mitihani na uchunguzi dhidi yao unaendelea.

Sitta alisema watahiniwa watakaothibitika kushiriki udanganyifu huo watafutiwa matokeo kwa mujibu wa kanuni za mitihani na kwamba ambao hawatathibitika watapewa matokeo yao.

"Matokeo ya ufaulu kwa kulinganisha mikoa hayatatangazwa kutokana na udanganyifu uliojitokeza katika baadhi ya mikoa nchini," alisema Sitta na kuongeza kuwa, mitihani haikuvuja bali kilichofanyika ni udanganyifu mbalimbali. Matokeo ya watahiniwa ambao hawabainika kufanya udanganyifu yatatolewa leo katika mikoa yote.

Waziri huyo, aliwahakikishia wananchi kuwa waliohusika na udanganyifu huo watachukuliwa hatua kali za nidhamu na sheria, huku akisita kutangaza aina ya hatua zitakazochukuliwa.

"Sio rahisi kutoa jibu la hatua gani zitachukuliwa, lazima tujue kwanza aina na kiwango cha udanganyifu...kila mwaka umekuwepo udanganyifu, lakini mwaka huu tumeamua kuwa wazi," alisema.

Kuhusu kiwango cha wanafunzi waliofaulu, Waziri Sitta alisema watahiniwa 664,323 walifanya mtihani huo na kati ya hao, watahiniwa 468,187 sawa na asilimia 70.48 wamefaulu ukilinganisha na kiwango cha kufaulu cha asimilia 61.67 mwaka jana.

Wasichana 211,224 kati ya 327,006 wamefaulu sawa na asilimia 64.6, huku wavulana 256,963 kati ya 337,317 sawa na asilimia 76.2 wakiwa wamefaulu. Jumla ya wanafunzi 686,192 walijiandikisha kufanya mtihani huo, lakini waliofanya mtihani ni 667,294 sawa na asilimia 97.2. Watahiniwa 18,898 hawakufanya mtihani.

Sitta alisema sio chini ya asilimia 70 ya waliofaulu watakaojiunga na sekondari na kuwataka wasichana kuongeza kasi zaidi katika masomo ili waweze kufikia kiwango cha wavulana na hata kuwapita na kutoa ushindani.

Katika hatua nyingine, Waziri Sitta alisema Februari mwakani, serikali inatarajia kuajiri walimu kwa ajili ya kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi watakaochaguliwa kuingia sekondari.

Alisema ongezeko la kiwango cha kufaulu ni sehemu ya mafanikio ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem) ambao umeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ikiwamo ongezeko la vyumba vya madarasa, vyoo, upatikanaji wa samani, maji, ajira ya walimu, vitabu na vifaa vingine.

Takwimu za Sitta zinaonyesha kuwa kiwango cha kufaulu kimekuwa kinaongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2002 waliofaulu walikuwa ni asilimia 27.1; mwaka 2003 (40.1%), mwaka 2004 (48.68%) na mwaka 2005 wasilimia 61.76.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Nestory K.Manoni)
    Rating
    Mh.Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

    Napenda kuwapongeza vijana wote
    waliochaguliwa kama washindi baada ya Mtihani wa Darasa la Saba.
    Kinachonisikitisha na kunikatisha tamaa kama mmoja wa wazazi nipale ambapo suala la baadhi ya wasimamizi kuendeleza wimbi la kutoa mitihani kwa baadhi ya wanafunzi kinyume cha utaratibu.
    Kitendo hiki pia kinavunja moyo na kuwanyima haki wanafunzi wanaotumia uwezo wao kiakili kutaka kushinda mitihani hiyo lakini wanashindwa kufikia malengo hasa watoto wa masikini kwa kuwa wanaoonekana kushinda ni wale wanaofanyiwa mpango wakati wa mitihani hiyo.
    Lakini kwa hali halisi wengi wao hawana uwezo wa kumudu mitihani hiyo iwapo mbinu hizo zisipotumika na ukiwafuatilia sana hao wanaoshinda mitihani kwa asilimia ya juu sana wanapata alama za mwisho kabisa wanapofikia mtihani wa mwisho wa kumaliza elimu ya sekondary.
    Suala la baadhi ya shule kugundulika na nyingine kutogundulika ni jinsi gani umahili wa kufanikisha mipango hiyo ulivyofanyika,pengine wazoefu wameadivance zaidi mbinu hizo au waliogundulika waliishi kwa mazoea yale yale na mbinu zile zile, hili ni tatizo la nchi nzima.

    Je,udanganyifu huu utaendelea hadi lini ili na wale wasiokuwa na uwezo wa kudanganya wapate haki zao za kimsingi katika elimu?

    Inasikitisha sana kuona kuwa wanafunzi wanafutiwa mitihani na hivyo kutohesabika kabisa kuwa walihitimu elimu ya msingi katika nchi yao kwa manufaa ya watu wachache tu.
    Ni vema serikali ikatazama na kuamua adhabu nyingine kwa wahusika kuliko kuwaadhibu hao wanafunzi kiasi hicho, ikizingatiwa kuwa wengi wao ni watoto waliochini ya umri wa miaka 16,hivyo kisheria hawana kosa la moja kwa moja kuweza kuwatia hatiani.

    kama watoto akili yao haiwezi kwa urahisi kupinga maauzi yaliyofikiwa na wazazi wao na waalimu wao katika harakati za kuandaa mipango hiyo,na kama wanaonekana kuwa na kosa la moja kwa moja ni vema wakashitakiwa kama waharifu ili uchunguzi wa kisheria ukafanyika kuliko kuwajenerolizi.

    Kufanikiwa kwa udanganyifu huo ni rushwa,kwa kuwa sheria ya kosa la kutoa na kupokea rushwa ipo na adhamu inajulikana kupitia mahakama ni bora zaidi ikatumika kuliko hiyo ya kufuta matokeo kwa shule nzima wakiwemo hao walemavu waliotajwa,nani ataubeba huo mzigo mzito iwapo serikali inawazuia kujiendeleza ki-elimu?

    Adhabu ya kufuta matokea mashuleni imedumu kwa muda wa miaka mingi sana hapa nchini,hivi sheria hiyo inayonyima haki za watoto kielimu haiwezi kuboreshwa kiasi kwamba watoto wa shule wasihusike moja kwa moja katika uhalifu huo kwa kuwa katika harakati za kuandaa mpango wa kuonyesha mitihani watoto wanaohusika hawashirikishwi moja kwa moja ila hupokea maelekezo kutoka kwa walimu na wazazi wao kwa kushirikiana na wasimamizi wa mitihani.

    Natambua bayana jitihada za awamu ya nne kuwa haitaki kuendeleza uharifu uliokithiri hapa nchini kwa baadhi ya watendaji wa umma lakini pamoja na mazuri hayo ni bora suala la wanafunzi kuonyeshwa mitihani kinyume cha utaratibu liangaliwe kwa makini na kuamuliwa kwa manufaa ya jamii nzima ya watanzania ili kuwanusuru watoto ambao ni hazina kubwa ya taifa katika mambo mbalimbali ya kuijenga na kuiendeleza nchi.

    Dereva anayekwepa kumgonga msafiri mmoja barabarani na kusababisha kuiingiza mtaroni gari iliyobeba abiria 60 au zaidi na kusababisha vifo vya watu wengi,huyo si dereva makini na hafai kabisa kuendelea kuendesha.
    Si vizuri sheria inayotumika sasa kuadhibu watoto inayofanana kabisa na mfano huo ikaendelea kutumika kwa manufaa ya wachache.

    Nakupongeza sana Mh.waziri mama Sitta kwa kutotaja shule zilizoshinda,haina maana kuendelea na mfumo huo maana unachochea kwa kiwango kikubwa sana mazingira ya rushwa kwa kuwapa wasimamizi chochote watakacho ili watoto wa shule husika wapewe mitihani kinyume cha utaratibu kama sehemu ya kutangaza sifa ya jina la shule (promotion)ili mwaka unaofuata wazazi wajikaange kwa mafuta yao kupeleka watoto wengi zaidi katika shule hiyo hasa shule za baadhi ya wamiliki binafsi,kwa kuwa mfumo mkuu wa shule hizo imekuwa ni biashara tupu na si vinginevyo.
    Utashangaa kuona kuwa shule za serikali tuition na pre-form one vimepigwa marufuku lakini katika shule za watu binafsi ambako ada ni kubwa sana bila udhibiti wowote,tuition, pre-form one,ununuzi wa ream za karatasi A4 na kuchangia majengo ndo vimepamba moto.
    Kivutio kimekuwa ni kuongea Kiingereza,Kifaransa na kujifunza computer tu na kwa kuwa wazazi wengi hatujui Kiingereza wala computer,tunafarijika kuweka watoto katika shule hizo kwa nia njema kabisa,lakini mwisho wa siku hakuna kinachoonekana.
    Mfano mzuri ni pale baadhi ya shule hizo zinapogundulika kuhusika na mchezo huo mbaya wakati zinawatoza wazazi fedha nyingi za ada ili watoto wao wawe na uwezo mzuri wa kushinda masomo bila mizengwe.

    Mh.mama Sitta umefika wakati mwafaka wa kuzifanyia kazi shule hizo ili ziendane na malengo yake na siyo kuendelea kuwaibia wananchi kwa janja ya nyani.
    Kwa kuwa serikali haina uchoyo wa kuwabagua wanafunzi wanaofaulu kutoka shule za wamiliki binafsi kwa kutoa nafasi za kuendelea na masomo popote nchini, ni vema nao wakahusika kuondoa baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuwa ni kero kubwa kwa wazazi kama vile ada za tuition, michango ya majengo na ununuzi wa ream nzima ya karatasi A4 kila mwaka."Sheria ni msumeno"

    Kwa upande wa shule za serikali,ni vema wizara husika ikapunguza vitisho vyake kwa wakuu wa shule na maafisa elimu kwa maeneo yanayoshindwa kufanya vizuri kwa kuboresha zaidi mazingira ya ufundishaji,kuweka walimu wa kutosha mashuleni na wenye sifa nzuri ,unategemea nini unapompangia mwalimu kufundisha masomo zaidi ya yale aliyojifunza chuoni kwenda kuyafundisha mashuleni,huo ujuzi wa masomo ya ziada kaupata wapi na hatimaye kuwezesha watoto washinde kwa alama za juu kuliko wale waliofundishwa na mwenye ujuzi kwa masomo husika?lazima atumie mbinu ili kutangaza jina lake na kuepuka vitisho iwapo mwanya unapatikana.

    Motisha kwa walimu hasa wanapokwenda kusimamia mitihani,per diem iwe nzuri ili kuwapunguzia vishawishi,lakini pia wapewe nafasi ndogo sana ya kukutana na wenyeji wao wanapokwenda kusimamia mitihani hiyo.
    Mh.Waziri napenda kutoa ombi iwapo inawezekana watoto waliopatikana na makosa wasamehewe na kuruhusiwa kurudia mtihani chini ya usimamizi mzuri na waliohusika kufanikisha uhalifu huo wachukuliwe hatua za kisheria iwe mfano kwa wengine wenye tabia kama hizo kwa kukwamisha maendeleo ya taifa.

    Natanguliza shukrani zangu za dhati.

     
  • Comment #2 (Posted by fortinatus mapera)
    Rating
    mor qualified teachers are to be employed in order to move up education
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.