MBUNGE wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), amekuwa kigogo wa kwanza kuzungumzia kashfa ya dawa za kulevya, ambayo inawahusisha watu maarufu nchini wakiwamo wanasiasa.
Azzan amesema kashfa hiyo ni kubwa na ya aina yake kuwahi kutokea hapa nchini, kwa sababu imewagusa viongozi wa serikali, wanasiasa, wafanyabiashara na watu wengine mashuhuri katika jamii, hivyo serikali inapaswa kuifanyia kazi haraka na kutoa msimamo wake kwa wananchi.
Mbunge huyo alisema pia kwamba, anazo taarifa kuwa jina lake ni miongoni mwa majina yanayodaiwa kuwamo katika orodha ya vigogo wanaohusishwa na biashara ya mihadarati, ambayo imewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Pamoja na kukiri kupata taarifa za namna hiyo kutoka kwa watu ambao hata hivyo hakuwataja, alisema bado hajaitwa kuhojiwa na chombo chochote.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima jana, Azzan alisema vyombo vya dola vinapaswa kuyafanyia kazi haraka madai hayo, na ripoti yake itangazwe kwa wananchi ili Watanzania wote waujue ukweli.
Bila kuingia katika undani wa suala hilo, Azzan alisema anao uhakika kwamba, siku moja siri iliyojificha nyuma ya kelele hizi za watu kushutumiana juu ya biashara hiyo haramu, itakuja kuwekwa bayana.
Azzan ambaye mara zote alionekana akizungumza kwa umakini na kwa kuchagua maneno ya kutamka, alisema alikuwa hayuko tayari kulizungumzia suala hilo kwa undani hivi sasa.
Hata hivyo, alisema litakuwa jambo zuri iwapo watu wote wanaohusishwa na biashara hiyo haramu, ambayo imegharimu afya na maisha ya vijana wengi, wakatajwa ili kuondoa hofu, wasiwasi na minong’ono inayozidi kusambaa katika jamii.
“Nimesikia jina langu limo kwenye orodha, lakini hizi ni habari za kusikia tu, hivyo siwezi kuzifanyia kazi au kuchukua hatua yoyote… Binafsi sijahojiwa na wana usalama au mtu yeyote kuhusiana na tuhuma hizi, lakini madai haya yamewaweka wengi roho juu.
“Sitaki kulizungumzia hili kwa undani maadam najifahamu vizuri kuwa sihusiki hata chembe na biashara hiyo, lakini nafikiri kuna haja ya lazima ya kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na wa kina, na ripoti ya uchunguzi huo itolewe kwa vyombo vya habari ili Watanzania wote wajue ukweli.
“Sina wasiwasi, nauhakikishia umma, ikibainika kuwa najihusisha na mihadarati, sheria ichukue mkondo wake, nikamatwe, nishitakiwe. Sio mimi tu, bali mbunge yeyote atakayebainika anahusika na biashara ya mihadarati, kwanza aondolewe bungeni, hastahili, kisha sheria ifuatwe kama kawaida,” alisema Azzan.
Mbunge huyo alisema akiwa mwanasiasa, anajua vyema kwamba anao maadui ambao miongoni mwao wako aliowaangusha katika kinyang’anyiro cha ubunge na wale ambao wanatarajia kuchukua nafasi yake mwaka 2010.
Kimantiki, hoja hiyo ya Azzan inafafana na ile iliyotolewa na Amina Chifupa na ikanukuliwa na gazeti hili katika toleo lake la Novemba 24, mwaka huu akieleza kwamba, vita yake dhidi ya mihadarati haina uhusiano wowote wa yeye kuwa na dhamira ya kutaka kugombea nafasi ya ubunge sehemu yoyote nchini.
Akizungumzia fedha alizonazo, Azzan alikiri kuwa ana utajiri wa kutosha, lakini akasema utajiri na pesa alizonazo, zina maelezo, na yuko tayari kuyatoa mahali popote yatakapohitajika.
Alifafanua kuwa, uwezo wa kipesa alionao unatokana na juhudi zake za kujiendeleza kibiashara jambo ambalo lilimpatia mafanikio makubwa akiwa mtoto mdogo wa darasa la sita, alipokuwa akiiba gari la baba yake na kuifanya teksi bubu nyakati za usiku.
“Sikatai kuwa nina pesa, ninazo, kuna watu wana pesa hapa mjini, lakini sio kwamba walizipata kwa kuuza madawa ya kulevya, hapana, kuna biashara nyingi halali ambazo kwa mtu makini aliyemaanisha kufanya biashara, kuinuka ni jambo rahisi tu.
“Mimi nimeanza kufanya biashara mwaka 1985, wakati huo nikiwa namiliki ‘Coaster Min Bus’, enzi hizo ikijulikana kwa jina la Luxury, iliyokuwa ikisafirisha abiria kati ya Pugu na Kariakoo, hiyo ndiyo biashara yangu ya kwanza. Mwaka 1987 nilinunua gari ya pili na mwaka 1988 nilikuwa mmoja wa vijana wadogo kabisa tulioomba mkopo wa kununua mabasi, niko kwenye biashara tangu wakati huo, kuna ajabu gani nikiwa na pesa?
“Na si hivyo tu, nakumbuka wakati nikiwa darasa la sita, baba yangu alikuwa na gari dogo, ambalo mimi nilikuwa na tabia ya kulichukua nyakati za usiku kwa njia ya kificho na kwenda kuifanya teksi bubu, nikiiegesha Mwembechai na wakati mwingine nikifuata abiria katikati ya jiji ilipokuwa Maggot,” alisema Azzan.
Alisema hashangai baadhi ya watu kumuhusisha na biashara ya mihadarati, kwa sababu wao wamejenga utamaduni wa kudhani kuwa vijana wote wanaopata mafanikio wanajihusisha na biashara hiyo.
Azzan ambaye aliingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka jana, alikanusha kutumia pesa nyingi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Alisema hakutumia pesa nyingi katika kampeni hizo na ushindi wake ulichangiwa na jinsi anavyokubalika katika jimbo la Kinondoni.
Hata hivyo, alikiri kuwa kuna tatizo kubwa la utumiaji na uuzaji wa mihadarati katika Wilaya ya Kinondoni.
Alisema tatizo hilo linafahamika na Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni imekwishaunda tume maalumu ya kuwasaidia vijana kuacha tumiaji wa dawa za kulevya.
Alisema tume hiyo iliundwa mwaka 2001 na yeye alikuwa mmoja wa wajumbe wake. Alisema kwa kutambua athari wanazozipata vijana kutokana na kutumia dawa za kulenya, alishiriki kikamilifu katika tume hiyo na walifanikiwa kuwaokoa vijana wengi kutoka katika utumiaji wa mihadarati.
Hivi karibuni, Tanzania Daima ilifanikiwa kuiona ripoti ya siri inayowataja vigogo wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya iliyowasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Ripoti hiyo ambayo imeanza kusambazwa katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi hapa nchini, ina majina ya vigogo wanaozidi 70.
Baadhi ya majina yaliyomo katika ripoti hiyo, ni ya wabunge sita, wote kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), miongoni mwao wakiwamo wale wanaotoka jijini Dar es Salaam.
Gazeti hili katika toleo lake la Ijumaa iliyopita, Desemba 8, lilidokezwa na mmoja wa watu waliojitambulisha kuwa waandaaji wa ripoti hiyo kwamba, wabunge wanaotajwa katika ripoti hiyo, waliweza kushinda ubunge katika uchaguzi wa mwaka jana kutokana na fedha walizovuna kwa kufanya biashara ya mihadarati.
Kwa mujibu wa mwandaaji huyo, wabunge hao sita ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa hoja iliyotolewa na mbunge mwenzao wa CCM, Amina Chifupa ya kujitoa mhanga kupambana na biashara hiyo, ikishindwa kupata nguvu ndani ya Bunge na nje.
Akizungumza na gazeti hili wiki kadhaa zilizopita, Chifupa alieleza kushangazwa kwake na taarifa zinazomtuhumu kwa kuwaripoti polisi, watu kadhaa kuwa ni wahusika wakuu wa biashara hiyo haramu.
Mwanzoni mwa mwezi Oktoba, wakati Rais Kikwete akizungumza na waandishi wa habari, alikiri kupokea orodha ya majina ya watu wanaodaiwa kuwa ni vigogo wa mihadarati.
Kikwete ambaye alikuwa akijibu swali kutoka kwa mwandishi mmoja wa habari alisema, alikuwa ameiwasilisha ripoti hiyo kwa vyombo dola ili kufanya uchunguzi juu ya suala hilo.
Katika majibu yake hayo, Kikwete alisema uchunguzi huo utasaidia kujua iwapo tuhuma hizo zina ukweli wowote au zilikuwa zikielekezwa kwa watu fulani kwa sababu zisizohusu dawa za kulevya.
Hivi karibuni, Waziri wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu, alisema, tayari vyombo vyake vilikuwa vimeshaanza kuifanyia kazi ripoti hiyo na kwamba, hakuna mtu atakayebainika kufanya biashara hiyo haramu atakayeachwa bila ya kuchukuliwa hatua.