Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Chonde IGP Mwema, usiruhusu polisi wabweteke
Chonde IGP Mwema, usiruhusu polisi wabweteke
By Habari Tanzania | Published  12/13/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

HAKUNA ubishi kwamba tangu Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, ateuliwe kuongoza Jeshi la Polisi kumekuwako na mafanikio makubwa katika kukabiliana na wimbi la uhalifu lililokuwa limegubika nchi.

Moja ya juhudi hizo ni kupungua kwa kiwango kikubwa kwa ujambazi wa kutumia silaha. Uporaji wa fedha katika mabenki ambao kwa hakika katika kipindi cha mwishoni mwa utawala wa awamu ya tatu na miezi ya mwanzo ya utawala wa awamu ya nne, ulikuwa ni jambo la kawaida, sasa umetoweka.

Tunaamini kujipanga upya kwa Jeshi la polisi kuliwezesha kupungua kwa kiwango kikubwa kabisa kwa matukio haya ya uhalifu. Hii ni kazi nzuri iliyofanywa, na tunaipongeza kwa dhati kabisa.

Jijini Dar es Salaam wananchi wameshuhudia doria za askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao wamesaidia kwa kiwango kikubwa kurejea kwa utulivu katika mitaa ya jiji. Askari si tu ni wengi zaidi mitaani, bali hata uitikiaji wa wito pale linapotokea jambo umekuwa ni wa haraka zaidi na unaofanana na kazi za kulinda maisha ya raia na mali zao.

Pamoja na mafanikio haya yote, ambayo kwa kweli hakuna anayeweza kuthubutu kuyabeza hasa ikizingatiwa hali ya usalama ilivyokuwa imedorora ndani ya nchi, matukio ya hivi karibuni ya uhalifu tena wa kutumia silaha yameanza kuwasilisha ujumbe mmoja kwa polisi wetu.

Kwamba baada ya mafanikio yote haya, sasa polisi wameamua kupumzika kidogo au tuseme wamejisahau kiasi cha kutoa mwanya kwa majambazi kuendesha vitendo vya uporaji kwa wananchi?

Yapo matukio makubwa ya uporaji wa kutumia silaha yaliyoripotiwa mkoani Kilimanjaro na Arusha, ukiachilia mbali tukio la Shinyanga ambalo lina zaidi ya wiki mbili tangu litokee kwa kijiji kizima kuporwa na majambazi ambao walidaiwa pia kuwabaka wanawake mbele ya waume wao.

Matukio haya yanaelezwa kuanza kuota mizizi kwa kile kinachodaiwa eti kukusanya fedha za Krismasi na mwaka mpya. Kwa bahati mbaya askari polisi mmoja ameuawa huko Arusha katika tukio la uporaji lililoua pia raia mmoja.

Matukio haya yanawezekana kuonekana madogo ikilinganishwa na huko nyuma tulikotoka, lakini jambo moja la msingi la kukumbuka ni kwamba moto unaoteketeza mahekari ya msitu mnene huanza kwa cheche moja tu.

Kwa maneno mengine si dalili njema kwamba wananchi wanaanza kusikia matukio haya ya ujambazi wa kutumia silaha, lakini kibaya zaidi wenye silaha wakifanikiwa kutoroka bila kutiwa nguvuni na vyombo vya dola.

Ni kutokana na kuanza tena kwa matukio haya, ikisingiziwa eti sasa ni msimu wa mwisho wa mwaka wa majambazi kutafuta fedha kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, tungependa kutoa rai kwa Jeshi la Polisi kutambua kwamba majambazi wana kawaida ya kupima upepo kama polisi wamelala au bado wapo macho katika kazi yao.

Matukio haya tuliyoyataja tunahofu yanaweza kuanza kuongezeka kwa kasi na baadaye tukarejea pale pale tulipokuwa mwaka huu ulipoanza ambao ilikuwa haipiti wiki bila kusikia mabilioni yameporwa benki au kwa mfanyabiashara au kwenye kituo cha mafuta, na pengine mabasi ya abiria kutekwa nyara na kuwapora kila walichokuwa nacho.

Jeshj la Polisi hadi sasa limekwisha kuonyesha kwamba linaweza kutekeleza wajibu wake ipasavyo, sasa isije ikawa kwamba wapo wachache ambao wameanza kubweteka na kusababisha hali hii inayoanza kusikika huko na huko. Tunamshauri IGP Mwema asema hapana kubweteka ndani ya Jeshi lake


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.