Na Gasper Andrew
POLISI mkoani Singida, inakusudia kuwafungulia mashitaka ya kijeshi askari wake wawili kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa ng’ombe 25, wenye thamani ya zaidi ya Sh7.5 milioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Celina Kaluba, alisema askari hao ni koplo mmoja na konstebo ambaye alikuwa akifanya kazi katika Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo.
Kamanda Kaluba alisema Novemba 16 mwaka huu, alipewa taarifa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Munang’ana, wilayani Singida, Yusuf Missanga juu ya kupotea kwa ng’ombe 25 waliokamatwa na wananchi wa kijiji hicho kisha kuwakabidhi kwa polisi.
Alisema mwenyekiti huyo alidai kuwa sungusungu wa kijiji chake waliwakamata ng’ombe hao pamoja na watuhumiwa wawili waliokuwa wanawachunga kwenye mbuga ya kijiji hicho Oktoba 28 mwaka huu.
Baada ya kuwakamata, walitoa taarifa kwa mkuu wa kituo kidogo cha polisi Sepuka, Singida Vijijini, ambaye alikwenda eneo la tukio na kuwachukua watuhumiwa siku iliyofuata.
Alisema licha ya kuondoka na watuhumiwa hao hadi Singida mjini, askari huyo alirudi tena kijijini hapo baada ya siku mbili akiwa na mwenzake pamoja na watuhumiwa hao.
Askari hao waliutaka uongozi wa kijiji kuwakabidhi ng'ombe hao kwa madai kuwa wametumwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Singida, Shilogile Kitambi ili ng'ombe hao wakatunzwe kwenye zizi la serikali Singida mjini hadi hapo atakapopatikana mwenye mali.
Kaluba alisema viongozi wa kijiji waliwakabidhi kwa maandishi ng'ombe hao, lakini hawakufika kwenye zizi la serikali wala kwa kwenye ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya.
Alisema imebainika kuwa tukio la wizi wa ng’ombe hao, halijaripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Sepuka wala katika ofisi ya OCD Singida hadi sasa.
Hata hivyo, Kaluba alisema baada ya kuwahoji askari waliokabidhiwa ng’ombe hao, wanaodaiwa ni mali ya Samweli Mahola wa kijiji cha Bukundi wilayani Meatu, wakati wote wamekuwa wakidai kuwa baada ya kuwafikisha katika ofisi ya OCD, aliwaamuru wamkabidhi ng’ombe hao kwa watuhumiwa.
Alisema askari hao wamedai kuwa walitii amri ya bosi wao na kukabidhi kwa maandishi ng’ombe hao kwa watuhumiwa ambao hawakuwa na kibali cho chote cha kuwamiliki.
Hata hivyo alisema baada ya kumwita OCD ambaye kwa sasa amehamia Muleba Mkoani Kagera, alikataa kata kata kulijua wala kulisikia tukio hilo kwa kipindi chote alichofanya kazi wilayani Singida.
Pamoja na kukataa kuhusika kwake katika tukio hilo, Kamanda Kaluba alisema wakati wao wakishughulikia askari hao, wengine waliohusika kwenye tukio hilo pia wanasubiri uamuzi kutoa makao makuu ya jeshi hilo juu ya OCD huyo.
Hili ni tukio la pili la baadhi wa polisi katika Wilaya ya Singida kuhusishwa na matukio ya wizi ndani ya mwezi moja.
Hivi karibuni askari moja alikamatwa kwa tuhuma za kuiba madumu 10 tupu ya kuwekea mafuta ya alizeti. Kaluba amesema anatarajia kutoa uamuzi uliofikiwa juu ya askari huyo wakati wowote kuanzia sasa.