Na Mwandishi Wetu, Moshi
INAWEZEKANA likiwa ni moja ya matukio adimu kutokea baada ya kundi la nyuki kuvamia eneo la msiba na kuwashambulia masheikh na waombolezaji ambao walilazimika kutimua mbio kuokoa maisha yao.
Tukio hilo ambalo limekuwa gumzo mjini hapa, lilitokea juzi saa 8.30 mchana mtaa wa Dar es Salaam, wakati waombolezaji wakisubiri maakuli baada ya kumaliza mazishi
Athuman Hamisi ambaye ni mtoto wa marehemu Hamisi Abdallah (64) aliyefariki Jumapili kwa ugonjwa wa kansa ya koo, jana alihibitisha kutokea kwa tukio hilo.
"Watu walikuwa wanakuja kwa makundi na bila kujua walipita eneo lenye nyuki, wakaanza kushambuliwa nao wakakimbilia huku nyumbani ndio wakawaleta kwa hiyo ikawa mshikemshike," alisema.
Hamisi alifafanua kuwa waombolezaji waliokuwepo nyumbani hapo nao walijaribu kuokoa maisha yao lakini bila kujua nyuki walikuwa wakitokea wapi nao wakakimbilia kulekule walikotokea nyuki hao na kuzidisha tafrani hiyo.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni pamoja na mtoto huyo wa marehemu ambaye alishambuliwa usoni na Levina Mtenga ambaye ni mama mjamzito ambaye aliokolewa na wasamaria wema.
Hata hivyo alisema hawezi kukumbuka majina ya ndugu na marafiki waliojeruhiwa katika mkasa huo lakini akasisitiza walikuwa saba, na watano walitibiwa Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi na kuruhusiwa.
"Mtaa wote ulikuwa ni nyuki mpaka mitaa ya jirani na hadi sasa (jana) unaona bado kuna nyuki tunapambana nao japo si wengi kama wa jana (juzi)," alifafanua Athuman.
Alimtupia lawama mkazi mmoja wa mtaa wa jirani na kwake kwa kuendelea kufuga nyuki hao kiasi kwamba wamefikia hatua ya kutaka kuangusha dari la chumba chake lakini hachukui hatua yoyote.
Kwa mujibu wa Athuman, suala la kuwepo kwa nyuki hao linafahamika muda mrefu hadi maafisa wa Idara ya Nyuki waliwahi kufika eneo hilo na kuahidi kuwaondoa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.
Waandishi wa habari wawili, jana walipata wakati mgumu kuifikia nyumba yenye msiba kutokana na eneo hilo kuendelea kuzagaa nyuki hao na hivyo kutishia maisha ya watu.
Mwananchi lilishuhudia eneo hilo likiwa katika hali ya wasiwasi ambapo watu walionekana wakipita mitaani wakiwa wamejifunika kwa kanga, taulo na vitambaa ili kukabiliana na nyuki waliokuwa bado wamezagaa eneo hilo.
Habari zilizowakariri walioshuhudia tuki hilo, zilidai kuwa nyuki hao walianza kuwashambulia masheikh na wapishi kabla ya kuhamia kwa waombolezaji wengine ambao walilazimika kutimua mbio.
Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo, Awadhi Said, alimtaja mwanamke mwingine aliyejeruhiwa kuwa ni Hadija Bomoabomoa, ambaye aliokolewa kwa kumwagiwa ndoo nzima ya dawa ya kuulia wadudu.
Jitihada za waandishi wa habari kupata wasemaji katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi jana zilishindikana baada ya kuelezwa kuwa viongozi wote walikuwa wamekwenda hospitali ya rufaa ya KCMC kwenye mkutano.
Ingawa wasemaji hao hawakuweza kupatikana, lakini mlinzi mmoja wa hospitali hiyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa majeruhi waliokuwa wamelezwa hospitalini hapo waliruhusiwa jana asubuhi