Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tanzania yapeleka majeshi Lebanon
Tanzania yapeleka majeshi Lebanon
By Habari Tanzania | Published  12/13/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Tanzania imepeleka wanajeshi 77 nchini Lebanon kwa ajili ya kuungana na wanajeshi wengine watakaounda jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini humo.

Hata hivyo, wanajeshi wanaokwenda Lebanon ni Polisi wa Jeshi (Military Police) ambao tayari wamekwisha kupata mafunzo pamoja na maandalizi ya vifaa kwa ajili ya kazi hiyo.

Rais Jakaya Kikwete, jana alikagua maandalizi ya askari hao wanaokwenda kuungana na wenzao kutoka nchi mbalimbali duniani kulinda amani nchini Lebanon.

Polisi Jeshi hao wanaojumuisha maafisa 11 na askari 66, wanatoka katika Kombania ya 603 ya Polisi Jeshi katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyoko Ukonga jijini Dar es Salaam. Kati yao, wapo wanawake 10 ambao ni afisa mmoja na askari 9.

Akizungumza na maafisa na askari hao mara baada ya kuona zoezi fupi la majukumu wanayokwenda kufanya, pamoja na kukagua vifaa, Rais Kikwete alisema maafisa na askari hao, ni vema wakatambua kwamba wamepewa heshima kubwa ya kwenda kuiwakilisha Tanzania na JWTZ katika kazi ya kulinda amani.

"Kuna mambo matatu ambayo nataka myatambue, kwanza mmepewa heshima kubwa nyinyi binafsi ya kwenda kushiriki zoezi hili, na mkifanya vizuri mtapata sifa, wenzenu watawasifia na kusema kumbe Watanzania ni wazuri," alisema

Alisema kwa kwenda kwao kushiriki zoezi hilo, ni heshima kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiombwa kwenda kushiriki shughuli za kulinda amani. Alisema utendaji wao mzuri utatoa fursa zaidi kwa JWTZ kushiriki katika mazoezi hayo.

"Na jambo la tatu mtambue kwamba mnabeba heshima ya Tanzania nzima na hili si jambo geni kwenu. Sina wasiwasi kwamba mtafanya kazi vizuri na nchi itapata heshima na jeshi litapata heshima. Nawatakia kazi njema."

Akitoa nasaha hizo mbele ya Mkuu wa Majeshi General George Waitara, Naibu Waziri wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Omar Yussuf Mzee na maafisa wengine wa JWTZ, Rais aliwasisitiza maafisa na askari hao kwamba wanakwenda nchi ya watu na ugenini na hivyo ni lazima wakaishi vizuri na askari kutoka nchi nyingine.

Aliwataka pia askari hao kuishi vizuri na raia wa Lebanon huku wakichukua tahadhari kubwa ya kutoingia mitaani na kuanza kufanya urafiki na raia au kufanya miradi itakayoleta aibu kwa jeshi na nchi.

Alisema uamuzi wa Tanzania kutoa kikosi hicho cha Polisi Jeshi kwenda kulinda amani nchini Lebanon umetokana na maombi yaliyowasilishwa kwake na Umoja wa Mataifa ya kuitaka Tanzania kushiriki katika shughuli za kulinda amani.

Alibainisha kwamba kwa muda mrefu, Umoja wa Mataifa umekuwa ukiiomba Tanzania kutoa vikosi vyake, lakini Tanzania pamoja na nia nzuri na ahadi ya kushiriki katika shughuli hizo, ilishindwa kufanya hivyo kutokana na ukata.

Alisema Tanzania inapewa nafasi na heshima kubwa na inaaminiwa kuwa ni nchi makini ambayo inapaswa kushiriki katika shughuli za kulinda amani duniani.

Aliwahakikishia maafisa na askari hao na JWTZ kwamba serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuwapatia mahitaji yote wanayohitaji ili kurahisisha utendaji na majukumu yao wakiwa Lebanon.

Akitoa taarifa fupi ya maandalizi ya kikundi hicho, Mkuu wa Majeshi, Jeneral George Waitara, alimweleza Rais kuwa JWTZ pamoja na kutoa maafisa na askari hao 77 pia limeandaa na kutoa malori manne yenye uzito wa tani tano yakiwa yamefungwa vifaa vyote vya mawasiliano na kupakwa rangi nyeupe na nembo ya UN.

Alisema JWTZ pia imetoa magari 17 aina ya Landrover, mbwa wawili kwa ajili ya shughuli za kunusa mabomu, vifaa vya malazi, burudani na fedha za awali za kujikimu kwa maafisa na askari hao.

Jenerali Waitara allisema gharama zote za maandalizi ya maafisa askari na vifaa hizo zimetolewana jeshi lenyewe, na kwamba zitarejeshwa na Umoja wa Mataifa.

Alieleza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa JWTZ kupeleka askari wake nje wa bara la Afrika na kwamba hatua hiyo ni changamoto kubwa wa jeshi.
Aidha alisema wakaguzi kutoka Umoja wa Mataifa wameridhishwa na maandalizi ya maafisa na askari hao, pamoja na vifaa vilivyotolewa na jeshi hilo.

Moja ya majukumu ya Polisi Jeshi hao 77 litakuwa ni kutoa ulinzi kwa askari wenzao wapatao 9,000 kutoka nchi sita ambao tayari wako nchi Lebanon.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.