Na Mwandishi Wetu
MGOGORO kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) umeingia hatua mpya na sasa Mkemia Mkuu wa Serikali anahusishwa.
Tanesco ndiyo imechukua hatua ya kuifikisha kampuni hiyo kwa Mkemia Mkuu wa serikali ili kutafuta usahihi wa gesi hiyo inayodaiwa kuwa na mchanga.
Taarifa ya Tanesco kwa vyombo vya habari ilisema jana kuwa imepeleka sampuli ya mabaki ya uchafu unaodaiwa kuwa ulikuwa kwenye gesi na kuupeleka kwa Mkemia Mkuu, ili baada ya uchunguzi, aweze kutoa taarifa sahihi iwapo uchafu huo ulitokana na gesi hiyo ama uchafu ulio ndani ya mabomba au mitambo ya kampuni hiyo.
"Tanesco imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa uchafu unaochujwa kwenye vichujio vya Songas na Aggreko una rangi nyeusi, wakati ule wa Richmond una rangi ya kahawia (brown)," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia imedai kwamba Richmond iliagiza vifaa vya kuchujia gesi kutoka Marekani kwa ajili ya mitambo yake ya megawati 20, lakini bado havijafika wanakofunga mtambo wao.
"Uagizaji huo unafuatia makubaliano kati ya Tanesco na kampuni hiyo kuwa lazima Richmond ifunge vifaa hivyo vya kuchuja gesi kabla ya kuzua madai ya gesi chafu. Hivi sasa Richmond inaendelea na utayarishaji wa sehemu vifaa hivyo vitakapofungwa," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Kampuni ya Richmond juzi iliibebesha Tanesco lawama kwamba ndiyo kikwazo cha wao kuanza kuzalisha umeme kama ilivyopanga kutokana na kupewa gesi chafu.
Makamu wa Rais wa Fedha na Utawala wa kampuni hiyo, Zahoor Gire, alinukuliwa akisema kwamba ingawa wamefanikiwa kufunga mitambo yao tayari kwa kuzalisha umeme, juhudi zao zimekwamishwa na Tanesco ambao wanawapa gesi yenye mchanga.
“Wakati wa majaribio ya kawaida ya wahandisi wa Richmond Development Corporation, waligundua kwamba gesi waliyopewa na Tanesco haikufikia viwango vya mtambo,” ilisema sehemu ya taarifa ya Richmond juzi.
Gire alisema kwamba kuwasha jenereta kwa kutumia gesi yenye mchanga iliyotolewa na Tanesco, inaweza kuharibu mitambo na hivyo kuleta hasara ya muda na fedha kwa serikali.
Pia alisema RDC imechukua tahadhari zote kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama na upatikanaji wa umeme wa dharura wa uhakika ili kutatua tatizo la umeme nchini, “lakini sasa mafanikio ya juhudi zetu yanategemea Tanesco kutupa gesi safi.”
Kutokana na hali hiyo, taarifa hiyo ilisema kwamba Richmond sasa inasubiri ratiba kutoka Tanesco itakayoainisha vipi na lini gesi safi na ya kutosha itapatikana.
Katika taarifa ya Tanesco ya jana, imeitaka Richmond kuacha visingizio na kutekeleza wajibu wake wa kuzalisha megawati 20 za umeme.
"Pamoja na ukweli kuwa mkataba ulisainiwa kati ya Richmond na Tanesco, lakini kampuni inayopaswa kuipa Richmond gesi ni Kampuni ya African Energy. Kampuni hiyo ndiyo inayozipa gesi Kampuni za Songas na Aggreko na kampuni hizo hazijawahi kulalamika kuwa gesi wanayopewa ni chafu na inakwamisha kazi ya uzalishaji umeme wao," inasema.
Ilisema kwa kuwa kuwapo mabaki ya uchafu kwenye gesi ni jambo la kawaida, Tanesco iliarifu Richmond kununua vichujio kwa ajili ya kuchuja mabaki hayo kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.