Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Ngara watahadharisha Rwanda, Burundi kujiunga A.Mashariki
http://www.habaritanzania.com/articles/23/1/Ngara-watahadharisha-Rwanda,-Burundi-kujiunga-A.Mashariki
By Habari Tanzania
Published on 05/2/2006
 
Katika ziara yake mkoani Kagera hivi karibuni, Waziri Mkuu Edward Lowassa alipokea kilio cha wazee wa mkoa huo kuhusu tatizo la wahamiaji haramu, mifugo pamoja na hofu ya kujengwa kwa himaya ya kimataifa ya nguvu ya Watutsi katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu.

Katika ziara yake mkoani Kagera hivi karibuni, Waziri Mkuu Edward Lowassa alipokea kilio cha wazee wa mkoa huo kuhusu tatizo la wahamiaji haramu, mifugo pamoja na hofu ya kujengwa kwa himaya ya kimataifa ya nguvu ya Watutsi katika ukanda wa nchi za Maziwa Makuu.
 
Wakati nchi za Rwanda na Burundi zikisubiri kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, wazee wilayani Ngara mkoani Kagera wanalo jambo la kutahadharisha.
 
Wanaeleza kwamba mara nchi hizo zikiungana na Uganda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, zitapata nafasi ya kumiliki miradi muhimu kwani watawashinda Watanzania na Wakenya.
Kwa maoni yao, wazee hao wanasema mipango ya Rwanda na Burundi kujiunga katika Jumuiya hiyo ni hatari kwa taifa.
 
’’Usalama wa nchi kwa miaka ijayo hautabiriki kwa vile suala la wahamiaji haramu toka nchi ya Rwanda kwa ushirikiano na nchi jirani zake zimejiwekea malengo ya kutawala nchi za Maziwa Makuu,’’ anasema Mzee Richard Bgoya,85, wakati akisoma risala ya wazee wa wilaya ya Ngara mbele ya Waziri Mkuu Edward Lowassa.
 
Wanasema nchi hizo, zina mpango wa siri wa kuanzisha mfumo wa utawala wanaouita Tutsi International Power.
 
Waziri Mkuu Lowassa alifanya ziara ya kwanza ya kikazi mkoani humo, kuanzia Aprili 20 hadi 24 tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete mwishoni mwa mwaka jana kushika wadhifa huo.
 
Ziara hiyo pamoja na mambo mengine ilikuwa ikichochea chachu ya maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo.
 
’’Tunatoa tahadhari kwa viongozi wa ngazi za juu na kati na pia viongozi wa CCM kuwa makini na watu hao,’’ inasema sehemu ya risala hiyo.
 
Wanaeleza kwamba kwa Tanzania hawatapigana vita vya bunduki kama wafanyavyo Kongo, isipokuwa wanatumia mbinu kuhamishia watu wao mkoa wa Kagera, kwa malengo kuwa wakiisha kuchukua makazi na watoto wao kusoma ndani ya nchi hii, wataweza kujipenyeza na kutawala nchi hii hata kama ni miaka 100 ijayo.
 
Wazee hao wanaishauri Serikali kuwa makini katika mpango mzima wa kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi katika muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Kwa hali hiyo,Wazee hao wanapendekeza kuwa Serikali itumie Jeshi la Wananchi kuwaondoa wahamiaji wote haramu walioingia nchini tangu mwaka 1995 na wanaoendelea kuingia.
 
Pia wanasema Serikali ifanye uchunguzi wa kina kwa wale wanaofanya kazi serikalini, kwa kuwa Wanyarwanda hufanya mipango ya kuwaozesha binti zao kwa viongozi wa Serikali ili kupata taarifa mbalimbali za nchi.
 
Wanasema Wanyarwanda walioajiriwa katika vyombo vya dola, wataweza kutumiwa na wenzao na watauza habari za nchi na watakuwa vizuizi vya habari muhimu zinazowahusu na nyingine kuhusu usalama wa nchi jirani zisiwafikie viongozi wa hapa.
 
Kilio cha wazee hao, kinatokana na kukithiri kwa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Rwanda na Burundi na wahamiaji haramu pamoja na mifugo yao kutoka nchi hizo na Uganda.
 
Wakimbizi hao wameingia nchini kuanzia mwaka 1962. Tangu wakati huo hadi sasa, baadhi ya wakimbizi na watoto wao walibahatika kusoma na kuajiriwa na Serikali katika vyombo muhimu vya dola.
 
Hata hivyo anasema, wapo raia wengine wa Rwanda, Burundi na Uganda ambao ni wahamiaji haramu wanajifichaficha na mifugo yao katika mapori ya mkoani humo, kwamba watasakwa na kurejeshwa makwao kwa nguvu.
 
Licha ya kero ya uporaji na vitendo vya ujambazi, wahamiaji haramu wanaingia nchini wakiwa na makundi mengi ya mifugo ya ng’ombe ambao huwafugia katika mapori ya hifadhi za mbuga za wanyama Burigi, Kimisi, Kyaka na sehemu zingine mkoani humo.
 
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Enos Mfuru anasema kwa mfano, mwaka 2005 kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa miguu na midomo katika wilaya za Muleba, Bukoba na Biharamulo.
 
Aidha anasema ugonjwa wa homa ya chambavu ulitokea katika wilaya za Biharamulo na Karagwe na kwamba kusambaa kwa magonjwa haya, kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na uvamizi wa wafugaji wahamaji toka nchi jirani, pamoja na wafugaji wenyeji wahamaji.
 
Katika kudhibiti ugonjwa huo, Kanali Mfuru anasema mkoa wake ulianzisha zoezi maalumu kwa kuwahusisha Idara za Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Mshauri wa Mgambo, Mifugo, TRA , viongozi wa kata na vijiji la kuwakamata katika wilaya za Karagwe, Muleba, Bukoba na Biharamulo.
 
Katika zoezi hilo la kuwakamata wahamiaji haramu, Mkuu wa Mkoa ameahidi kwamba litakuwa la kudumu.Tayari wahamiaji na ng’ombe wao wapatao 36,044 wamerudishwa katika nchi walizotoka na kwamba Serikali Kuu na Halmashauri zimekusanya ushuru mbalimbali wa kiasi cha Sh. 300,441,000.
 
Akitoa takwimu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kapteni mstaafu John Chiligati anasema mkoa wa Kagera una wahamiaji haramu 76,353.
 
Anasema wilaya ya Bukoba inao wahamiaji haramu wapatao 5,002, Karagwe 67,755, Biharamulo 1,035, Ngara 1,400 na Muleba 1,161.
 
Aidha anasema wakimbizi wote wamekwisharejeshwa makwao isipokuwa 46,000 waliosalia katika makambi ambao wanatarajiwa kurudishwa hivi karibuni.
 
Waziri Chiligati anawashukuru wakazi wa mkoa huo kwa ukarimu wao wa kuwapokea wakimbizi, licha ya adha kubwa ambayo wameipata kutokana na wakimbizi hao.
 
Baadhi ya wakimbizi walikuwa wakitoka katika makambi yao na kwenda maeneo wanayoishi raia wa kawaida kufanya uhalifu wa kupora mali, fedha na mifugo hali ambayo imewafanya wakazi wa mkoa huo kuwaangalia wakimbizi katika sura ya ujambazi zaidi.
 
Mkuu wa wilaya ya Muleba, Bw. John Tuppa anasema licha ya kufanya vitendo vya ujambazi na uporaji,wahamiaji haramu kutoka Rwanda na Burundi wamekuwa wakiwateka wakazi wa wilaya yake, na kuwafanya kuwa makuli wa kubeba mizigo yao hadi mpakani ambako huwaacha.
 
Anasema pamoja na juhudi za serikali ya wilaya yake kuwanasa na kuwarejesha makwao wahamiaji haramu, zoezi hilo linakwamishwa na baadhi ya maafisa ubalozi wanaokwenda wilayani humo kuwatetea bila kuwasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
 
Katika uwanja wa mashujaa wa Bunazi wilayani Misenyi, Waziri Mkuu Lowassa alitoa msimamo wa Serikali kuwa wahamiaji wote haramu watarejeshwa makwao.
 
Anafafanua kwa makini kuwa hatua ya kuwarejesha wahamiaji haramu makwao haina maana ya kuwa na ugomvi na nchi majirani.
 
’’Hatuna ugomvi na majirani zetu, tunaendelea kushirikiana nao vizuri na katika vikao vya ujirani tulikubaliana wahamiaji haramu na mifugo yao warudishwe makwao?Tanzania sio shamba la bibi ambalo kila mtu anaweza kuja kufanya analotaka,’’ anasema.
 
Akiwa katika wilaya ya Biharamulo, mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Serengo Mrengo anasema baadhi ya watendaji wa vijiji wamekuwa wakiwapa vibali feki, raia wa nchi jirani ili waweze kuishi nchini.
 
Baadhi ya wananchi katika wilaya hiyo walimlalamikia Waziri Mkuu Lowassa kwamba watendaji hao wa vijiji wamekuwa wakiuza vibali hivyo feki na kumegewa vipande vya ardhi vya kuishi kwa Sh. 10,000.
 
Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Mkuu Lowassa anasema Serikali itahakiki hati za kuishi kwa raia wa kigeni na wale ambao watabainika kuwa na vibali feki watarejeshwa makwao.
Anasema Serikali imedhamiria kufanya zoezi hilo hivi karibuni.
 
Kwa upande wake, Balozi wa Uganda nchini, Bw. Ibrahim Mukiibi anasema hakuna mtu atakubaliwa kuharibu uhusiano kati ya Watanzania na Waganda.
 
Balozi Mukiibi anaunga mkono msimamo wa Serikali ya Tanzania kuwarejesha makwao wahamiaji haramu hatua ambayo anasema itaimarisha uhusiano kuwa wahamiaji haramu wanakiuka sheria.
 
Anawashukuru Watanzania kwa kuwasaidia viongozi wa sasa wa Uganda kuundoa utawala katili.
 
Anasema kama alama ya undugu na urafiki kati ya nchi hizo, Serikali yake imejenga shule ya sekondari ya kisasa katika kijiji cha Muhutwe wilayani Muleba sehemu ambako Rais Yoweri Museveni wa Uganda alikuwa akiishi wakati wa mapambano ya kuuondoa utawala katili.
 
Akijibu risala hiyo, Waziri Mkuu Lowassa anasema, ’’mengi mliyosema tunakiri na tutayazingatia.’’
 
Anasema Watanzania watapata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu Jumuiya hiyo baadaye mwaka huu ambapo suala la Rwanda na Burundi pia litajadiliwa.
 
SOURCE: Nipashe