Na Mwandishi Wetu POLISI mkoani Morogoro wamedai kuusambaratisha kabisa utandao wa ujambazi baada ya kumkata mtuhumiwa wa mwisho ambaye walikuwa wakimsaka kwa udi na uvumba.
Mtuhuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa mkazi wa Mjipya katika Manispaa ya Morogoro, alikamatwa Ijumaa iliyopita alfajiri wakati ameweka mitego yake ya kuwanasa wapita njia kwenye kilabu cha pombe za kienyeji cha Kaloreni kilichopo jirani na makazi yake.
"Mtuhumiwa huyu amekuwa akisakwa kwa muda mrefu sasa kutokana na matukio mbalimbali ya uporaji wa kutumia silaha... alikuwa amebaki peke yake baada ya kuvunjwa kwa mtandao wao, akiwepo kaka yake ambaye alishakamatwa na kesi yake ipo mahakamani," alisema jana Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro, Hemedi Msangi wakati akizungumza na waaandishi wa habari ofisini kwake.
Baada ya kukamatwa, inadaiwa kuwa, mtuhumiwa huyo aliwaelekeza polisi maeneo ambako alikuwa akiuza vitu mbalimbali alivyokuwa akipora na kukamata baiskeli 11.
Mtuhumiwa huyo inadaiwa kuwa anamiliki bunduki ambayo hadi sasa bado haijapatikana na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini mahali ilipo.
Wakati huo huo; watu nane wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukamatwa na nyaya za umeme mali ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Mkoa wa Morogoro
Watu hao walikamatwa Desemba 8, majira ya alfajiri katika maeneo ya Mafisa na barabara ya Uhuru mjini hapa, wakiwa na nyaya hizo nyumbani kwao.
Miongoni mwa watu hao, ndugu wawili ambao ni wanunuzi wa nyaya hizo, wakazi wa Mtaa wa Uhuru na wengine ni walioiba, wakazi wa Mafisa.