Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Richmond Development Corporation (RDC) imelibebesha Shirika la Umeme (Tanesco) lawama kwamba ndiyo kikwazo cha wao kuanza kuzalisha umeme kama ilivyopanga kutokana na kupewa gesi chafu.
Kauli ya Richmond imo kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotoa jana jioni, ikiwa ni siku ya tano sasa kampuni hiyo imeshindwa kutekeleza ahadi yake ya kuzalisha umeme wa megawati 20 na kuunganisha kwenye gridi ya taifa tangu Ijumaa iliyopita.
Katika taarifa hiyo, Makamu wa Rais wa Fedha na Utawala wa kampuni hiyo, Zahoor Gire, amenukuliwa akisema kwamba ingawa wamefanikiwa kufunga mitambo yao tayari kwa kuzalisha umeme, juhudi zao zimekwamishwa na Tanesco ambao wanawapa gesi yenye mchanga.
“Wakati wa majaribio ya kawaida ya wahandisi wa Richmond Development Corporation waligundua kwamba gesi waliyopewa na Tanesco haikufikia viwango vya mtambo,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya ukurasa mmoja.
Gire alisema kwamba kuwasha jenereta kwa kutumia gesi yenye mchanga iliyotolewa na Tanesco, inaweza kuharibu mitambo na hivyo kuleta hasara ya muda na fedha kwa serikali.
Pia alisema RDC imechukua tahadhari zote kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama na upatikanaji wa umeme wa dharura wa uhakika kutatua tatizo la umeme nchini, “lakini sasa mafanikio ya juhudi zetu yanategemea Tanesco kutupa gesi safi.”
Kutokana na hali hiyo, taarifa hiyo ilisema kwamba Richmond sasa inasubiri ratiba kutoka Tanesco itakayoainisha vipi na lini gesi safi na ya kutosha itapatikana.
Gire amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema kwamba mara baada ya wahandisi wake kugundua hitilafu hiyo katika gesi, waliwataarifu rasmi Tanesco, hasa wakisukumwa na uelewa wao kwamba umeme wa dharura unahitajika sana kwa sasa.
Akizungumzia malalamiko ya Richmond, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Daniel Mshana, alithibitisha kuyapata na kwamba waliwajibu jana.
Mshana alisema kwamba Richmond walielezwa tangu mapema kwamba wanatakiwa kufunga kifaa cha kuchuja gesi hiyo kama walivyofanya wenzao wa Aggreko kama mkataba baina yao unavyoelekeza.
“Kulingana na mkataba Richmond wanapaswa wa-provide filters za kuchuja hiyo gesi, hili si jukumu la Tanesco,” alisema Mshana.
Alisisitiza kwamba mwenye jukumu la kutoa gesi kwa Richmond si Tanesco bali ni Songas. Songas ni kampuni inayosafirisha gesi kwa bomba kutoka Songosongo hadi jijini Dar es Salaam na pia kufua umeme wa gesi katika mitambo yake iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, taarifa za ndani ambazo Mwananchi inazo zinaeleza kwamba mkataba wa Tanesco na Richmond umetoa jukumu la kutoa gesi kwa Tanesco na si kwa Songas.
Malalamiko haya ya Richmond yanafungua ukurasa mpya wa rekodi yake ya utekelezaji wa mkataba baina yake na Tanesco ambao ulisainiwa Juni 23, mwaka huu ukiipa (Richmond) jukumu la kuzalisha umeme wa megawati 100.
Baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, iliwachukua Richmond hadi Oktoba 29, mwaka huu kuwasilisha nchini mitambo yake ya awali ya kuzalisha megawati 20 za awali.
Kulingana na mkataba huo, kazi nzima ya usafirishaji, ufungaji hadi kuwasha mitambo inatakiwa ikamilike katika kipindi cha siku 150, ikiwa imekamilisha uzalishaji wa megawati 100.
Richmond awali ilisema kwamba ilikuwa inatafuta ndege kubwa za kukodi kusafirisha mitambo yake ambayo ilidai ilikuwa ikihitaji ndege kubwa sana za mizigo ambazo hazipatikani kirahisi.
Mitambo hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Marekani ambako kampuni hiyo ina makao yake makuu. Kampuni hiyo imeandikishwa Houston, katika Jimbo la Texas nchini Marekani.
Hadi sasa wananchi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuona mitambo ya Richmond ikiwashwa ili walau kupunguza makali ya mgao mkali wa umeme ambao sasa unafanyika hata saa za usiku.
Hali ya kukosekana kwa umeme wa uhakika ilianza kujitokeza mapema mwaka huu na mgawo wa kwanza kutangazwa Februari mwaka huu.
Mabwawa ya maji ya Kidatu, Kihansi na Mtera, yamo katika hali mbaya kutokana na kukosa maji baada ya mvua kutokunyesha. Uzalishaji wa umeme wa nguvu za maji umepungua baada ya kufungwa kwa mabwawa na mengine kuzalisha chini ya kiwango chake.
Richmond kama walivyo Aggreko, walipata zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kutumia gesi lakini hadi sasa ni Aggreko tu ambayo imeweza kutekeleza jukumu lake.