Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Mzee Mwanakijiji  »  Tunauliza kwa nini?
Tunauliza kwa nini?
By Mzee Mwanakijiji | Published  12/12/2006 | Mzee Mwanakijiji | Rating:
Na HabariTanzania.com

Tumeuliza kwanini, jawabu lake ni nini,
Tuambiwe ndiye nani, aliyesaini kwa nini,
Jawabu lake ni nini, aliyeanza ni nani,
Vyetu vya kwao kwa nini, vyao si vyetu kwanini?


Wameyauza madini, kama njugu za sokoni,
Wachangamkia wageni, tumebaki maskini,
Kumikumi mifukoni, watutambia wahuni,
Vyetu vya kwao kwa nini? vyao si vyetu kwanini?


Umeme nao kwa nini, twashinda kujiamini,
Richmondi kina nani, dili lao ni la nini,
Huyo Gire ndiye nani, wanamlinda kwa nini?
Vyetu vya kwao kwa nini? vyao si vyetu kwanini?


Mmeziuza kwa nini, nyumba zetu gulioni,
Mmepanga hotelini, tunauliza kwanini,
Mtazirudisha lini, wa kwanza awe ni nani,
Vyetu vya kwao kwa nini? vyao si vyetu kwanini?


Mwakatazana bungeni, kuleta hoja kwa nini?
Eti mambo ya chamani, hiyo siri ni ya nini,
Mlishika mkononi, kiapo chenu cha nini?
Vyetu vya kwao kwanini? vyao si vyetu kwanini?


Kikwete sema ni nani, wamekupatia nini,
Wamekupa kitu gani, unamuogopa nani,
Tuambie ni wa kwanini, watetema bila soni,
Vyetu vya kwao kwa nini? vyao si vyetu kwa nini?


Watu wamekuamini, kuwatoa mashakani,
Wamebakia gizani, wanauliza kwa nini,
Kila siku safarini, unamkimbia nani,
Vyetu vya kwao kwa nini? vyao si vyetu kwanini?


Mipango yenu ni nini, kuleta matumaini,
Porojo nyingi kwa nini, maneno tele vinywani,
Tumechoka samahani, tupeni jibu jamani,
Vyetu vya kwao kwa nini? vyao si vyetu kwanini?


Mtu huuliza nini, apewe jibu yakini,
Yalojili mafichoni, yawekeni hadharani,
Kalamu naweka chini, jibu lenu natamani,
Vyetu vya kwao kwanini? vyao si vyetu kwanini?


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.