Na Paulina David
GHARAMA za mradi wa kupelekea maji ya Ziwa Victoria wilayani Kahama na Shinyanga zimeongezeka kutoka Sh210 bilioni hadi Sh225 bilioni.
Waziri wa Maji, Dk Shukuru Kawambwa, amefahamisha hayo kwenye majumuisho
ya ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo ya maji iliyofanyika katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema mradi huo sasa unataraji kugharimu kiasi hicho badala ya kile cha awali, ikiwa ni Sh15 bilioni zaidi, baada ya kuongezeka kwa maeneo ambayo hayakuwa kwenye mpango wa mradi, kujenga uzio kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya uhalifu wilayani Misungwi, Mkoa Mwanza.
Waziri alizitaja shughuli nyingine ambazo hazikuwemo kwenye mradi, lakini zinatakiwa
kutekelezwa kuwa ni ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo la mradi na nyumba mbili za watu watakaokuwa wanafanya shughuli ya kwenda kuendesha mitambo.
Alisema kuwa vitu hivyo vimelazimika kuongezwa kwa kuwa ni vitu muhimu, ingawa wakati wa tathimini ya awali juu ya utekelezaji wa mradi huo havikuwemo.
Waziri huyo alisema kuwa pamoja na ongezeko la gharama za mradi huo, mwezi Septemba na Oktoba mwakani vijiji 54 vya mikoa ya Mwanza na Shinyanga vitaondokana na tatizo la maji, kwa kuwa mradi huo utakuwa umeishakamilika na kukabidhiwa kwa serikali.
Alisema kuwa kulingana na hali aliyoiona, kazi inayofanywa na makandarasi wanne inaridhisha na mkandarasi namba tano, National Contract Company, anayetoa
umeme kutoka Bulyanguru hadi Ihelele, atakamilisha usambazaji wa umeme Septemba
mwakani kutokana na kuchelewa kuanza kazi hiyo.
Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC)
inajenga mtambo wa kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo cha maji hadi kwenye tanki kuu umekamilika kwa asilimia 98 na asilimia iliobaki inasubiri
umeme ili iweze kukamilika.
Kampuni ya CCECC inayojenga mtandao wa kusambaza mabomba kutoka Kijiji cha Sola hadi Shinyanga imekamilisha kwa asilimia 80, wakati Kampuni ya Sinohydro Corporation ambayo imekwisha kabidhi kazi moja tangu mwezi uliopita, sasa inadaiwa kazi nyingine ambayo imekamilika kwa asilimia 50.
Kutokana na hali hiyo, waziri huyo aliagiza mkandarasi huyo atekeleze mradi wake na kuukabidhi kabla ya Juni,mwakani kwani sababu aliyoitoa kuwa waliathiriwa na mvua si ya msingi kwa kuwa wakati wanaomba kazi walifahamu hali ya Tanzania hivyo walipaswa kujiandaa.