Na Frederick Katulanda
HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imezuia ujenzi wa jengo la ghorofa sita baada ya kubainika kuwa linajengwa chini ya viwango na bila kibali.
Akizunzungumza na Mwananchi juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alisema uamuzi wa kuzuia ujenzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwa mmiliki wa nyumba hiyo alikuwa akiendelea na ujenzi bila kibali cha halmashari.
Jengo hilo la Magnum, lililokusudiwa kutumika kama nyumba ya kulala wageni na ukumbi wa disko, limeelezwa kuwa lilikuwa linajengwa kinyume na kanuni za ukandarasi, jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji endapo lingekamilika na kutumika.
Alisema katika ujenzi huo wamekuta nguzo za juu zikiwa zimepishana na za chini, wakati nguzo nyingine zikianzia juu ya venti za ukuta, jambo ambalo alisema ni hatari, hasa ikizingatiwa kuwa mhusika anakusudia kulitumia kama ukumbi
wa disco na vyumba vya kulala wageni.
Alisema kutokana na hatua hiyo, Novemba 28, 2006, alimwandikia barua mmiliki wa jengo hilo lililopo katika viwanja namba 374 na 375 Kirumba Valley, kumtaka kusitisha ujenzi huo na kubomoa jengo hilo mara moja.
“Pamoja na kumtaka kusitisha ujenzi, pia tumemwagiza kuwasilisha nyaraka za hati za kiwanja chake na hati ya ujenzi, ramani zilizopitishwa, hati za wakaguzi waliokagua jengo hilo tangu hatua ya msingi kwa kuzingatia sheria, lakini hajafanya hivyo,” alisema.
Kibao cha ujenzi kilichowekwa katika eneo hilo, kimeonyesha kuwa ujenzi wake ulikuwa ukiendeshwa chini ya kandarasi ya HI-Tech Engineering kwa kibali cha ujenzi namba 11000.
Kabwe asema kibali kilichotajwa na wajenzi hao hakitambuliwi na ofisi yake. Kwa mujibu wa kabwe, kutokana na jengo hilo kuwa la zamani, haikuwa rahisi kwa halmashauiri kugundua mapema ujenzi huo, hadi mjenzi akafikia hatua ya kumwaga zege katika ghorofa ya kwanza.
Alisema sambamba na hatua hiyo, pia ameandika barua Novemba 29 mwaka huu kuitaarifu bodi ya wakandarasi juu ya mkandarasi HI-Tech engineering anayeendesha ujenzi huo juu ya hali halisi ya ujenzi huo.
Akizungumza na gazeti hili, mmiliki wa jengo hilo, Henry Matata, alisema amesikitishwa na hatua ya kuzuiliwa kuendelea na ujenzi huo wakati anavyo vibali halali.
Matata alisema kutokana na kibali alichonacho, halmashauri ya Jiji haipaswi kukikana kwa vile ni wao wenyewe waliokitoa Machi 29, 1984 wakati akianza ujenzi wa jengo hilo.
“Jengo hili nimeanza kulijenga mwaka 1984 na wao ndiyo walionipa kibali, nilikwama kuendelea na ujenzi, sasa nimepata fedha za mkopo kutoka benki nimeamua kuendelea wamenisimamisha kujenga, hapa nadhani hawajanitendea haki,” alisema.
Matata alisema anakiri kuwapo kwa kosa la ujenzi wa nguzo ambazo zimejengwa kimakosa na mkandarasi huyo, lakini alipinga hatua ya halmashauri ya jiji kumwagiza kusitisha ujenzi na kubomoa eneo hilo.
“Mimi sina nia ya kukaidi agizo lao lakini sikuwa na mpango wa kujenga ghorofa sita kama wao walivyodhani, kwa vile kujenga hivyo ni hatari kutokana na makosa hayo ya nguzo basi ningeomba halmashauri iniruhusu kuweka bati eneo hilo na kupaka rangi kwani hivi ni vitu vyepesi ambavyo kutokana na makosa haya havitaweza kuleta madhara,” alifafanua
Matata.
Hata hivyo, Bodi ya wakandarasi (CRB), imesema itamchukulia hatua mkandarasi aliyehusika na ujenzi wa jengo hilo kutokana na kukiuka kwa taratibu za ujenzi. Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Kanda wa CRB, Lucas Leonard, alisema mara baada ya kupokea barua kutoka Halmashauri ya Jiji iliyokuwa ikimtaka mmiliki wa jengo hilo kusitisha ujenzi, alikwenda kutembelea eneo la mradi.
Alisema baada ya kutembelea alibaini makosa ya kiufundi na kumwandikiwa mkandarasi wa HI-Tech Engineering kumtaka kuwasilisha nyaraka zake katika bodi ikiwa ni pamoja na mkataba wa ujenzi.
“Tumebaini makosa ya ujenzi huo yametokana na kukiukwa kwa taratibu kwani katika ujenzi huo lazima awepo msanifu, na mhandisi mshauri, lakini pale panasimamiwa na mtu binafsi kama mhandisi mshauri,” alisemaa meneja huyo wa kanda.
Alisema kutoka na kubaini hatua hizo tayari wamekwisha mwandikia barua Desemba 4, 2006 kumtaka kutekeleza agizo la Jiji ikiwa ni pamoja na kutoa maelezo juu ya uwezo wake katika ujenzi, kutoa taarifa za kampuni yake na kuwasilisha nyaraka za vyeti vya watalaamu wake katika kipindi cha siku saba.
Alisema iwapo hatafanya hivyo katika kipindi hicho, mara baada muda huo kwisha watamwandikia barua nyingine wakimpa siku 14 kutimiza maagizo ya awali na iwapo hatajibu watalazimika kumfikisha mahakamani