Na Muhibu Said WIKI chache baada ya kukimbiwa na Mwenyekiti wa wake na wanachama zaidi ya 600 mkoani Singida, Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, amepata pigo jingine baada ya Katibu Mwenezi wake, Octavian Matikila kujiengua na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Matikila, ambaye alipata kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu Taifa ya TLP, alijiunga na CCM katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yusufu Makamba, Tabata Mbuyuni eneo la Dampo, jijini Dar es Salaam juzi. "Nimetumia uhuru wangu wa kikatiba wa kujiunga na chama chochote cha siasa kati ya vyama 18 vilivyopo nchini," alisema Matikila alipofika katika ofisi za gazeti hili jana.
Alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na mabadiliko ndani ya CCM ambayo yamekifanya chama hicho hivi sasa kuwa chama cha kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na kwamba, sababu zilizomfanya ajiunge na upinzani hazipo tena. Pia, alisema amevutiwa na jinsi serikali ya awamu ya nne inavyopiga hatua kwa kasi kuendana na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 na kwamba, falsafa ya ari, nguvu na kasi mpya iliyoasisiwa na Rais Jakaya Kikwete inakwenda na matendo ya uhakika na u halisia wa mabadiliko halisi. "Binafsi nimeridhika sana. Nimevumilia, nimeshindwa nimeamua kusema lililo la ukweli.
Siwezi kufanya siasa za kimbumbumbu. Ndio maana nimejiunga CCM," alisema. Aliwataka wanachama wa TLP kutafakari upya juu ya kuwapo kwa ukomo wa uongozi wa mwenyekiti wa chama hicho, (Mrema), ambaye alidai kwamba tofauti na alivyokuwa CCM, umaarufu alionao hivi sasa hauwezi kuisaidia chochote TLP.