NEW YORK, Marekani
ASKOFU Mkuu, Emmanuel Milingo anazidi kulichokoza Kanisa Katoliki kwa kuwasimika waumini watatu waliooa kuwa mapadri katika ibada itakayofanyika leo mjini hapa.
Gazeti la The Herald linalochapishwa jimboni New Jersey, Marekani limeripoti jana kuwa, Askofu Milingo ambaye alitengwa na kanisa hilo, Septemba mwaka huu amekuwa katika harakati ambazo anaziita kuwa za kusuluhisha uhusiano mbaya kati ya Vatican na Mchungaji Sun Myung Moon, kutoka Korea.
Askofu Milingo ambaye alirejea Marekani Julai mwaka huu na kuzindua mtandao wa kupigania haki za mapadri wa Kikatoliki kuruhusiwa kuoa, anaouita, Married Priests Now.
Shughuli hiyo ya kuwabariki waumini wake kuwa mapadri inatarajiwa kufanyika katika hoteli ya Sheraton iliyoko kitongoji cha Parsippany, ambako unafanyika mkutano wa waumini wake wapatao 600 ambao anasema kuwa ni mapadri waliooa wakitokea sehemu mbalimbali duniani.
Waumini wenye msimamo mkali wa madhehebu ya Kikatoliki mjini New York, wameeleza kuwa hawawezi kuhudhuria ibada hiyo inayoambatana na maombezi na kufanyika katika Kanisa la Trinity Reformed Church, magharibi mwa New York.
Tayari, Vatican ambayo ilimtenga Askofu Milingo tangu Septemba imeeleza kuwa haitambui 'upadrisho' huo wa Milingo na kamwe haiwezi kujihusisha nao.
Kutengwa kwa Askofu Milingo, ambaye amejaliwa kuwa na kipaji cha kuponya, kulitokana na hatua yake ya kuwasimika watu wengine wanne kuwa maaskofu, akiwamo padri mmoja kutoka Jimbo la Newark. Hatua ya kutengwa kwake, kwa mujibu wa taratibu za Kanisa Katoliki, kuna maana kuwa shughuli zake zote anazozifanya hazitambuliwi na kanisa hilo.
Mmoja wa wenyeji wake, ambaye ni mratibu wa shughuli za leo, Askofu Dairo Ferrabolli anaeleza kupingana na msimamo wa kanisa hilo (Katoliki) kuhusu mabadiliko ya kubadili mwelekeo na kuukubali useja.
Anasema: “Sisi ni Wakatoliki. Ikiwa Vatican haipendi kututambua ni sawa.” . “Mama anamkana na kumkataa mtoto. Unategemea nini kutoka kwa mtoto?”
'Askofu' huyo ambaye alipadrishwa nchini Brazil mwaka 1979, aliongeza kuwa alilazimika kujiondoa upadri wa Kanisa Katoliki baada ya kuoa. Baada ya hapo akaanzisha kanisa huru, lialoitwa, Familia ya Kanisa Katoliki (Catholic Family Church) lenye kujumuisha familia 350 nchini Marekani na kutoka nchi za Karibiani.
Alieleza kuwa mara chache amekuwa akitoa huduma zikiwamo za ndoa na ubatizo, au sherehe za kuzaliwa. Mratibu huyo anaeleza kuwa anaendelea na maisha ya ndoa akiwa na watoto watatu.
Askofu Milingo na wafuasi wake wamekuwa wakieleza kuwa kuwaruhusu mapadri wa Kikatoliki waliooa kutoa huduma kamili kanisani litakuwa suluhisho la kuepukana na uhaba wa mapadri, kuboresha hadhi ya wanawake katika kanisa hilo na kuwa mfano mzuri kwa familia ya Kikristo.
Mkutano huo wa kiroho wa Askofu Milingo unaoendelea kwa wiki nzima umefadhiliwa na makundi yenye uhusiano na Moon, mwanzilishi wa madhehebu ya Unification Church, ambalo lina waumini wenye uwezo mkubwa kifedha na linaloabudu ndoa za pamoja.
Askofu Milingo amekuwa na uhusiano na kundi hilo tangu mwaka 2001, ambako alimchagulia mke kutoka miongoni mwa waumini wake na kufungishwa ndoa ya pamoja. Baada ya maombi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Yohane Paul II, Askofu Milingo aliachana na ndoa hiyo na kurejea kanisani hadi mwaka huu alipoanza vitimbi.
Shirika la Habari la Kikatoliki (CNS) linaeleza kuwa 'askofu' Ferrabolli, naye ana uhusiano na kundi la Mchungaji Moon.
Mkutano huo wa Milingo unaonyeshwa kupitia televisheni na satelaiti ukiwa na mapadri 1,200 na wake zao kutoka Ulaya, Afrika na Marekani ya Kusini.
Katika mkutano wake wa dharura mwezi uliopita, Vatican chini ya Papa Benedict XVI ilieleza kuwa kamwe haiwezi kubadili msimamo kuhusu useja, ingawa Kanisa Katoliki linaeleza wasiwasi kuhusiana na kutumiwa kwa umaarufu wa Milingo katika kuwapotosha wengi, hasa kutoka Afrika na ulimwengu wa tatu