Na Muhibu Said
MAELFU kwa maelfu ya watanzania, wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, jana walishuhudia kufana kwa aina yake sherehe za miaka 45 ya uhuru wa Tanganyika zilizofanyika kitaifa, jijini Dar es Salaam jana.
Kunoga kwa sherehe hizo kulihitimishwa na umahiri wa Rais Jakaya Kikwete kuongoza maelfu ya Watanzania kuimba wimbo maalum wa kusherehekea siku ya kuzaliwa, maarufu kama "happy birthday".
Sherehe hizo zilizohudhuriwa na marais na wawakilishi wa serikali za nchi nane za Afrika, zilipambwa pia na maonyesho ya ndege za kivita zilizoruka na kuzunguka angani juu ya Uwanja wa Taifa, huku maelfu ya watu wakishangilia zilipopita.
Rais Kikwete, aliongoza kuimba wimbo huo muda mfupi baada ya kuhutubia taifa ikiwa ni mara yake ya kwanza kuongoza sherehe hizo tangu ashike wadhifa wa urais, Desemba 21, mwaka jana.
Kabla ya kuongoza kuimba, Rais Kikwete, aliwaomba watu wote waliofika uwanjani hapo kusimama, akauliza kama kuna mtu anayeweza kujitokeza hadharani na kuongoza kuimba wimbo huo.
Hata hivyo, Kikwete alijiteua na kuanza kuimba kwa sauti inayotumika kila mara wimbo huo unapoimbwa, huku akiitikiwa na umati wa Watanzania na wageni waliofurika uwanjani hapo.
Tukio hilo lilitanguliwa na matukio mbalimbali yaliyopamba sherehe hizo na kuwavutia maelfu ya watu waliohudhuria katika uwanja huo.
Tukio mojawapo ni la ndege za tano za kivita zilizoruka angani na kupita kwa kasi juu ya uwanja huo, huku zikijibinua kwa mbwembwe kulia na kushoto.
Hali hiyo iliamsha msisimko na kuufanya umati wa watu waliohudhuria, wakiwamo viongozi wakuu wa serikali waliokuwa wamekaa jukwaa kuu, kushangilia kwa nguvu.
Tukio jingine lillilopamba sherehe hizo, ni la wanafunzi 4,000 kutoka katika baadhi ya shule za sekondari jijini Dar es Salaam waliounda halaiki na kujikusanya katikati ya uwanja huo na kuumba maneno: "Miaka 45 ya Uhuru".
Jingine, ni la Watanzania 50 waliozaliwa Desemba 9, mwaka, 1961 siku ambayo Tanganyika ilijipatia uhuru wake waliopata nafasi ya kupita mbele ya jukwaa kuu na kutoa heshima zao kabla ya kusimama na kuimba wimbo maalum wa kujipongeza na kushukuru kwa tukio hilo.
Sherehe hizo zilianza saa 4:17 asubuhi baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuwasili uwanjani hapo na kukagua gwaride la vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama.
Kabla ya kukagua vikosi hivyo, akiwa ndani ya gari la wazi, Rais Kikwete, alizunguka uwanjani hapo akiwapungia mikono watu waliohudhuria sherehe hizo na kushangiliwa.
Baadaye, Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alisimama katika jukwaa maalum lililoandaliwa kwa ajili yake na wimbo wa taifa na mizinga 21 vilipigwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa heshima yake na taifa.
Baadaye, alikwenda katika jukwaa kuu na vikosi hivyo vilianza gwaride kwa kupita mbele yake kwa mwendo wa polepole na baadaye wa kasi na kutoa heshima za utii na unyenyekevu kwake.
Gwaride hilo liliongozwa na Luteni Kanali Venance Mbele wa JWTZ na wananchi na viongozi waliohudhuria sherehe hizo, walishangilia kila askari walipokuwa wakionyesha ukakamavu na uhodari wao wa kumiliki silaha. Tukio hilo lilitokea kabla na baada ya Rais Kikwete kuwasili uwanjani hapo.
Vikosi vilivyoshiriki gwaride hilo, ni Kikosi cha Bendera, Nchi Kavu-wanaume cha JWTZ, Ulinzi wa Anga, Wanamaji (Navy), JWTZ-wanawake, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)- wanaume na wanawake, Kutuliza Ghasia (FFU)-wanaume, Polisi-wanawake, Magereza- wanaume na wanawake.
Kila kikosi kilichopita karibu na jukwaa kuu, Rais Kikwete pamoja na viongozi wengine waliokuwa katika jukwaa hilo, walisimama kama ishara ya kupokea heshima kutoka kwa vikosi hivyo.
Hata hivyo, gwaride hilo liliingia dosari baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuanguka na kupoteza fahamu uwanjani hapo kutokana na kusimama kwa muda mrefu.
Askari huyo ambaye hakuweza kufahamika mara moja, aliondolewa uwanjani hapo kwa kubebwa kwenye machela na polisi jeshi (MP) na kwenda kupatiwa huduma ya kwanza katika hema maalum lililoandaliwa uwanjani hapo kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
Mbali na askari huyo, watu kadhaa waliohudhuria sherehe hizo, walianguka na kupoteza fahamu kutokana na sababu mbalimbali. Nao walibebwa kwenye machela na watoa huduma wa Msalaba Mwekundu (Red Cross) na kwenda kupatiwa huduma ya kwanza katika hema hizo.
Viongozi waliohudhuria sherehe hizo, ni Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Mwai Kibaki wa Kenya, Levy Mwanawasa wa Zambia, Bingu wa Mutharika wa Malawi, Ahmed Abdallah Sambi wa Shirikisho la Visiwa vya Comoro, Makamu wa Rais wa Burundi, Marie Barampamba na Waziri Mkuu wa Lesotho, Pakalitha Mosisili.
Mbali na marais hao, sherehe za maadhimisho hayo zilihudhuriwa pia na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume na mawaziri wa serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ.
Wengine, ni baadhi ya viongozi wakuu wastaafu wa serikali hizo, mabalozi wa nchi mbalimbali duniani, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, mashirika ya umma, binafsi, wafanyabiashara wakubwa na wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa kambi ya upinzani waliohudhuria sherehe hizo, ni pamoja na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na John Cheyo wa UDP.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete, alisema nchi hivi sasa imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika nyanja zote za maisha ya Watanzania, ikiwamo umoja wa kitaifa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kulinganisha na walipoiacha wakoloni.
"Ni dhahiri kabisa kwamba ukilinganisha tulipo sasa na kule tulikotoka miaka 45 iliyopita tumepiga hatua kubwa sana. Katika nyanja zote za maisha ya mwananchi wa Tanzania Bara tumepata maendeleo makubwa ukilinganisha na pale alipotuacha mkoloni. Tumefaulu," alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, aliwataka Watanzania katika nafasi walizonazo kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi.
"Kauli ile ya 'Uhuru na Kazi' bado ina maana sasa kama ilivyokuwa wakati ule. Sisi sote tufanye kazi kwa bidii kwani Uhuru ni Kazi," alisema Rais Kikwete.
Naye Burhan Yakub kutoka Tanga, anaripoti kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sara Dumba, jana alikuwa kivutio katika maadhimisho ya miaka 45 ya uhuru yaliyofanyika mkoani humo baada ya kuchukua jukumu la kuwa msemaji (MC) wakati wa gwaride.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, aliwataka wananchi kulisaidia jeshi la polisi katika kampeni linayoiendesha kupambana na uhalifu na akalipongeza jeshi hilo.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Chuo cha Ualimu, Dumba, alipoanza kutangaza wakati gwaride la wahitimu wa mgambo wakipita mbele ya Mkuu wa Mkoa, kivutio kilitokea baada ya wananchi kugombea kutaka kumuona Dumba na hivyo kuvuruga utaratibu uliokuwa umewekwa ambapo walisema amewakumbusha alipokuwa akitangaza.
Mkuu huyo wa Wilaya ambaye ni mtangazaji wa zamani alimudu vyema na kutaja kila hatua za kijeshi zilipokuwa zikitendeka na kusababisha kushangiliwa na watu waliokuwa wamekusanyika.
Katika risala yao, wahitimu 100 wa mgambo, walilalamika kuwa kampuni ya ulinzi bado zinawanyonya kwa kuwalipa mshahara wa Sh30,000 kwa mwezi na kumwomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa mgambo kuonyesha gwaride kuapa kiapo cha utii kwa Rais na maonyesho ya kivita