Na Waandishi Wetu
TANGANYIKA jana imetimiza miaka 45 ya uhuru wake huku wasiwasi ukitanda miongoni mwa wananchi kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Wengi wa wale waliozungumza na Mwananchi Jumapili kuhusu iwapo uhuru huo umeweza kutimiza matakwa au matarajio yao, wameonyesha dhahiri kukata tamaa hasa kutokana na mahali ambako taifa lao linaelekea huku wengine wakijiuliza ni lipi wamekosea, lipi lifanyike ili kukwamua hali ngumu inayolikabili taifa.
Mafanikio ya awali yaliyoanza kujengwa na awamu ya kwanza, chini ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yaliyoambatana na kujenga misingi ya ujamaa, kupambana na rushwa, kubomoa ufa kati ya maskini na tajiri, kujenga msingi wa elimu ya kujitegemea, kuanzisha vijiji vya ujamaa na kutoa huduma za msingi kwa raia bure, yanabaki kama historia isiyowezekana tena kufikiwa.
James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi anafafanua hali hii kwa kusema: “ Wakati wa kipindi cha mwisho cha utawala wa Mwalimu Nyerere, shilingi ilikuwa inabadilishwa na dola kwa wastani wa shilingi 350. Katika kipindi cha Rais Alli Hassan Mwinyi, hususan, wakati anamaliza muda wake wa uongozi, aliacha dola moja ikibadilishwa kwa shilingi 550.
Wakati wa miaka kumi ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa shilingi iliporomoka kwa asilimia 100 na kufikia kuwa sawa na shilingi 1,050 huku mwaka mmoja wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ikianza kwa kuporomosha shilingi kwa asilimia 20 zaidi na kufikia shilingi 1,300.”
Mtazamo huu wa kuporomoka kwa shilingi unaambatana na kuongezeka kwa bei za vitu mbalimbali na ugumu wa maisha toka kipindi kimoja cha utawala hadi kingine. Uhalisia katika matukio yote hayo ni kuwa; hali inazidi kuwa ngumu na huwezi kufananisha leo na jana kutokana na leo kuwa na ugumu kuliko unafuu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba anaelezea wasiwasi wake kuhusu bajeti ya taifa hili kwa kusema: “Bajeti yetu inategemea sana misaada na mikopo toka nje sasa kuliko ilivyokuwa kipindi cha awamu ya kwanza. Hili ni jambo ambalo nchi iliyokuwa huru kwa miaka 45 haiwezi kujivunia hata kidogo.”
Profesa Haroub Othman, mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam, anasema: “kipindi cha kwanza cha utawala, Tanzania ilifanikiwa katika kujenga uchumi wa kijamaa na kujitegemea hali iliyowanufaisha wengi.
“Awamu ya pili ilifungua milango, ikaruhusu kila jambo kuingia. Lengo la kufungua milango likatumika vibaya na kusababishia madhara taifa.
“Sasa, awamu ya nne imewekeza muda wake katika kuwavutia wawekezaji wakubwa bila kutilia mkazo wawekezaji wa humu ndani na uwezo wao wa ushindani,” anasema.
Ufa kati ya matajiri na maskini uliobomolewa kwa kiasi kikubwa na serikali ya awamu ya kwanza, ulianza kutanuka katika awamu ya pili na kisha kuonekana kama haki ya maisha ya Tanzania wakati wa awamu ya tatu. Ni jambo hili hili linaloonekana kuwepo katika awamu ya nne pia.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, John Malecela amekaririwa akisema: “Tusiruhusu hata kidogo suala la watu wachache kuwa matajiri sana na maskini kuwa maskini.”
Kauli hii ya Malecela haiwezi kutekelezeka katika Tanzania ya sasa; Tanzania ambayo mipango yake ya uchangiaji huduma za msingi zimegeuka mwiba kwa raia maskini na kuwa asali kwa raia tajiri.
Bado anayenufaika na huduma ni tajiri na kundi hili linaishi maisha ya kifahari huku maskini akizidi kudunishwa kutokana kutetereka kwa soko la mazao, kutokuwa na mikakati ya kilimo cha mazao ya chakula, kupanda kwa gharama za shule na afya, kukosekana huduma za maji na nishati ya umeme, barabara mbovu na mzizi mkubwa wa rushwa unaozidi kulitafuna taifa.
Mbunge wa zamani wa Ilala, Idd Simba ambaye pia ni mfanyabiashara anazungumza kuwa, rushwa hapa nchini inashindikana kutoweka kutokana na kuwa wakubwa wa juu kabisa wa nchi hii nao wanajihusisha nayo.
Kauli hii ya Simba ni marudio ya kauli aliyowahi kuitoa Mbunge wa zamani wa jimbo la Makete Dk Hans Kitine aliyesema vigogo wengi wa nchi hii wanajihusisha na kula rushwa.
Kauli za wabunge hawa zinaendana na ushahidi wa kimazingira, hasa ukifuatilia kuongezeka kwa mikataba inayotia utata katika sekta za madini, zoezi la ubinafshaji na zabuni mbalimbali za kutoa huduma kwa jamii.
Mingi ya mikataba hii inapatikana kuanzia awamu ya pili kisha kuendelea kwa kasi zaidi katika awamu ya tatu na inavyoonyesha inachanja mbuga katika awamu hii. Shirika la Transparency International katika ripoti yake ya mwaka 2006 iliyotoka mapema wiki hii, inaonyesha bara la Afrika kama kituo kikuu cha rushwa na inafafanua kuwa rushwa inapatikana katika majeshi ya polisi na sehemu za huduma za jamii.
Huu ni ukweli katika Tanzania ambapo Tume ya Kudhibiti Rushwa nchini imekuwa ikilalamika kuwa haina nguvu ya kutazama mikataba ambayo ndiyo hasa inayobeba rushwa kubwa huku viongozi wa serikali nao wakikumbatia mikataba hiyo kwa kudai ni siri ya wao kama serikali na wenye mikataba hiyo yaani wawekezaji.
Profesa Lipumba anafafanua kutanuka kwa rushwa nchini kwa kusema: “Usingeweza kusikia kuibiwa mitihani katika miaka ya 1960, lakini sasa hali hii ni ya kawaida kabisa.”
Tanzania iliwahi kusifika kutokana na uwezo wake wa kuwawezesha wananchi kujua kusoma na kuandika katika kipindi cha awamu ya kwanza, ushahidi ulipatikana mapema mwaka jana baada ya zoezi la kuandikisha wapiga kura na kufahamika idadi ya asilimia tano ya watanzania haijui kusoma na kuandika sasa.
Inawezekana kabisa idadi hiyo ikaongezeka huku pia ikiathiri sekta nyingine za afya ambapo huko, wananchi wamehamia katika matumizi ya mitishamba kufuatia kutomudu gharama za afya.
Kwa hiyo, miaka 45, ya uhuru inalikuta taifa hili likiwa halina uwezo wa kujiendesha katika sekta ya nishati, mathalan umeme. Ule unaopatikana nchini umebakia kuwa jambo la anasa na mikakati ya kuutanua hadi vijijini umebakia katika vitabu, huku maeneo ya mijini pia yakigubikwa na makali ya mgawo wa huduma hiyo.
Watanzania, kwa ujumla wanaachwa katika hofu, hasa ile ya kutawaliwa upya kufuatia, kuwa na idadi ndogo ya wasomi, mfumo wao wa elimu kukosa hadhi ya ushindani pale wanapokutanishwa na mataifa mengine, na pia uwezo wao mdogo katika biashara za ndani na nje ya nchi.
Harakati za kuwaendeleza Watanzania kwa kuwapa uwezo na mtaji zinashindwa kutekelezeka kutokana na matatizo mengi yanayojitokeza. Mfano, taaluma katika kuwekeza, aina za biashara za kufanya na uwezo wa kupata huduma za msingi za maisha.
Ni vigumu kwa Mtanzania wa leo kwa mfano kuweza kuchukua mkopo kutoka benki, kuutumia kama inavyohitajika kufuatia maisha yake kuambatana na matatizo mengi yakiwamo ya ukosefu wa huduma muhimu na za msingi kama chakula, afya na elimu.