Na Mwandishi Wetu
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kagera, Venance Tossi ameonya kuwa atawatia mbaroni viongozi wanaotetea wahalifu mkoani humo.
Tossi alitoa onyo hilo juzi katika Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Kagera ambacho kilihudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, wadau wa maendeleo kutoka asasi binafsi na za serikali na watendaji wa serikali mkoani humo.
Kamanda huyo alifafanua kuwa, ametoa onyo hilo baada ya kuwapo kwa baadhi ya viongozi ambao wanadaiwa kushirikiana au kuwatetea wahalifu kwa maslahi yao binafsi.
Aliwaomba viongozi hao kutoshiriki kutetea uharifu na kuwashauri kuzingatia kiapo walichokula cha kuwa waaminifu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lasivyo yeye kama msimamizi wa utekelezaji wa sheria mkoani humo, atahakikisha anawatia mbaroni.
“ Tutende kama tulivyokula kiapo chetu, tusipende kuwafurahisha wahalifu kwa manufaa ya mtu binafsi, ” alisisitiza Kamanda Tossi katika kikao hicho kilichokuwa kikijadili aendeleo ya Mkoa wa Kagera katika Ukumbi wa Kolping.
Kamanda hyuyo aliwaahidi viongozi hao kuwa atahakikisha anafanya kazi kwa uaminifu, hekima na busara bila ya kumwonea mtu na kuhakikisha anajenga uhusiano mwema na wananchi ili jeshi la polisi liwe kimbilio la wananchi.
Alisema ili jeshi hilo liweze kufanya vizuri na kuhakikisha linadhibiti vitendo vya uhalifu vilivyokithiri mkoani humo, unahitajika ushirikiano wao ndipo kazi itakuwa nyepesi.
Tossi alizitaja wilaya ambazo zimekithiri kwa uhalifu wa kutumia silaha kuwa ni Biharamulo, Ngara na Karagwe kutokana na kuwa mpakani na kuwapo kwa wakimbizi.
Aliapa kukabiliana na uhalifu mwingine wa kutozingatia sheria za barabara hasa katika wilaya za Bukoba na Muleba, kwa waendesha magari, pikipiki na baiskeli.