Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mabilioni ya Kikwete yapelekwa benki
Mabilioni ya Kikwete yapelekwa benki
By Habari Tanzania | Published  12/8/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Midraji Ibrahim

SERIKALI na benki ya National Microfinance (NMB) na CRDB, zimekamilisha taratibu za kuanza kutoa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuinua vipato vyao.

Akizungumza ofisini kwake jana, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Kapteni John Chiligati, alisema fedha hizo tayari zimepelekwa katika benki hizo baada ya kukamilisha mazungumzo na benki hizo.

"Ninavyozungumza hivi sasa tayari Sh10.5 bilioni zimeshapelekwa kwenye benki hizo," alisema.

Waziri Chiligati, alisema fedha hizo ni dhamana ya mkopo utakaotolewa na benki hizo na kwamba benki zenyewe zimeahidi kutoa mkopo mara tatu ya fedha hizo. Kwa maana hiyo, NMB na CRDB zitatoa mkopo wa Sh30 bilioni.

Akizungumzia kuchelewa kwa fedha hizo kwa takriban miezi sita, Kapteni Chiligati alisema mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu kwa sababu kulikuwa na mlolongo wa masharti kwa wakopaji wa benki hizo, ambayo serikali iliona yatakuwa ni kikwazo kwa walengwa.

Alisema benki hizo hutoza riba kati ya asilimia 10 na 30 kwa wateja wake, kodi ya mkopo na dhamana, huku serikali ikitaka riba ya mkopo iwe asilimia 10 na kusiwepo na kodi wala dhamana ya mkopo.

"Wenzetu waliona kama tunawavurugia utaratibu wao, lakini tumezungumza na Oktoba tulifikia makubaliano na kusaini makubaliano," alisema.

Alisema mchakato unaoendelea ni mafunzo ya wiki mbili kwa maafisa ushirika, maendeleo ya jamii na mipango katika kila halmashauri ambao watawezeshwa kwa ajili ya kwenda kutoa elimu ya jinsi ya kuandika michanganuo kwa maafisa wa ngazi za kata.

Mafunzo hayo yamegawanywa katika kanda tano; Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma, Arusha na Mwanza na kwamba, ifikapo mwisho wa Desemba taratibu zote zitakuwa zimekamilika na wananchi wataanza kukopa.

Kapteni Chiligati alisema baada ya kukamilika kwa mazungumzo na wakopeshaji wakubwa, hivi sasa wanataka kuanza kujadiliana na wakopeshaji wadogo ambao ni vyama vya akiba na mikopo na benki za wananchi.

"Hata hawa wakopeshaji wa kundi hili, baada ya kujadiliana nao na kufikia muafaka tutawapa Sh10.5 bilioni, tofauti na wakopeshaji wakubwa, fedha tutakazowapa sio dhamana bali ndizo watakazotumia kukopesha," alisema.

Alisema wakopeshaji wote wanalenga kumkopesha mwananchi wa kawaida na masharti yanabaki yale yale.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ben Christiaanse, alisema wiki hii watapeleka maelekezo katika matawi yote nchini kwa ajili ya wananchi wanaotaka kukopa.

Katika Bunge la bajeti Juni mwaka huu, serikali ilitangaza kutoa Sh500 milioni kwa kila mkoa kwa ajili ya kukopesha wananchi wa kawaida, lakini Rais Jakaya Kikwete akiwa ziarani Mkoa wa Mara, alitangaza kuongeza kiwango hicho na kufikia Sh1 bilioni.

Fedha hizo ambazo zilitengwa katika bajeti ya mwaka huu, hadi sasa ni miezi sita hazijaanza kutolewa, suala lililozusha hisia kwamba, huenda mwaka wa fedha 2006/07 ukamalizika bila kutolewa kwa mikopo hiyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.