Frederick Katulanda
MVUA kubwa zilizonyesha katika Jiji la Mwanza jana zilisababisha mafuriko makubwa na kuharibu mali za watu na kusababisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwaza kufungwa.
Mitaa mbalimbali ya jiji hilo jana ilifurika maji, ukiwemo mto Mirongo uliojaa maji na kuleta wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa jiji la Mwanza.
Kutokana na mafuriko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Alex Msekela, alitangaza kuufunga Uwanja wa Ndege wa Mwanza kutokana na kujaa maji hadi hapo maji yatakapopungua na hali kurejea kuwa ya kawaida.
Mafuriko hayo yalitokea kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha saa 4.21 asubuhi hadi saa 7:13 mchana na kusababisha kujaa kwa maji katika maeneo mbalimbali ya mitaa ya Mkuyuni, Mkolani, Nyamanoro, Liberty na Uwanja wa Ndege.
Kutokana na mafuriko hayo, mto Mirongo ulifurika na kumwaga maji yake katika mitaa mbalimbali ya jiji na kuleta tafrani kubwa.
Baadhi ya wakazi wa Mitaa ya Mabatini unapopita mto Mirongo, walikuwa wakihaha kuhamisha familia zao pamoja na mali ndani ya nyumba kutokana na maji kufurika huku baadhi yao wakitoka kazini kukimbilia nyumbani kwao kuangalia usalama wa familia zao.
Barabara iendeyo Musoma eneo la Mabatini Mlango Mmoja, Misheni na Uhuru kupitia Liberty, zilikuwa hazipitiki kwa muda wa saa tatu kutokana na maji hayo ya mafuriko kujaa hadi juu ya daraja na hivyo kusababisha magari na watu kushindwa kuvuka.
Katika mafuriko hayo, watu wawili wanahofiwa kufa baada ya kusombwa na maji wakiwa katika daraja la Liberty wakiokota vitu vilivyokuwa vikipita katika daraja hilo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Zelote Stephen, alisema alikuwa hajapata taarifa za vifo hivyo, ingawa alikiri kupokea taarifa za mtu mmoja aliyechukuliwa na maji katika eneo la Mkolani na baadaye kuokolewa na kukimbizwa hospitalini.
Hata hivyo, Kamanda huyo alisema kuwa hali ni mbaya katika maeneo ya mabatini na kueleza wasiwasi wake
kuwa iwapo mvua itaendelea kunyesha tena, huenda maafa makubwa yakatokea na watu kupoteza zaidi mali zao.
"Nadhani watu wanaoishi kando kando ya mto sasa wanapaswa kuwa na tahadhari kubwa na ikiwezekana kuhama kwa muda kwani maafa makubwa zaidi yanaweza kutokea iwapo mvua hizi zitaendelea kunyesha," alisema Kamanda Zelothe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa, alisema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu ambazo
baadhi zimeharibiwa na nyingine kusombwa na maji.
Alisema ofisi yake imeiagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutafuta ufumbuzi wa watu waliojenga kando ya mto huo, ikiwa ni pamoja na kukutana naye kujadili namna ya kujenga kingo za mto huo ili kuepuka maafa makubwa zaidi.
"...Hili limetokea kama fundisho kwetu mimi toka nimekuwa mkuu hapa nilikuwa siujui mto huu, nadhani sasa ni wakati wa kuchukua hatua," alisema Dk Msekela.
Hii ni mara ya pili kwa mafuriko kutokea jijini Mwanza na kusababisha maafa. Desemba 2001 mafuriko makubwa yatokea katika mto huo na kuua watu wanne baada ya maji na Waziri Mkuu wakati huo, Frederick Sumaye, aliagiza Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha waliojenga kando ya mto huo wanahamishwa mara moja ikiwa ni pamoja na kupatiwa viwanja vipya agizo ambalo halijatekelezwa hadi leo.