Na Waandishi Wetu
SHEREHE za miaka 45 ya Uhuru wa Tanganyika zitapambwa kwa mbwembwe za aina mbalimbali, yakiwamo maonyesho ya ndege za kivita zitakazokuwa zikiruka kuzunguka angani juu ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kesho.
Kabla ya maonyesho hayo ambayo yatafanyika sambamba na gwaride la vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama, leo usiku kutakuwa na tukio la ulipuaji wa fataki kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, kuashiria kushushwa kwa bendera ya mkoloni na kupandishwa bendera ya Tanganyika huru.
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo atakuwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye pamoja na kulihutubua taifa kwenye uwanja wa taifa kesho, atawaongoza Watanzania katika uzinduzi wa sherehe hizo saa 6.00 leo usiku kwa kufyatua fataki hewani, katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Juma Akukweti, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuwa maonyesho hayo yatakayoshirikisha ndege tano za kivita, yatafanyika wakati gwaride likiwa uwanjani na kwamba zitapita katika anga la eneo la Uwanja wa Taifa na kutoa heshima.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu na kutoogopa wakati ndege hizo zitakapokuwa katika tukio hilo. “Watanzania wasishtuke hili ni jambo la kawaida na ili kuondoa hofu itapita ndege moja kwanza kisha zitafuatia nyingine, tunategemea zitakuwepo ndege tano,” alisema Akukweti.
Waziri huyo alisema, sherehe hizo ambazo zitahanikizwa na mizinga 21, zitahudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida, viongozi wa ndani na nje ya nchi na kwamba Watanzania 50 waliozaliwa siku ya uhuru mwaka 1961 pia watashiriki.
Akukweti alisema hadi sasa marais nane kutoka nchi mbalimbali wamethibitisha kushiriki kwenye sherehe hizo Marais hao ni Ahmed Abdallah kutoka, Visiwa vya Comoro, Levy Mwanawasa (Zambia), Bingu wa Mutharika (Malawi) na Armando Guebuza wa Msumbiji.
Wengine ni Mwai Kibaki (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Pierre Nkurunziza (Burundi) na Waziri Mkuu wa Lesotho, Pakalitha Mosisili. Jumla ya marais 15 wamealikwa kuhudhuria maadhimisho hayo.
Akielezea kisa cha serikali kufanya sherehe kubwa namna hii, Akukweti alisema, "Kupata uhuru si jambo la mzaha, wenzetu wa nchi nyingine wanakufa wakitafuta uhuru, hivyo naomba Watanzania popote pale walipo washerehekee siku hii.”
Naye Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Vicent Mrisho, alisema ahadi zote za michango ya kufanikisha sherehe hizo za miaka 45 ya uhuru zimetekelezwa kwa wakati ambapo jumla ya Sh334,543,000 zimepatikana.
Alisema maelekezo ya kudhibiti usalama wakati wa maadhimisho hayo yametolewa kwa vyombo vyote vya usalama hivyo wananachi wasiwe na wasiwasi juu ya suala hilo.
“Tunawashukuru kwa dhati kabisa wakuu wa mashirika, taasisi, makampuni, wafanyabiashara na wananchi mbalimbali ambao wameitikia wito na kutoa michango yao ili kufanikisha sherehe hizi,” alisema Mrisho.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, amewataka wakazi wa Dar es Salaam, kuvumilia misongamano ya magari kuanzia leo kutokana na wageni wengi kutoka nje ya nchi waliothibitisha kuhudhuria sherehe hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Tibaigana alisema wageni waliothibitisha kuhudhuria sherehe hizo wa watawasili kwa nyakati tofauti leo na kuwa barabara zinazoelekea katika hoteli za Kilimanjaro Kempinsk, Moven Pick, Holday Inn na Golden Tulip zitakuwa zinafungwa kadri wageni hao watakavyokuwa wanaingia.
Alisema barabara ya Nelson Mandela itafungwa kwa malori makubwa na yale yanayobeba mafuta kuanzia eneo la Bendera tatu hadi Tazara kuanzia leo saa 12.00 jioni hadi kesho saa 8.00 mchana ili kupunguza usumbufu kwa wageni.
Tibaigana pia alitangaza kuruhusu kupigwa fataki katika mkesha wa uhuru kuanzia leo saa 5.30 hadi 6.00 usiku na kwamba, wananchi wasiwe na wasiwasi watakaposikia milio na mwanga angani, huku akisisitiza kuwa ulinzia umeimarishwa zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro aliwatangazia wananchi kuanza kuingia katika viwanja vya mnazi mmoja kuanzi leo saa 1.00 jioni kwa ajili ya mkesha wa uhuru, ambapo vikundi vya burudani mbalimbali vitatumbuiza ikiwa ni pamoja na Shikamoo Jazz, DDC Mliman Park, Msondo, Zanzibar Stars Taarab na mwanamuziki wa kizazi kipya, Juma Nature. Pia zitakuwepo ngoma za asili kutoka Arusha, Zanzibar, Dodoma na Chuo cha Sanaa Bagamoyo.