Na Mwandishi Wetu
WATENDAJI wa Halmahauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, wameuomba mradi wa kuendeleza Sekta ya Kilimo ngazi ya wilaya (ASPS-DADS) kuendelea kufadhili miradi
ya kilimo cha umwagiliaji nchini.
Ombi hilo liliwekewa msisitizo na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Tina Senkambo, kutokana na maelezo ya afisa mipango mwezeshaji wa mpango huo, Dk Mshindo
Msolla, kuwa ASPS-DADS inajiondoa kufadhili eneo hilo.
Dk Msolla alitoa msimamo huo jana katika kikao cha pamoja kati ya Mkurugenzi huyo, wakuu wa Idara na waandishi wa habari wanaotembelea miradi inayofadhiliwa na mpango huo.
Alisema ASPS-DADS inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida) itaendelea kufadhili miradi mingine itakayoibuliwa na wakulima hata kama si ya umwagiliaji.
“Wizara ya kilimo ina miradi mingine yenye fedha nyingi ambazo zinaweza kuelekezwa kusaidia kilimo cha umwagiliaji na si vizuri wote tukasaidia eneo moja
tumeona kuanzia mwakani tujiondoe,” alisema Dk Msolla.
Alifafanua kuwa serikali imekwishaweka wazi kuwa inazo karibu Sh2.5 trilioni kwa ajili ya kilimo na kuna miradi iliyoko chini ya wizara ya kilimo
ikiwamo Padep na ASPD ambayo inaweza kujikita eneo hilo.
Hata hivyo maelezo hayo yalionekana kutomuingia Senkambo na wakuu wake wa Idara ambao waliiomba ASPS DADS kubadili msimamo huo na kuiangalia wilaya hiyo kwa jicho la huruma.
Senkambo alisema japo wananchi wake wengi wanategemea kilimo katika wilaya yake, lakini asilimia 70 ya eneo lote la wilaya halipati mvua za kutosha na hivyo kuwafanya wananchi wake kutegemea kilimo cha umwagiliaji.
“Ni kweli hatuna budi kuheshimu msimamo wenu, lakini kwa kuwa bado mtasaidia miradi ya wakulima na miradi inayohitajika wilaya yetu ni ya umwagiliaji
tunaomba mtuangalie tofauti,” alisema Mkurugenzi.
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Goliati Temu, alisema japo ipo miradi inayoweza kufadhili miradi ya umwagiliaji, lakini kujiondoa kwa ASPS DADS kutakuwa pigo kubwa kwa wilaya hiyo.
Afisa Kilimo wa wilaya, Fidelica Myovella, alisema ni tarafa mbili za Kiponzelo na Mlolo ndizo zinazopata mvua za kutosha lakini tarafa za Kalenga,
Idodi, Ismani na Pawaga zitaendelea kutegemea zaidi kilimo cha umwagiliaji.
Kwa mujibu wa mratibu wa shughuli za ASPS DADS katika wilaya hiyo, Abel Mgimwa, karibu Sh500 milioni zimetumika tangu mpango huo uanze kufadhili miradi ya kilimo vijijini mwaka 2004 hadi sasa