Na Muhibu Said
SIKU mbili baada ya kuripotiwa na gazeti hili kwamba biashara ya ukahaba imerejea upya katika eneo la Uwanja wa Fisi, Manzese, serikali imeamka na kuisambaratisha tena.
Katika operesheni hiyo watu 12 wamekamatwa na wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo.
Habari kutoka katika eneo hilo zilizothibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, zinaeleza kuwa kati ya watu waliokamatwa, saba wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya madanguro na watano kufanya biashara ya ukahaba.
Madanguro maarufu yanayotumiwa kuendesha biashara ya ngono katika eneo hilo, ni pamoja na Kwa Shangazi, Nyota, Kwa Charles, Mpolampola na Kizigo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Jamal Rwambow, amethibitisha kukamatwa kwa watu katika eneo hilo, lakini akasema hadi jana mchana, alikuwa hajapata majina ya watuhumiwa hao.
Watu hao walikamatwa katika operesheni iliyofanywa upya na polisi kwa kushirikiana na mgambo wa kata na wa manispaa juzi usiku.
Operesheni hiyo, iliongozwa na DC Massawe siku mbili baada ya gazeti hili kuchapisha habari zinazoelezea kurejea upya kwa biashara ya ukahaba, uuzaji na uvutaji wa bangi, matumizi ya dawa za kulevya, pombe za kienyeji na nyama choma zinazoandaliwa na kuuzwa katika mazingira machafu.
Sambamba na operesheni hiyo, eneo hilo hivi sasa linalindwa mchana na usiku na askari wa kata, manispaa na polisi.
Massawe alisema watu hao ambao hadi jana asubuhi walikuwa wakishikiliwa katika kituo cha polisi Magomeni, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mbali na kukamatwa watu hao, baa tatu zilizoko katika eneo hilo, ikiwamo ya Massawe, Rombo Silent na Kwa Wasiwasi, zimepigwa marufuku baada ya serikali wilayani humo kuzifutia leseni.
Mkuu wa wilaya huyo pia alisema nyumba 17 zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya watu kuendesha biashara ya ukahaba, zitabomolewa na kujengwa mradi mpya wa maendeleo, kama vile zahanati au shule.
Mwananchi ambayo ilifika katika eneo hilo, ilishuhudia nyumba hizo zikiwa zimewekewa alama ya X ikiwa ni hatua ya awali kuelekea katika utekelezaji wa bomoabomoa hiyo.
"Tutawalipa fidia na tutawatafutia pia viwanja mahali pengine ambako watakwenda kujenga nyumba mpya za kuishi," alisema Massawe.
Kwa upande mwingine, DC Massawe, alisema serikali inaendelea na juhudi za kuwapata wafadhili watakaozinunua nyumba hizo na kuwekeza mradi mmojawapo wa maendeleo katika eneo hilo.
Alisema baada ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kesi yao kwisha, wataanza ukaguzi wa mikataba ya wapangaji wanaoishi katika nyumba zilizoko katika eneo hilo.
Massawe alisema baada ya ukaguzi huo, hawataruhusu mpangaji kuingia mkataba wa muda mfupi na mmiliki wa nyumba na badala yake itakayoruhusiwa ni mikataba ya muda mrefu pekee. Hakutaja muda halisi wa mikataba hiyo.
Alisema serikali imefikia hatua hiyo baada ya kushindwa kuvumilia kuona watoto ambao ni taifa la kesho, wanaharibika kimaadili na kiafya katika eneo hilo.
"Hapo (Uwanja wa Fisi) kuna dawa za kulevya na kuna magonjwa ya zinaa babu kubwa," alisema Massawe.
Miezi kadhaa iliyopita, biashara ya ukahaba katika eneo hilo ilisambaratishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro kabla ya kurejea upya wiki chache zilizopita.
Mbali na biashara hiyo ya ukahaba, biashara za pombe za kienyeji, uuzaji na uvutaji wa bangi, matumizi ya dawa za kulevya na nyama choma zinazoandaliwa na kuuzwa katika mazingira machafu, pia vilirejea upya na kuendelea kufanyika kwa kasi kabla ya kusambaratishwa juzi na Mkuu huyo wa Wilaya.
Hata hivyo, Massawe amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa, kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha eneo hilo halitumiwi tena kuendesha biashara ya ukahaba na kuongeza kuwa jukumu hilo si la Kandoro.
"Hili si la Kandoro, hili ni la viongozi wa serikali za mitaa," alisisitiza Massawe