Na Waandishi Wetu
WAKATI bado Watanzania wakigugumia kutokana na maumivu ya mgawo wa umeme, uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) umeanza kampeni kubwa kuhakikisha bei ya nishati hiyo inapanda kwa asilimia 6 mwezi ujao.
Tayari kampeni za Tanesco kutaka kupandisha bei ya umeme na hivyo kuzidi kuongeza makali kwa mtumiaji, imekwisha kushika kasi, na sasa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura), imetoa muda wa siku saba kwa wananchi kutoa maoni yao kama bei ya umeme ipande kwa kiwango hicho au la.
Muda huo umetolewa kutokana na ombi la Tanesco la kutaka kupandisha bei ya umeme kwa kiwango hicho kuanzia mwezi ujao.
Iwapo umeme utapanda bei ifikapo Januari, hii itakuwa ni mara ya pili katika kipindi cha miezi sita. Bei ya umeme ilipanda mara ya mwisho Juni mwaka huu kwa asilimia tano ikifuatia ongezeko kama hilo Januari mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alitoa muda huo wakati akizungumza na watumiaji wa umeme wa majumbani na viwandani jijini Dar es Salaam jana.
Akitetea mapendekezo hayo, Mkurugenzi wa Tanesco, Adriaan Van Der Merwe, alisema Shirika lake limefikia uamuzi huo kutokana na mfumuko wa bei ambao alisema ulijitokeza baada ya bajeti.
Sababu nyingine inayolazimisha shirika hilo kutaka kupandisha bei ya umeme ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, ikilinganisha na kipindi cha nyuma.
Alisema endapo Ewura itaridhia ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 6, nishati hiyo sasa itakuwa ikiuzwa kwa Sh40 kwa uniti moja badala ya Sh38 kwa uniti za sasa.
Van Der Merwe alisema endapo wananchi watakataa bei ya umeme kuongezeka, basi serikali italazimika kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi inayolipwa na shirika hilo kwa asilimia 6 ili liweze kijikwamua na kuendesha shughuli zake bila ya hasara.
Kutokana na umuhimu wa ombi hilo, Masebu alisema mamlaka yake imeshindwa kupandisha bei ya umeme kama ilivyoombwa na shirika hilo na badala yake kwanza inataka kupata maoni ya watumiaji wa nishati hiyo, majumbani, viwandani na wengineo kuona kama wanaridhia au la.
Hii ina maana kuwa mbali na mgawo wa umeme, iwapo bei ya nishati hiyo itaongezwa Januari, Mtanzania wa kawaida atazidi kubebeshwa mzigo wa gharama za maisha.
Haijulikani iwapo mgawo wa umeme utakuwa umekoma hadi kufikia Januari, ingawa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kiwango cha megawati zilizopungua katika gridi ya taifa kitakuwa kimepatikana hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
Ombi la Tanesco kutaka kupandisha bei ya umeme, linakwenda kinyume cha rai aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete Januari mwaka huu alipowataka watendaji wa shirika hilo na wizara kuanza kufikiria kushusha umeme na si kupandisha kama wanavyofanya sasa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bernard Membe, ameishutumu Tanesco kwa utegemezi wake kwa serikali na kuagiza menejimenti ya shirika hilo kuchukua hatua kupunguza hali hiyo.
Akifungua mkutano wa 37 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Tanesco na kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu mpya wa Shirika hilo, Dk Idris Rashid jana, Membe alisema matatizo ya kifedha yanayolikabili shirika hilo yanasababishwa na shirika hilo kushindwa kukusanya mapato yake.
Naibu Waziri alienda mbali na kuhoji shirika hilo linaelekea wapi, kama litaendelea kuwa na matatizo hayo ya kifedha, yanayolilazimisha kukopa mara kwa mara.
"Kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji, shirika limekuwa likichukua mikopo ya muda mfupi ya zaidi ya Sh100 bilioni kwenye mabenki ya CRDB na Stanbic, hivi shirika litaendelea na hali hii hadi lini, kwa nini shirika halikusanyi madeni yake yote kwa wateja ili fedha hizo zisaidie kupunguza matatizo?" alihoji Membe.
Membe aliyeonekana kukerwa na utendaji wa sasa wa shirika hilo, alikemea tabia ya wafanyakazi wa shirika hilo kuwaacha wateja wake kulala katika giza katika baadhi ya maeneo kutokana na hitilafu ya umeme, ilhali hawapo katika mgao wa umeme, suala alilodai kuwa halikuwapo katika miaka ya nyuma.
Asema katika miaka ya themanini mameneja wa mikoa, viongozi wakuu na Tanesco makao makuu walikuwa tayari kutoka majumbani kwao bila kujali muda na kuhakikisha kuwa hitilafu iliyotokea inapatiwa ufumbuzi na umeme kurudishwa bila kuchelewa.
"Siku hizi wateja wanaweza kukaa siku tatu hadi wiki moja bila hata fundi wa Tanesco kwenda kuona tatizo ni nini, achilia mbali kulishughulikia, hii Tanesco ya sasa inakwenda wapi? Je wafanyakazi ndio wafalme ama wateja ndio wafalme? Mbona mmegeuza kauli mbiu hiyo ya huduma bora?" alihoji.
Pia aliitaka Tanesco kutafuta ukweli na kuisaidia serikali kufanya utafiti juu ya hali halisi ya matumizi mabaya ya maji katika maeneo ya mabwawa ya kuzalisha umeme, kuangalia namna itakayowezesha maji kupatikana katika mikoa yenye mabwawa hayo, hasa katika msimu ujao wa mvua na kufanya usimamizi wa kisayansi wa maji katika maeneo ya mabwawa.
Aliongeza kuwa pamoja na azima ya kuwa na vyanzo vingine vya umeme nchini, bado mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme kwa kutumia maji yaliyopo ya Mtera, Kidatu, Pangani na Hale yana umuhimu mkubwa kwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa mfumo wa uzalishaji umeme nchini.
Alisema tayari serikali imekwisha kuanza mpango utakaowezesha umeme kuzalishwa kwa kutumia makaa ya mawe katika mgodi uliopo Kiwira mkoani Mbeya unaotarajiwa kupanuliwa na kuzalisha megawati 200 ifikapo mwishoni mwa 2008 na Mchuchuma uliopo wilayani Ludewa, Iringa unaotarajiwa kuzalisha megawati 400 ambao upo mbioni kukamilika.
Mradi mwingine mbadala ni wa megawati 200 zinazotarajiwa kuzalishwa kwa kutumia gesi asilia itakayopatikana Kinyerezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Pamoja na Naibu Waziri Membe kuahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Tanesco aliyeteuliwa hivi karibuni Dk Idris Rashid anaimarisha na kuboresha shirika hilo, aliomba ushirikiano kwa wafanyakazi wa shirika hilo, ambao kwa pamoja walimhakikishia kumpa ushirikiano wa kipekee katika utendaji wao wa kazi.
"Tunaahidi kutoa ushirikiano wa kipekee hasa kwa menejimentri hii mpya kwa kuwa nio ya wazalendo wenzetu, tumekuwa tukijisikia vibaya kutokana na kuzongwa kufuatia matatizo ya umeme, tunakubali lawama hizo ila tunaahidi tutajitahidi kuondoa aina yoyote ya ubadhirifu na kuhakikisha kuwa misaada yote inayotolewa kwa shirika inatumika vyema kufuatana na malengo," alisema Joyce Ngahyoma, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Pwani alipokuwa akizungumza kwa niaba ya wenzake.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo mpya hakuwa tayari kuzungumza kutokana na ugeni wake katika nafasi hiyo, lakini pia kwa kuwa bado hajakabidhiwa rasmi ofisi yake kutoka kwa uongozi wa sasa wa Kampuni ya Kigeni ya Net Group Solutions (Pty) ambayo inamaliza muda wake mwisho wa mwezi huu.
Mkurugenzi wa Tanesco anayemaliza muda wake chini ya Kamapuni ya Net Group Sulutions Ltd, Adriaan van der Merwe, alitumia nafasi hiyo kuaga rasmi, alisema yeye na wenzake wapo tayari kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuwezesha shirika hilo. Soma maoni Uk. 6