Na Elizabeth Mjatta
ASKOFU wa Kanisa la The Blessing Africa la Marekani, Peter Mutafungwa (51), anayekabiliwa na mashitaka 30 ya utapeli wa Sh3 bilioni, ameionyesha mahakama majeraha aliyoyapata katika sehemu za siri kutokana na mateso anayodai kupata kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe.
Askofu Mutafungwa alifanya hilo jana, ikiwa ni siku ya kufunga utetezi wake, baada ya kutakiwa na Mwendesha Mashitaka, Maxmilian Biligi, kufanya hivyo kama alikuwa tayari.
Biligi alimuuliza mtuhumiwa huyo kama yuko tayari kuionyesha mahakama majeraha ambayo amedai kuyapata wakati akihojiwa katika kituo kikuu cha polisi.
“Mshitakiwa unaweza kuionyesha mahakama majeraha ambayo unadai kuyapata wakati ulipokamatwa ili utoe maelezo juu ya tuhuma hizo kutokana na ushahidi ulioutoa mahakamani hapa,” alisema Biligi.
Mtuhumia huyo raia wa Zambia, baada ya kuambiwa hivyo alikubali.
Baada ya kukubali, Mwendesha Mashitaka, aliomba Hakimu Neema Chusi aamuru watu wote kutoka nje ya mahakama ili mtuhumiwa aweze kuonyesha majeraha hayo kama kilelezo cha ushaidi wake alioutoa hivi karibuni.
Watu wote waliokuwa mahakamani, wakiwamo waandishi wa habari, walitoka nje na kuwaacha ndani mtuhumiwa na wakili wake, hakimu na mwendesha mashtaka, waliobaki kushuhudia ushahidi wa askofu huyo.
Novemba Mosi, Askofu huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa Zombe pamoja na askari wengine walimchoma kwa sindano za kushonea na kumtishia kumkata sehemu za siri kwa kutumia mkasi.
Alidai kuwa Zombe na wenzake wanne walitishia kumkata sehemu za siri, huku wakimtaka awape Sh3 milioni alizopewa na wafadhili.
Akijitetea jana mbele ya Hakimu Chusi,
Askofu Mutafungwa alidai kuwa, alikamatwa na askari na kupelekwa chumba cha giza na akiwa ndani ya chumba hicho, askari hao waliomkamata walimtukana kila aina ya matusi.
Alidai kuwa, siku hiyo ilipofika usiku wa manane aliingia Zombe na wenzake wanne aliowataja kwa majina ya Rehema Ramadhani, Rashid Mohamed, Hamis Bakari na Nasri Juma huku wakiwa na bisibisi, mkasi mkubwa, sindano za kushonea na nyembe na kumuamru avue nguo zote na kubakia uchi.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kutii amri hiyo, Zombe alitishia kumkata sehemu zake za siri kwa kutumia mkasi, huku wengine wakimchoma na sindano za kushonea katika sehemu hizo na kumtaka awapatie kiasi hicho cha fedha.
Siku hiyo, askofu Mutafungwa, aliomba amuonyeshe majeraha aliyoyapata Hakimu Chusi ambaye alibakia kimya na kutoa ishara ya kesi iendelee na kuendelea kumshangaa Zombe jinsi alivyomfanyia unyama huo.
Alidai kuwa, siku hiyo hiyo Zombe alifunua suruali yake aliyokuwa ameivaa na kumuonyesha bastola na kuongeza kuwa yeye ni mgonjwa wa kisukari, lakini alimnyimwa maji ya kunywa, chakula na dawa zake za ugonjwa huo.
Alidai siku ya tatu askari hao walimchukua na kumpeleka Kimara, sehemu anayoishi na kupekua mali zake ambako walichukua hati za kusafiria na kadi yake ya malipo ya benki kwa lengo la kumwacha masikini.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 5, mwakani kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu baada ya upande wa utetezi kufunga utetezi wao jana.