Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Jamii  »  LOWASSA: Wahamiaji haramu lazima warudishwe kwao
LOWASSA: Wahamiaji haramu lazima warudishwe kwao
By Habari Tanzania | Published  05/3/2006 | Jamii | Rating:
Utaratibu unaotumiwa na Waziri Mkuu Edward Lowassa kuwataka wananchi kuuliza maswali kuhusu kero zao mbele ya mkutano wa hadhara na kisha wahusika kutoa majibu papo hapo, unaibua changamoto kwa watendaji kuwajibika zaidi na wananchi kuwa na imani na serikali yao.
 
Kama ilivyokuwa kawaida katika mikutano yake yote aliyoifanya mkoani Kagera Aprili 20 hadi 24, Waziri Mkuu Edward Lowassa alikuwa akianza kwa kuwataka watu wenye kero mbalimbali kujitokeza na kujieleza hadharani.
 
Utaratibu huu ulikuwa ukionekana kuwavutia watu wengi ambao walikuwa wakijitokeza kuuliza maswali, kutoa ushauri na maoni yao kuhusu shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika ngazi ya kitaifa au katika maeneo wanayoishi.
 
Chini ya utaratibu huo, Waziri Mkuu alikuwa akiruhusu watu wasiozidi wanane kutegemeana na mazingira ya eneo na muda uliokuwepo.
 
Kwa utaratibu huo, Bw. Lowassa anasema asilimia tano tu ya maswali yote aliyokuwa akiulizwa na wananchi katika mikutano hiyo ilikuwa ikimhusu yeye kama Waziri Mkuu na asilimia 10 yalikuwa yakiwahusu mawaziri na asilimia kubwa iliyosalia ilikuwa ikihusu matatizo katika maeneo yao ambayo yangeweza kupatiwa ufumbuzi na wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Maafisa Watendaji wa Kata, Madiwani, Wabunge, Wakurugenzi, Wenyeviti na Mameya wa Halmashauri za Manispaa na Miji, Wakuu wa Wilaya na Mkoa.
 
Wananchi waliojitokeza kuuliza maswali au kutoa kero zao, waliweza kupatiwa majibu papo hapo.
 
Majibu hayo yalikuwa yakitolewa baada ya Bw. Lowassa kuwataka wahusika kusimama na kutoa majibu kufuatia kero iliyoelezwa na wananchi hao.
 
Mathalani, katika uwanja wa mashujaa wa Bunazi uliopo katika jimbo la Nkenge wilayani Misenyi mkoani Kagera, mwananchi aliyejitambulisha kuwa ni Vincent Kawa alitaka kujua Serikali inafanya nini katika kupambana na ushindani katika soko la kahawa, nini cha kufanya ili uishe na wao wapate bei nzuri.
 
Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Bw. Nazir Mustapha Karamagi alipata nafasi ya kujibu kero hiyo ambapo baada ya kusimama alisema, ’sio kweli soko la dunia la kahawa kila wakati linashuka.
 
Anasema lazima muangalie mnavyotayarisha shamba, mnavyolima, mbegu mnayoitumia, mnavyoitunza, mnavyovuna, mnavyoianika.
 
’Sisi tumezoea kuacha mibuni kuwa miti pori na tukivuna mazao yake yanakuwa hayana ubora unaotakiwa kimataifa?siku hizi soko linataka kahawa isiyokuwa na maganda lakini sisi tumezoea kuuza kahawa na maganda yake,’ anajibu.
 
Katika kutekeleza azma hiyo, Waziri Karamagi anahawakikishia wakulima hao kuwa Serikali itasambaza vinu vya kukobolea kahawa ili waache kuuza kahawa ya maganda na kwa kufanya hivyo anawahakikishia soko la uhakika na la bei nzuri.
 
Kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu Lowassa alipata nafasi ya kutembelea shamba la miwa la kampuni ya Kagera Sugar ambalo linalimwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji maji.
 
Alielezwa na meneja wa kiwanda hicho, Bw. Yahya akuwa kiwanda chake kinapenda kuwashirikisha wakulima wanaokizunguka.
 
Anasema kiwanda kitawapatia mbegu bora za miwa na watawasaidia matrekta ya kulimia mashamba yao kwa sharti kwamba shamba liwe la ekari zisizopungua 20 na zilizokuwa pamoja ili kurahisisha ulimaji.
 
Awali Bw. Anas Swaibu alionyesha wasiwasi wake kwamba makampuni mengi yamekuwa yakiwahamasisha kulima mazao kama vanilla, mkonge, pilipili na kisha kuingia mitini.
 
Alilalamika kuwa soko la uhakika la mazao hayo halijulikani lilipo na wao wamekata tama kuendelea na kilimo hicho.
 
Waziri Mkuu Lowassa alimtaka Bw. Yahaya kutoa ufafuzi wa azma yao na ndipo alipowahakikisha kwamba kiwanda kinataka kushirikiana na wakulima hao wadogo wadogo katika kilimo cha miwa.
 
Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuwachukua wakulima 200 na kuwapeleka Kilombero kujifunza kutoka wakulima wadogo wadogo wa miwa na kuona jinsi wenzao walivyobadilika kimaendeleo.
 
Mkazi mmoja Bi. Eufrasia Josephat alitoa kero ya fedha za noti na sarafu ambazo zimezeeka kuwa zinawaletea usumbufu katika biashara zao na Waziri Mkuu alisema suala hilo litafikishwa sehemu inayohusika na kutafutiwa ufumbuzi.
 
Katika eneo la Benako mahali ambapo miaka michache iliyopita kulikuwa na kambi ya wakimbizi zaidi ya milioni moja, Mzee Silvester Ntulijane 73, alitoa kero moja iliyowachekesha watu.
 
Alianza kwa kusema, mheshimiwa Waziri Mkuu nimesikia kuwa wahamiaji wote haramu watarudishwa makwao, sasa mimi ni kero moja ya mwanamke.
 
Nilikuwa nimeoa wake watatu na wote wamefariki. Kwa sasa nina mwanamke mmoja wa Rwanda ambaye nimezaa naye, sasa akirudishwa kwake nitaishi vipi katika umri huu.
 
Waziri Mkuu Lowassa alimtaka mkazi huyo kufuata taratibu iwapo anataka mke wake asikumbwe na zoezi la kurejeshwa kwao.
 
Alimwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kapteni Mstaafu John Chiligati ambaye alifuatana naye katika ziara hiyo kufuatilia suala lake na mara ya baada ya agizo hilo, Waziri Chiligati naye aliwaagiza maafisa wake wa uhamiaji kumsaidia mzee huyo.
 
Kero kama hiyo ilijitokeza katika kijiji cha Muhutwe wilayani Muleba ambako mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja aliomba kusaidiwa uraia wa Tanzania.
 
Mheshimwa Waziri Mkuu mimi katika kijiji hiki najulikana kama Mtutsi, sasa nimesikia kuwa kuna zoezi la kuwarejesha makwao wahamiaji haramu, nina wasiwasi na mimi ninaweza kukumbwa katika zoezi hilo, naomba nisaidiwe.
 
Katika kijiji hicho, Waziri Mkuu alipata kero kutoka wa wananchi wa eneo hilo kufuatia kuachiwa huru kwa watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mama mmoja kijijini hapo.
 
Walilalamika kwamba hakuna upelelezi wa makini uliofanywa na polisi kwenda kijijini hapo kupata ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani watuhumiwa.
 
’Ushahidi upo wa kutosha na hakuna polisi waliokuja hapa kuwahoji wananchi na wahusika na hivyo kupata ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani,’ alilalamika mama mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa.
 
Waziri Mkuu Lowassa alimtaka Kamanda wa Polisi wa Wilaya kutoa maelezo ya malalamiko hayo ambapo alisema kesi hiyo ilifutwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa kutumia Nolle Proseque.
 
Maelezo hao yaliwafanya wakazi hasa akina mama kulalamika zaidi, na ndipo Waziri Mkuu alisema hajaridhika na maelezo ya OCD na akamwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Ignas Mbinga kufuatilia malalamiko hayo.
 
Huko Ngara, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Samuel Ndomba anasema vyama vya upinzani katika wilaya yake vimekuwa kero.
 
Kanali Ndomba ambaye sio mstaafu kama wengine, mara kwa mara hupenda kuanza na cheo cha ’Afande’ kwa mkuu wake wa kazi.
 
Kwa mfano anasema, Afande Waziri Mkuu vyama vya upinzani hapa Ngara ni tatizo katika maendeleo.’
 
Wapinzani wengi hapa Ngara ni wahamiaji haramu kutoka Rwanda na Burundi na kwamba baadhi walitaka kuandamana kupinga kurejeshwa makwao.
 
Hapo Waziri Mkuu Lowassa anasisitiza tena msimamo wa Serikali wa kuwarejesha makwao wahamiaji haramu pamoja na mifugo yao.
 
Anahoji kuwa kama Serikali inawarejesha makwao wananchi wake waliovamia maeneo ya misitu inayohifadhiwa sembuse raia wa kigeni.
 
Anasema Tanzania sio shamba la bibi ambalo kila mtu anaweza kuja kufanya atakalo. Ni lazima warejeshwe makwao watake wasitake.
 
Hata akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani humo kwa madiwani, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri, Waziri Mkuu Lowassa alianza kwa kuwataka wenye kero kuzungumza kwanza.
 
Katika halmashauri hiyo kuna kero kubwa ya wapanda baiskeli na pikipiki ambao huzitumia kama biashara kwa kubeba abiria jambo ambalo limeleta mgongano mkubwa na watu wenye magari ya taxi.
 
Mgogoro huo unatokana na madai kwamba wenye pikipiki na baiskeli hawalipi kodi na kwamba sheria hairuhusu vyombo hivyo kufanya biashara ya kubeba abiria.
 
Diwani wa kata ya Bakoba CUF, Bw. Felician Bigambo alimwomba Waziri Mkuu kubadilisha sheria iliyopo ili baiskeli na pikipiki ziweze kutumika kama vyombo vya biashara kwa kubeba abiria.
 
’Sheria ibadilishwe ili kuwaruhusu vijana hawa kuendelea na biashara hiyo,’anasema na kuongeza, tuenzi ubunifu wa vijana hawa na pia tuige kutoka nchi jirani ambako vyombo hivi vinaruhusiwa kufanya biashara ya kubeba abiria.
 
Kwa upande wake, diwani wa kata ya Hamugembe (CUF), Bw. Nestor Akenyanya anaelezea miradi ya baiskeli na pikipiki kuwa ni ya wakubwa.
 
Anatoa madai hayo hasa kufuatia pale zoezi la kudhibiti biashara hiyo linapofanywa na polisi ambao baadaye hupewa kati ya Sh. 10,000 na Sh. 15,000 kwa kila mmoja ili waachiwe.
 
Anadai kuwa fedha wanazotoa vijana hao hawapati risiti yo yote.
 
Waziri Mkuu Lowassa alimtaka diwani huyo kuwataja hadharani wakubwa hao lakini anashindwa kufanya hivyo.
 
Huo ndio utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na Bw. Lowassa, utaratibu ambao umeonekana kuwa kisu kikali kwa watendaji ambao wanatakiwa kujua kazi zao vema na kuwajibika ipasavyo.
 
Katika majumuisho yake, Waziri Mkuu Lowassa anasema Serikali haina muda wa kupoteza katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM na imewataka madiwani, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri wasioweza kasi hiyo kujitoa wenyewe.
 
Aidha Waziri Mkuu alitoa muda wa mwezi mmoja kuanzia jana kwa viongozi wa halmashauri ya Bukoba kutatua tatizo la watu wanaotumia baiskeli na pikipiki kwa kufanya biashara ya kubeba abiria.
 
Alisema baada ya muda huo, wampelekee taarifa ya jinsi walivyolitatua tatizo hilo kabla ya yeye kutoa uamuzi.
 
Kuhusu utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, Waziri Mkuu amewapiga marufuku wenyeviti na wakurugenzi kufanya safari za mara kwa mara za Dar es Salaam na Dodoma na badala yake amewataka kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi na kutatua matatizo yao.
 
Anawataka viongozi hao kwenda vijijini kutatua matatizo ya wananchi.
 
SOURCE: Nipashe

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.