Na Mwandishi Wetu
WATUMISHI 19 katika Wizara ya Maji wamebainika kwamba walijipatia ajira kwa kutumia vyeti vya kughushi.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Patrick Rutabanzibwa imesema Wizara imehakiki vyeti vya watumishi wake walioajiriwa Mei na Agosti, mwaka huu na kubaini kuwa 19 kati ya 63 walioajiriwa walitumia vyeti vya kughushi ili kupata ajira.
Taarifa ya Katibu Mkuu ilisema kazi ya kuhakikisha vyeti ilifanyika kati ya Oktoba na Novemba, mwaka huu kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na Baraza la Mitihani la Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa vyeti vilivyobainika kuwa ni vya kughushi ni vya kidato cha nne na walioabainika kuwa na vyeti hivyo ni Mafundi Sanifu wawili, Karani wa Masjala mmoja, katika Muhtasi mmoja na madereva 15.
Rutabanzibwa alisema suala hilo limeripotiwa polisi kwa hatua za kisheria na tayari baadhi ya watuhumiwa wamesimamishwa kazi na wanahojiwa na Jeshi la Polisi.