Na Grace Msovela, Arusha
MAKAMU wa Rais, Dk. Ali Mohamed Sheni, amezitaka nchi za Afrika kufufua upya mfumo wa utendaji kazi serikalini, kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa jamii na kubuni teknolojia mpya.
Dk. Sheni alitoa wito huo jana wakati akifungua mkutano wa 28 wa kimataifa wa Jumuia ya Wataalamu wa Utawala na Menejimenti barani Afrika, uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Makamu wa Rais alisema ni vizuri kwa nchi za Afrika kuboresha miundo ya utoaji huduma kwa umma kwa kutumia teknolojia mpya, kwa lengo la kutoa huduma bora.
“Tunahitaji kujiuliza kwamba idadi ya rasilimali watu haitoshi kuweza kutoa ushindani kitaaluma,” alisema.
Dk. Sheni alisema serikali kuu katika nchi za Afrika haziwezi kutoa huduma bora bila ya kuzishirikisha ngazi mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo sekta binafsi na mashirika ya kiraia.
Makamu wa Rais alisema kuwa nchi za Afrika zinayo nafasi nzuri ya kusonga mbele katika kutoa huduma bora kwa wananchi wake, endapo menejimenti zitafuata taratibu zilizowekwa zisizo kuwa na ubabaishaji na ukwepaji wa majukumu yao.
Mkutano huo wa siku nne utajidili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchambua changamoto zinazoikabili sekta ya utumishi wa umma katika kutoa huduma zake, kwa mantiki ya kuziboresha ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Washiriki katika mkutano huo mbali na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ni Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia ambaye pia ndiye Mwenyikiti wa Mkutano huo.
Wengine ni Mawaziri, Makatibu wakuu, wakuu wa taasisi za kitaifa na kimataifa, wataalamu wa masauala ya utawala, maendeleo na biashara, viongozi wa maeneo ya biashara, mashirika ya biashara, mabenki na uwekezaji, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, NEPAD, COMESA, ECOWAS, SADEC na makundi mengine ya kikanda.