Yatima ‘waliotapeliwa’ nyumba wawasilisha vielelezo kwa DC
Na Mbazigwa Hassan
MKUU wa wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Luteni Abdallah Kihato, jana asubuhi alipokea vielelezo kutoka kwa watoto yatima wanne ambao nyumba yao ya urithi inadaiwa kuuzwa na mtu wasiyemfahamu, katika Mtaa wa Sandali, manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari hii alikuwepo katika ofisi ya mkuu wa wilaya wakati watoto wawili kati ya wanne walipowasilisha vielelezo muhimu vinavyoonyesha hatua zilizohukuliwa na uongozi wa serikali ya mtaa na kata kabla ya nyumba hiyo kuuzwa.
Miongoni mwa vielelezo vilivyokabidhiwa ni wosia wa marehemu bibi yao, Hidaya Mohamed, barua za kata kuiomba mahakama ya Mwanzo Temeke kutomtambua Seif Abdallah kuwa msimamizi wa mirathi na barua ya kuiomba mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wa Wilaya ya Temeke kutobadilisha hati ya kiapo ya kubadili jina la mmiliki wa nyumba hiyo.
Vielelezo vingine ni nakala ya hukumu ya mahakama ya Mwanzo Temeke kuhusu mirathi namba 48/2006 na barua ya mahakama hiyo kwenda kwa mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Sandali, ikimwamuru kutoa fomu ya makazi ya nyumba ya marehemu kwa mnunuzi kama alivyoagizwa na ofisa ardhi wa manispaa ya Temeke.
Maelezo ya barua hiyo ya Novemba 8, 2006 yanamwagiza mwenyekiti huyo kutoa fomu hiyo mara moja ili mnunuzi wa nyumba aweze kuipelekea idara ya ardhi kwa ajili ya kubadilisha jina.
Luteni Kihato alimwambia mwandishi wa habari hii kuwa, pamoja na uongozi wa kata husika kuchelewa kulifikisha tatizo hilo kwake mapema, analishukuru gazeti la Uhuru kwa kutoa taarifa za suala hilo na hivyo kuwawezesha kufahamu kilichotokea.
Alisema atapitia barua zote kwa makini na kutoa maelezo baadaye kuhusu suala hilo, na kuongeza kuwa baada ya hapo atafanya mazungumzo na wahusika wengine katika kutafuta ufumbuzi.
“Leo (jana) nitakuwa na kazi ya kupitia barua hizi kwa makini sana, na kwa kuwa vielelezo vyote muhimu viko mezani kwangu, kazi iliyobaki ni ya kutafuta ukweli wa malalamiko ya watoto hawa. Nitatoa taarifa mapema,” alisema.
Alisema kutokana na maelezo aliyopewa na watoto hao, ambao wana umri chini ya miaka 15, ameanza kupata picha ya suala hilo, japo hakupenda kufafanua zaidi.
Hatua ya Kihato kulipokea suala hilo inafuatia taarifa zilizochapishwa na gazeti hili kuhusu malalamiko ya watoto hao ambao mpaka jana walikuwa wakiendelea kuishi katika nyumba hiyo iliyofungwa vyumba vyote, isipokuwa chumba chao.
Katika malalamiko yao, wameeleza kuwa hawajawahi kumuona Seif aliyedai kuwa baba mdogo wa marehemu bibi yao, na kwamba hawana kumbukumbu yoyote kuhusu mtu huyo kama ni ndugu yao kwa sababu kawakuwahi kumwona wakati wa uhai wa marehemu bibi yao.
Jackline James, aliyefuatana na kaka yake, Jerry James alimwambia mwandishi wa habari hii muda mfupi baada ya kuzungumza na mkuu wa wilaya kwamba ana matumaini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi kutokana na linavyoshughulikiwa na serikali.
Alisema kuwa kitendo cha kudhulumiwa nyumba yao ya urithi, ambayo ni haki yao, kinaweza kuwaharibia maisha yao na kujikuta wakihangaika mitaani, jambo ambalo litawaongezea unyonge.