Na Festo Polea
RAIS Mstaafu, Benjamini Mkapa, amezungumzia matatizo ya umeme yanayoikabili Tanzania na kuelezea kufurahishwa na mpango wa serikali wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Stigglers Gorge katika mto Rufiji na kutumia vyanzo vingine mbadala.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ibada ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza utawala wake wa miaka 10 na kutimiza miaka 40 ya ndoa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Upanga, Mkapa alisema matatizo yanayotokea kuhusiana na umeme yanasababishwa na kutegemea mabwawa kama chanzo pekee.
Alifurahishwa na mikakati ya serikali ya kutaka kutumia njia mbadala za kuzalisha umeme akitolea mfano umeme wa nguvu za jua.
Alisema mradi wa umeme wa Stingglers Gorge, ulikuwepo tangu ya awamu ya kwanza na walijaribu kuutumia lakini ilionekana kuwa na gharama kubwa za uzalishaji na lingezalisha umeme mwingi ambao ungezidi matumizi ya Watanzania kwa wakati huo.
“Kipindi kile hatukuweza kwani umeme ungezalishwa mwingi bila matumizi na ungekuwa na gharama kubwa kuuzalisha lakini sasa itabidi serikali ifanye hivyo, nafikiri suluhisho litafikiwa kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya nne,” alisema Mkapa.
Akizungumzia maisha yake ya sasa baada ya kustaafu urais, Mkapa alisema serikali ya awamu ya nne inamjali na kumpa heshima zake zote anazostahili.
Alisema amekuwa akisafiri mara kwa mara kushiriki katika mikutano ya kujadili jinsi ya kuondokana na umaskini katika nchi za dunia ya tatu.
Alisema kuwa watu mbalimbali wamekuwa wakitaka busara zake na mchango wake naye bila kinyongo amekuwa akiudhuria mikutano hiyo inayofanyika katika mataifa mbalimbali.
Akielezea misa hiyo ya shukrani ya kumaliza salama kwa miaka 10 ya uongozi wake na kufanikiwa kuwa katika ndoa na mama Anna Mkapa kwa miaka 40, alisema aliifanya misa hiyo maususi kwa kuwaombea viongozi waliokuwepo katika serikali yake iliyopita na sasa wapo katika serikali ya awamu ya nne.
Aliomba watu wenye kinyongo naye kumsamehe kwani katika uongozi wake alikuwa akiwatendea haki Watanzania wote kwa ujumla na si mtu binafsi.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycapy Kadinali Pengo, alisema ni changamoto kwa viongozi wa siasa kutoa shukrani kwani wamezoea kuomba kura na kuingia mitini bila kushukuru na alimshukuru Mkapa kwa kuonyesha moyo wa imani wa kwenda kushukuru.
Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na siasa wakiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Philip Mangula