Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uwanja wa Fisi wamvuta shati Kandoro
Uwanja wa Fisi wamvuta shati Kandoro
By Habari Tanzania | Published  12/4/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Muhibu Said

BIASHARA ya ukahaba katika eneo la Uwanja wa Fisi, Manzese, jijini Dar es Salaam iliyosambaratishwa miezi kadhaa iliyopita na Mkuu wa MKoa, Abbas Kandoro, imerejea upya na hivi sasa wahusika wanaendelea kama kawaida, Mwananchi imethibitisha.

Mbali na biashara hiyo ya 'uchangudoa', biashara za pombe za kienyeji, uuzaji na uvutaji wa bangi, matumizi ya dawa za kulevya na nyama choma zinazoandaliwa na kuuzwa katika mazingira machafu, vimerejea upya na zinaendelea kufanyika kwa kasi.

Uchunguzi wa Mwananchi umethibitisha kuwa wanawake wanaouza miili yao wanaendelea kulitumia eneo hilo kama sehemu yao ya mawindo na hakuna juhudi zinazoendelea kudhibiti vitendo hivyo sasa.

Mwananchi ambayo ilifika katika eneo hilo katika nyakati za usiku imeshuhudia wanawake hao wakipatana na wateja wao na kisha kuwapeleka katika vyumba inamofanyika biashara hiyo ya ngono.

Vyumba hivyo vilivyoko katika baadhi ya nyumba zilizoko katika eneo hilo, vimekodiwa na baadhi ya makahaba na changudoa hao wanapofikia muafaka na wateja wao, hutumia vyumba hivyo kutimiza haja za wateja wao kwa makubaliano ya kuwalipa makahaba hao kiwango maalum cha fedha.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa, wanawake hao hukodi vyumba hivyo kwa kuwalipa makahaba hao kati ya Sh500 hadi 3,000 kulingana na muda anaouhitaji mteja kutimiza haja zake. Au huwapeleka wateja wao kwenye nyumba za kulala wageni zilizoko jirani au mbali na eneo hilo.

Mteja hutozwa, kuanzia Sh500 na kuendelea kulingana na muda, aina ya ngono, kuvaa au kutokuvaa kondom na 'starehe' nyingine atakazokuwa amepatana kuhudumiwa na mwanamke.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono, ni wa umri wa unaoanzia miaka 12 na kuendelea na hufika katika eneo hilo, kuanzia saa 12:00 jioni hadi 11:00 alfajiri.

Hali hiyo mbali ya kutishia usalama wa afya za wanawake hao na wateja wao, imekuwa ikiwasababishia pia kero wapita njia wanaopita katika eneo hilo kutokana na bughudha za kuitwa na kushikwa kwa nguvu na wanawake hao.

Mwananchi ilishuhudia pia pombe za kienyeji aina ya mnazi na nyama choma zikiendelea kuuzwa katika mazingira machafu kama kawaida.

Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa jirani na eneo hilo wamethibitisha kuwa wanawake hao walirejea wiki chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, kuendesha operesheni kali ya kuwaondoa wanawake hao katika eneo hilo.

Katika operesheni hiyo iliyofanywa na polisi kwa kushirikiana na askari wa manispaa, ulifanyika uvunjaji wa vibanda vilivyojengwa katika eneo hilo na kutumiwa na wanawake hao kama sehemu ya kuendeshea biashara ya ngono.

Pia ilihusisha amri ya kufunga milango ya baadhi ya nyumba zilizoko katika eneo hilo zilizokuwa zikitumiwa na makahaba hao kuendesha shughuli zao na kuwaondoa wafanyabiashara wa pombe za kienyeji na nyama choma.

Amri ya kufunga milango ya nyumba hizo, ilitokana na wanawake hao kutumia mlango wa mbele kuingiza wateja na kisha kuwapitisha katika mlango wa uani baada ya kutimiza haja zao.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Muungano, Kata ya Manzese, Joseph Mkude, alipoulizwa, alikiri wanawake hao kurejea katika eneo hilo na kumtupia lawama Mkuu wa Wilaya ya Kiondoni, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, kwamba ndiye anayepaswa kubeba msalaba huo kukwamisha kasi ya bosi Kandoro.

Mkude, alidai Massawe ameshindwa kutimiza ahadi aliyoitoa hivi karibuni ya kuweka ulinzi wa askari katika eneo hilo ili kuhakikisha biashara hiyo chafu hairejei.

"Matokeo yake, eneo limebaki huru," alisema Mkude na kuongeza: "wangepatikana japo askari watatu tu, tungewaondoa wote hao changudoa".

Hata hivyo, Mkude, alisema wamekuwa wakijitahidi kulitembelea eneo hilo na kuwahamasisha wakazi kufanya usafi, kumwaga pombe za jinsi hiyo na kuwaamuru baadhi ya wakazi walioanza kujenga katika eneo hilo kuvunja majengo yao.

Massawe kwa upande wake, alizirejesha lawama hizo kwa polisi na wenyeviti wa serikali za mitaa, kwamba wameshindwa kutekeleza wajibu wao kwa kuwa wao pia wanapaswa kuwaondoa wanawake hao katika eneo hilo.

"Polisi na wenyeviti wa serikali za mitaa, hao ni serikali pia, kwanini wasiwaondoe (hao changudoa)?," alihoji Massawe na kuongeza: "Si umeona jinsi tulivyovunja vibanda pale? Na umeona tumeweka alama za X. Nashukuru kwa kunifahamisha hilo (la kuweka ulinzi wa askari), tutalishughulikia na utaona mambo yatakuwa mazuri".


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.