Baada ya kuwaacha wengine wachangie kwa kina juu ya suala zima la muungano unaokuja wa Afrika ya Mashariki, nami pia nimeonelea ni vyema basi nitoe mchango wa mawazo yangu ili angalau kwa kiduchu niweza kuchangia katika mjadala mzima wa suala hili.
Msimamo wangu ni kuwa, Tanzania haiwezi kuwa kisiwa, na peke yake haitapiga hatua kubwa ya maendeleo inayotaka na haitatosheleza matamanio ya watoto wake. Vivyo hivyo, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi (katika eneo la Afrika ya Mashariki) kama nchi moja moja zitaendelea kutamani mafanikio ya haraka lakini matamanio hayo yataendelea kuwa njozi isiyotimia.
Ni kwa sababu hiyo basi naungana na wale wote ambao wanataka Shirikisho hilo, tena lije mapema kwa manufaa ya watu wetu na manufaa ya vizazi vyetu. Nina sababu kadhaa ambazo zinanisukuma kuja na msimamo huo.
Hata hivyo, kabla sijanyambulisha, kupambanua, na kuchanganua sababu hizo nina machache ya kusema kuhusu mjadala mzima na jinsi ambavyo inasikitisha kuona kuwa badala ya kujadili kiustaarabu na kindugu mara nyingi mjadala huo umekuwa ni wa kibaguzi, kutafuta sifa, na zaidi ya yote kuonesha ujuzi usio na msingi na visingizio vya uzalendo uliopotoka.
Nilisikitika zaidi hasa niliposoma maneno ya mwandishi wa Kinyarwanda Job Jabiro katika makala yake aliyoiita Cry Tanzania, Cry Beloved Country iliyochapishwa katika gazeti la The News Times la nchini humo October 13, 2006.
Maneno yaliyonishtua katika makala hiyo kauli za ufunguzi ambapo mwandishi huyo alidai kuwa Kamwe sikujua kuwa itakuja siku ambapo nitailinganisha Tanzania ya mpendwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na DRC ya Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Zabanga. Nahofia kuwa, kama mambo yataendelea kama yalivyo, nitajikuta nikifanya hivyo (tafsiri ya Kiswahili toka Kiingereza ni yangu).
Maneno hayo ya ufunguzi wa makala yake hiyo yalikusudia kushtua na kuumiza mioyo ya Watanzania mahali popote walipo duniani. Na kweli yalishtua na kuchoma kama ncha ya kisu kikali. Inahitaji ujasiri wa hali ya juu kuilinganisha Tanzania na DRC katika kipindi chochote cha historia za nchi hizo!!
Baada ya kusoma makala hiyo na kuirudia mara kadhaa sikuona hata mahala pamoja ambapo palinifanya niamini sababu ya mwandishi wa makala hiyo kutumia maneno makali namna hiyo, isipokuwa tu akiwa na lengo jingine kabisa, nalo ni kuchepushia pembeni hoja muhimu zinazotakiwa kuzungumzwa na wana Afrika ya Mashariki na kuzirahisisha kwa kudai kuwa Watanzania wanahofu na shirikisho la Afrika ya Mashariki kwa sababu wana chuki na wahamiaji/wageni nchini mwao.
Kama tabibu aliyebingwa, Bw. Jabiro anadai kwa ujasiri kuwa ametembelea tovuti ya www.habaritanzania.com na kuikuta tovuti hiyo ikijaza nchi ya Nyerere, sumu isiyofikirika ya chuki dhidi ya wageni. Na akaongeza kuwa Nyerere atabingirika kwenye kaburi lake kwa hali hiyo!
Mengine yote anayoyasema ni maneno ambayo tumeyasikia toka kwa baadhi ya ndugu zetu wa Kenya, na Waganda, nayo ni marudio ya hoja hiyo hiyo kuwa Watanzania ni waoga na wanachuki dhidi ya wageni (xenophobia).
Ukweli wa mambo ni kuwa hakuna ushahidi wowote ule isipokuwa ule ulio katika akili ya Bw. Jabiro kuwa Watanzania wana chuki dhidi ya wageni. Hatuna chuki hiyo, hatujawahi kuwa nayo, na sifikiri kuwa tutaanza sasa kuwa nayo!
Madai kuwa Watanzania wana chuki dhidi ya wageni ni tusi, kejeli, na kashfa nzito ambayo hakuna Mtanzania mwenye akili timamu ambaye hatajihisi kukosewa.
Tatizo la Bw. Jabiro na baadhi ya waandishi wenye msimamo kama wa kwake ni kutokuelewa au kutokutaka kuelewa kwanini Watanzania wanasitasita, na hawashangilii ujio wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki. Siyo kwa sababu hawajui faida zake, siyo kwa sababu ni wapumbavu, na siyo kwa sababu tuna chuki dhidi ya wageni!!
Kwa kifupi, ni kuwa watanzania wanasita kufurahia shirikisho hili sababu ya historia yao na jinsi ambavyo mara nyingi katika historia hiyo wamejikuta wakitoa zaidi na kupokea kidogo!
Siyo utoaji wa mali tu bali wametoa hata maisha yao kwa ajili ya wageni, lakini wao wenyewe wakiwa patupu!! Kama kura za maoni za www.habaritanzania ni kielelezo chochote Watanzania wanapinga kujiunga na shirikisho hilo kwa muda huu wakiwa mbele kwa zaidi ya 2/3 ya kura hizo.
Hivyo, kwa nchi ambayo imewakaribisha wageni wengi, na ambayo yenyewe ni mchanganyiko wa makabila mageni, madai kuwa tunaogopa wageni au tunachuki nayo yanakera, yanaudhi, na ni msingi mbaya wa kujenga shirikisho hilo.
Kama nilivyosema hapo juu, siyo kusudio langu kuorodhesha au kuainisha kwa kina sababu zinazowafanya Watanzania kutokuwa na hamasa ya Shirikisho hilo kwani wengi wameshafanya hivyo kwa ufasaha mkubwa katika sehemu mbalimbali.
Hata hivyo kwa upande wangu, licha ya mapingamizi yanayotolewa na Watanzania wenzangu dhidi ya shirikisho hilo naona nijenge hoja ya kwanini Shirikisho hili ni la lazima, la kiasili, na ambalo halina budi kukaribishwa kwa haraka na kwa matumaini.
Kabla ya kufanya hivyo, sina budi kukiri kuwa msimamo wangu wa kuunga mkono ujio wa shirikisho hilo na kufanya hima kujiunga nalo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mawazo ya Mwalimu juu ya Umoja wa Afrika na hasa juu ya Umoja wa Afrika ya Mashariki. Hivyo hoja zangu hizi ambazo ninmezijenga baada ya kuelewa kwa kina kwa nini Mwalimu alitaka Afrika ya Mashariki iungane licha ya pingamizi za wakati huo.
Tofauti kubwa iliyopo ni kuwa kwa wakati huu raia wa kawaida kama mimi tuko huru kutoa mawazo yetu na kuonesha misimamo yetu bila ya hofu ya serikali au kaka mkubwa.
Swali ambalo nimejiuliza na kujaribu kupata majibu yake ni kuwa, ni kwa nini Watanzania inawapasa wakubali, wafurahie, na waharakishe ujio wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na kuwa tayari kujiunga nalo badala ya kukaa nje na kuendelea kuonesha mapungufu yaliyopo katika mchakato mzima wa uundwaji wa shirikisho hilo? Yafuatayo basi ni majibu yangu.
Sababu ya kwanza na ya msingi ni kuwa, Tanzania ndiyo nchi pekee katika bara la Afrika ambayo imeundwa kutokana na muungano wa nchi mbili huru. Hivyo, tumeonesha siyo tu nia ya kuungana bali piwa uwezo wa kuungana.
Ni kweli kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar si mfano mzuri wa jinsi nchi zinavyopaswa kuungana, lakini ukweli wa uwepo wa muungano huo ni mfano wa kuigwa na Watanzania hawana budi kuonesha kuwa kuungana kwa nchi inawezekana.
Tangu kabla ya uhuru wetu, nadharia na haja ya umoja wa Afrika ilionekana na Tanzania imekuwa ni kinara na mtetezi wa dhana na ukweli huo. Jinsi ambavyo tumeweza kuhimili mikikimikiki ma kashkash zilizoutetemesha muungano wetu, hata hivyo kwa miaka zaidi ya 40 tumeweza kuulinda, kuutetea na kuenzi.
Ni kwa sababu hiyo basi, watanzania inawapasa wawe vinara na wawe wa kwanza kukumbatia shirikisho hili na kuwa tayari kuonesha ni makosa gani yasifanyike katika kuungana huku. Ninachosema hapa ni kuwa ni wito wa Tanzania kuchangamkia umoja wa Afrika kwani ni sehemu ya urithi wetu.
Mwalimu Nyerere akihutubia kikao cha Bunge kilichoridhia muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 25, 1964, Mwalimu alisema, nchi ambazo ni marafiki na majirani na ambazo katika historia yao zimewahi kuwa kuwa pamoja, zina wajibu wa pekee.
Kama zikishindwa kuungana , basi kushindwa huko kutatumika kama sababu ya kunyoshea kidole cha dhihaka kwa bara letu. Ila endapo zitaungana, na kufanya umoja huo kuwa halisi, basi watadhihirisha kuwa matumaini ya bara letu si ya bure. Kama nchi mbili zaweza kuungana, basi nchi tatu zaweza; na kama nchi tatu zaweza basi nchi thelathini zaweza!
Wiki chache baadaye, Mei 10, Mwalimu Nyerere alizungumza na waandishi wa habari akiwapokewa wabunge waliokuwa wakitembelea nchi hizo tatu kutaka ziharakishe uundwaji wa shirikisho.
Utabiri alioutoa hapo, umebakiwa kuwa kweli. Mwalimu alisema kuwa Nakubaliana kabisa kuwa endapo muungano hautafikia muda mfupi baada ya uhuru, itakuwa vigumu sana kuufikia hapo baadaye. Hivyo basi, kwa Watanzania muungano wa Afrika ya Mashariki ni njozi yetu, ni jukumu letu, na ni wito wetu.
Mwalimu (na ninakubaliana naye) alisema kuwa tofauti iliyopo kati ya nchi za Afrika ya Mashariki wakati ule zisiwe kizuizi cha kuungana kwani matatizo mengi yanaweza kutatuliwa kwa kadiri tunavyoendelea. Mfano mzuri hadi leo hii ni Muungano wa Marekani ambapo kwa zaidi ya miaka 200 Majimbo na Serikali ya Shirikisho yanaendelea kuangalia ni jinsi gani yanaweza kuhusiana zaidi na kuondoa kero zozote zilizopo.
Ni kujidanganya na kujikanganya kudhani ya kwamba sisi watu Waafrika ya Mashariki ni lazima tuondoe tofauti zote ndipo tuungane!! Nakubali kuwa ni lazima tujaribu kwa kadiri inavyowezekana kupunguza tofauti hizo na zile ambazo zapaswa kuondolewa kabisa ziondolewe na zile ambazo zaweza kuondolewa baada ya muda ziwe hivyo, lakini kuungana kwetu kusikome!
Hivyo muungano, watu wa Afrika ya Mashariki siyo muungano wa vyombo vya uzalishaji mali, majeshi, mahakama, taasisi n.k bali ni lazima uwe muungano wa watu wenyewe!
Hilo ndilo jambo la msingi na ambalo halina budi kutiliwa mkazo. Tunachotaka kuunganisha si mipaka ya Namanga na Hororo, au Mutukula na Ngara! Tunachotaka kuunganisha ni watu wetu ambao kwa asili na kwa damu ni wamoja. Ni kurejesha muungano wa asili katika sehemu hii ya Afrika.
Sababu ya tatu ni kuwa, bila kuungana eneo la Afrika ya Mashariki litaendelea kuwa nyuma licha ya jitihada za kila nchi kuleta mafanikio kwa watu wake. Kuna watu wanataka tuamini kuwa Wakenya wako mbali sana kimaendeleo kuliko Tanzania au Waganda na Wanyarwanda wako nyuma kwa masuala ya usalama kuliko Tanzania.
Na wapo wale ambao wanaona kuwa nchi zetu zina matatizo mengi kiasi cha kuwa kikwako cha kuungana kwetu. Ukweli ni kuwa Kenya haipo mbali sana kiuchumi ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki.Katika ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Mwaka 2005 ( Human Development Report 2005 ), Kenya iko nafasi ya 152, wakati Tanzania ipo nafasi ya 162, Uganda 145, Rwanda 158, na Burundi 169.
Kwa kuangalia ripoti hiyo na nyingine nyingi ukweli mmoja ni dhahiri kuwa nyingi ya ripoti hizo hazioneshi hali halisi iliyopo! Ni kweli kuna tofauti ya kiuchumi (ingawa si ya kimaisha kwa ujumla) kati ya nchi zetu, je hiyo ni sababu tosha ya kufanya tusiungane? Jibu langu ni Hapana!! Ni sababu tosha ya kutufanya tuungane!!
Sababu ya tatu ni kuwa, faida ya kuunganisha nchi zetu inapita hasara ya kutoungana kama nchi zetu zitaendelea kuwa moja moja. Wale wanaodhani kuwa Tanzania kama nchi moja itapiga hatua kubwa ya maendeleo kwa haraka kuliko kama itaungana na dada zake watu hao wanajidanganya.
Ni kweli kuwa kama tukifanya mambo yetu sisi wenyewe, sera zetu sisi wenyewe, uongozi wetu sisi wenyewe, tutaendelea; lakini maendeleo hayo yatakuwa ya pole pole. Tukiungana tunaweza kuyakabila matatizo ya nchi yetu kwa pamoja, matatizo ambayo yamechukua muda kutatulika katika nchi zao.
Tatizo la ardhi Kenya pamoja na mambo ya ukabila, vita vya kaskazini mwa Uganda kati ya UPDF na LRA pamoja na mfumo wa kisiasa huko Uganda, masalio ya machungu ya vita huko Rwanda na Burundi, na tatizo la kisiasa la Tanzania Bara na Zanzibar ni matatizo ambayo yanaweza kukabiliwa na kutatuliwa kwa pamoja, kwani zaidi ya miaka 40 nchi zote zimeshindwa kuyatatuta matatizo hayo!!!
Nitawapa mifano halisi. Ulaya ambayo leo inatolewa mfano wa muungano, imetoka katika historia ya maumivu ya vita na migongano ya ndani. Ujerumaini ikifuata sera za kinazi (chini ya Adolf Hitler)na Italia (ya Musolini) ikifuata Ufashsti leo hii zimeweza kuungana na nchi ambazo zilikuwa adui yaani Ufaransa na Uingereza.
Na hivi sasa nchi hizo za Ulaya ziko karibuni kuiingiza Uturuki katika Umoja huo wa Ulaya, watu wenye historia ya mapinduzi ya kijeshi! Kama wao wanaweza, bila ya shaka na sisi tunaweza. Hata muungano wa mataifa ya Marekani (siyo majimbo kwa maana yetu), wametoka katika historia ya vita vya wenyewe kwa wenyewe (kaskazini na kusini) vita ambayo hadi vilipomaliza zaidi ya wamarekani laki sita waliuawa!!
Hali ya maisha kati ya Kusini na Kaskazini ilikuwa ni tofauti sana, lakini hiyo haikuwa sababu ya kutokuungana au kuvunja muungano! Ilikuwa ni kichocheo cha kudumisha na kuboresha muungano. Hata baada ya risasi ya mwisho kurindima, baadhi ya majemedari walitaka kuidhabu kusini kwa kutaka kujitenga lakini Rais Lincoln alikataa kabisa kwa kuwaambia majemedari hao kuwa hao wa kusini ni ndugu zao!!!
Kwa mtazamo wangu, jambo la maana kwa Tanzania siyo kukaa pembeni au kuhofia ujio wa shirikisho bali kushiriki kikamilifu katika hatua zote za uundwaji wake.
Msingi mkubwa wa kushiriki huko ni ushirikishwaji wananchi katika mjadala mzima. Serikali ni lazima izungumze na Watanzania na kujenga hoja ya kwanini ni muhimu tuungane badala ya kudhania kuwa Watanzania wote wanaelewa umuhimu wa shirikisho hilo.
Kuendelea kupiga debe tu hakutoshi bali tuzungumze kwa pamoja. Katika sehemu ya pili ya makala hii, nitazungumzia ni hatua gani wana na mabinti wa Afrika ya Mashariki wanaweza kushiriki kikamilifu katika uundwaji wa shirikisho hili katika muda unaofaa na shirikisho ambalo siyo la kuwafurahisha viongozi bali lenye kuwaletea heri, matumaini, na maendeleo vizazi vijavyo vya wana Afrika ya Mashariki.