Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Habari za uhalifu hazifai kwa wawekezaji
Habari za uhalifu hazifai kwa wawekezaji
By Habari Tanzania | Published  06/8/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Balozi wa Uswisi hapa nchini, Bw. Emanuel Jenni amevishauri vyombo vya habari kubadili mwelekeo wa kuandika na kutangaza habari zinazohusiana na jinai, ili kuepuka hatari ya kusababisha wawekezaji wa nje kutofungua biashara mpya hapa nchini.

Alisema, waandishi wa habari wanapaswa kujihusisha na mambo ya msingi yatakayochangia kuinua uchumi wa nchi, kwa vile kuna baadhi ya wawekezaji wanaotishwa na habari zinazohusiana na matukio ya jinai kwenye vyombo vya habari.

Bw. Jenni aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), Bw. Reginald Mengi ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yatakayochangia kuimarisha ushirikiano kati ya makampuni ya biashara kati ya Tanzania na Uswisi.

Hata hivyo, Bw. Mengi alisema matukio kama ujambazi, vitendo vya uporaji wa kutumia silaha na wizi kwenye mabenki na taasisi za fedha, vinajulikana sana kutokana na uwazi uliopo nchini na uhuru wa vyombo vya habari vinavyotoa kipaumbele kwa matukio hayo.

’’Lakini kuna nchi zenye matukio kama hayo yanayotokea kwa kiwango cha hali ya juu sana ikilinganishwa na Tanzania, na unapoangalia vyombo vyao vya habari, utayakuta kwenye kurasa za mwisho za magazeti...yaani hazipewi kipaumbele,’’alisema.

Bw. Mengi alisema Tanzania ina vivutio vingi na mazingira bora ya uwekekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika, ingawa vivutio na mazingira hayo havikutangazwa tangu awali.

Aidha, Bw. Jenni alishauri kuimarishwa kwa sekta binafsi ili isaidie kukuza biashara ndogo na za kati (SMEs) na hivyo kufanikisha mkakati wa kuboresha uchumi wa nchi na watu wake.

Alisema, biashara ndogo na za kati zinatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kujenga uwezo wa taifa na watu wake kujitegemea.

Bw. Jenni alitoa mfano kuwa, kukua kwa uchumi wa Uswisi kulitokana na ushiriki wa biashara ndogo na za kati ambazo hadi sasa, zinachangia asilimia 99 ya uchumi wa nchi hiyo wakati wawekezaji wakubwa wanachangia asilimia moja tu.

’’Kuimarika kiuchumi wa taifa hakutokani na mchango wa makampuni makubwa ya uwekezaji tu, bali pia biashara ndogo na kati,’’ alisema.

Alisema, kama Tanzania inataka kupiga hatua katika kukuza uchumi wake, inapaswa kuwekeza na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati ili waweze kuimarika kama ilivyo katika nchi nyingine zilipiga hatua kubwa kiuchumi duniani.

Hata hivyo, Bw. Jenni alisema hatua ya kujenga jamii yenye dhamira ya kuendesha biashara kiuchumi, inachukua muda mrefu kufikia malengo yake.

Kwa upande wake, Bw. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited alisema kuna haja ya kuendeleza ushirikiano kati ya Uswisi na Tanzania ili kufanikisha maeneo yatakayochangia kukuza uchumi wa nchi.

Bw. Mengi aliyataja maeneo hayo kuwa kujenga uwezo kwa wadau wa sekta binafsi kupitia CTI, kutoa mafunzo na uzoefu katika sekta ya hoteli na kufanikisha uanzishaji wa benki ya wanawake nchini.

Alisema, suala la kujenga uwezo linapaswa kulenga maeneo ya tafiti hasa zitakazofanikisha kukuza na kuendeleza biashara ndogo na za kati.

Aidha, Bw. Mengi alisema sekta za hoteli na benki ni maeneo yanayoweza kupata mafanikio makubwa ikiwa yatapata msaada wa kitaalamu na uzoefu kutoka Switzerland.

Akizungumzia umuhimu wa benki ya wanawake, Bw. Mengi alisema kada hiyo ina wajibu mkubwa kuanzia ngazi ya familia, hivyo ikiwa watawezeshwa kupitia umiliki wa benki maalum, watapiga hatua na kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Bw. Mengi alisema, kwa hali ilivyo hivi sasa benki nyingi haziwanufaishi watu maskini wanaohifadhi fedha zao katika taasisi hizo.

’’Akiba za watu maskini kwenye mabenki haziwanufaishi na badala yake watu matajiri ndiyo wanaonufaika kupitia akiba za watu maskini,’’alisema.

Pia Bw. Mengi alisema kuna haja ya kupunguza wigo uliopo kati ya fikra za watu na hali halisi kwa watu wa nchi za magharibi kuhusu nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Alisema, kuwepo kwa fikra potofu kunaweza kuwafanya wawekezaji kuzikimbia nchi za Kiafrika na kwenda katika nchi nyingine.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.