Na Yahya Charahani , New York
SERIKALI ya Tanzania itapeleka kikosi cha jeshi la kulinda amani nchini Lebanon, wakati wowote kuanzia sasa.
Akizungumzia mafanikio ya Tanzania katika kipindi cha miaka miwili ya uanachama wake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dk Augustine Mahiga, alisema kikosi hicho cha kombania moja kitaondoka wakati wowote.
“Ni kitu ambacho nafurahi sana , tumefanikisha, tumepata mwanya wa kuingia na kutambulika kulinda amani mahali ambapo ni pagumu, papya, halafu wanasema hawa askari wetu watakuwa kwa kamanda wa brigedi sasa sijui kamanda atakuwa ni wa kitaliani au kifaransa lakini watu wetu wanaenda kuwa militari polisi kwenye makao makuu ya kamandi ya brigedi,”alisema.
Lebanon na Israeli, zilikuwa katika mgogoro mkubwa uliosababisha vita kati yao Julai mwaka huu, na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.
Akielezea jinsi fursa hiyo ilivyopatikana, alisema alipewa maagizo na Rais Jakaya Kikwete kwamba azungumze na Umoja wa Mataifa idara ya kulinda amani, ili Tanzania ipeleke batalioni kulinda amani, akaulizia na kuelezwa kwamba Tanzania inakubalika, huku kukiwa na nchi zingine zilizokataliwa kwa kuwa hazina uhusiano na Israeli.
“Lakini batalioni hiyo lazima iwe fully mechanized, yaani doria kule siyo ya kutembea kwa miguu, ni doria ya APCS ni gharama sana kuiandaa batalioni na kuifanya iwe na vifaa vya kisasa, nikapewa jukumu la kutafuta watu ambao wanaoweza kutusaidia kutupa vifaa hivyo,”alisema.
Alisema serikali ilipewa jukumu la kuandaa kombania moja ya polisi jeshi (MP-military police) na kombania moja ni kama watu 75. Hata hivyo, kombania inahitaji vitu vingi yakiwemo magari mapya 25.
“Nikafika hapa kupiga ripoti Umoja wa Mataifa wakasema sasa tunapeleka timu ya wakaguzi , tuone kama kweli nyinyi mnavyo hivi vitu na vinafaa ni vitu vingi ikiwa ni pamoja na mbwa wa kunusa, wale mbwa wametolewa polisi na wamefanya mpango polisi wamewapa wale mbwa.”
“Na wale askari wetu wakajifunza lugha ikanyooka, timu ya ukaguzi imetoka New York ikaenda Dar es Salaam ikasema safi ,”alisema Balozi.
Alisema kupelekwa kwa jeshi hilo ni matokeo ya azimio namba 1701 , ambalo licha ya kuchukua muda mrefu kuliko ilivyostahili kuchukuliwa, walijadiliana na hatimaye likapelekwa jeshi la kulinda amani.
Hadi sasa majeshi makubwa ya Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, italia, Indonesia , Malaysia, Bangladesh yamepelekwa na yanahitajika majeshi 15,000 ya ziada.