Na Alphan Mlacha.
KAMPUNI ya Kimarekani ya Richmond Development Corporation (RDC) iliyopewa tenda ya kufua umeme wa megawati 100 imeendelea kutoa ahadi, mara hii ikisema megawati 22 zitaingizwa katika gridi ya taifa ifikapo mwisho wa wiki.
Kampuni hiyo ambayo juzi ilidaiwa kuzuia waandishi kuingia katika yadi yake iliyoko Ubungo, Dar es Salaam jana iliruhusu jopo la wanahabari kuingia na kushuhudia kazi zinazoendelea ikiahidi kufanikisha azma hiyo.
Uamuzi huo umetolewa huku kukiwa na hisia kuwa serikali tayari imekatishwa tamaa na kuchukizwa na mwenendo wa Richmond zinazoonyesha kuchukizwa na utendaji wa kampuni hiyo ambayo inaibebesha mzigo serikali kwa kutoipa fedha.
Richmond, ilitangazwa na Waziri wa Nishati na Madini, Nizar Karamagi Novemba 23 mwaka huu akiwa na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuwa, ingeanza kutoa nishati ya umeme ifikapo Desemba Mosi, jambo ambalo halijafanyika hata sasa.
Hata hivyo, waziri Karamagi ambaye yuko safari nje ya nchi ya nchi kikazi, hajaeleza hatma ya Richmond na wala kugusia kuhusu ahadi aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari baada ya kutotimizwa.
Tayari, kuna taarifa kutoka Ikulu zinazoonyesha hofu ya wazi ya Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na utendaji huo unaosuasua wa kampuni hiyo. Kikwete alikuwa makini kwa kutogusia suala la umeme katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka.
Meneja wa Richmond, Naeem Gire aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa, tayari kuna mikakati za ufuaji huo wa umeme wa megawati 22 na akabainisha kufanyika kwa majaribio ya kuwasha mashine, jambo ambalo halikuthibitishwa na gazeti hili. Ni megawati hizo 22 zinazotarajiwa kuanza kufuliwa, kuanzia mwishoni wa juma.
Katika ziara hiyo ya waandishi wa habari kuruhusiwa kuingia sehemu inapofungwa mitambo ya kampuni hiyo,eneo la ubungo, jijini Dar es Salaam ambalo picha za awali za gazeti dada, Mwanachi juzi zilionyesha kazi zikiendelea na zilipigwa kutokea nje ya uzio baada ya waandishi kuzuiwa kuingia ndani mahali ilipo mitambo.
"Tumeshajaribu mtambo jana na uliwaka vizuri, kwa hiyo sasa hivi tunafanya marekebisho madogo na kujaribu ili tuweze kuingiza kwenye gridi," alisema Gire na kuongeza kuwa uwezo wa mashine hiyo ni megawati 22 huku megawati 80 zilizobaki, zikisubiri mitambo mingine kuletwa nchini kwa meli kutokea Afrika Kusini, hapo baadaye.
Hata hivyo, Gire alieleza kuwa kukwama kwao kunachangiwa na kampuni yake kuwa haijapata malipo kutoka serikalini, licha ya kuwa ilishatuma ankara za kuomba malipo hayo. Alieleza baadaye kuwa, kamopuni hiyo iko radhi kuendelea na zoezi la ufuaji wa umeme na kisha kudai malipo yao baada ya zoezi hilo kukamilika.
''Mara ya kwanza tuliomba fedha serikalini, lakini hatukupewa hata shilingi, tukaona tuendelee tu na shughuli zetu. Tumeshindwa kuelewa kuwa walikuwa hawana imani na sisi au la!''alisema.
Mhandisi wa kampuni hiyo, Gordon Ware alisema kuwa, kazi ya ufungaji mitambo imechukua muda mrefu kuliko matarajio kutokana na sababu za kiufundi. Hata hivyo hakueleza sababu hizo.
Mtaalam huyo akawataka Watanzania na serikali wasiwe na wasiwasi kwani sasa kampuni hiyo iko katika hatua za kukamilisha shughuli ndogondogo kabla ya uzalishaji kuanza.