Na Waandishi Wetu
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akionyesha dhahiri kuelemewa na mzigo mzito katika kukabiliana na matatizo ya ndani ya nchi yake yakiwamo ya utatuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar, mgawo wa umeme na kudorora kwa uchumi,kiongozi huyo amejibebesha mzigo mwingine.
Hofu na wasiwasi huo ambao umeonyeshwa na wasomi na wanataaluma mbalimbali waliozungumza na Mwananchi Jumapili kuhusu wazo la kukubaliwa kwa wiki hii kwa nchi za Rwanda na Burundi kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baadhi yao, wanaeleza wasiwasi wao, hasa wa kuiona Tanzania ikikubali kirahisi rahisi kujibebesha mzigo mwingine.
Wanaeleza kuwa kitendo cha kuzikubalia mapema nchi hizo, ambazo zina rekodi ndefu, chafu ya migogoro iliyosababisha wakimbizi ambao wamekuwa mzigo kwa Tanzania kwa miaka mingi kabla na baada ya uhuru, kunahitaji mjadala wa kitaifa.
Wasomi hao, wanaeleza kuwa Tanzania inakabiliwa na matatizo mengi sugu yanayoathiri uchumi wake na hali ya maisha ya wananchi na kitendo cha serikali kujiingiza katika maamuzi ya kuziruhusu Burundi na Rwanda kuingia katika mchakato wa kujiunga na Afrika Mashariki, kunaonyesha wazi namna Tanzania itakavyoathirika zaidi, kinyume na mafanikio inayoyatarajia.
Kwa mfano, wanaeleza kuwa tayari haijalipatia jawabu tatizo la mpasuko wa kisiasa uliopo visiwani Zanzibar, mgogoro uliodumu kwa muda mrefu, sasa inalazimika kufikiria jinsi ya kutatua mauaji ya kikabila huko Tarime, migogoro ya wafugaji na wakulima katika mikoa ya Morogoro na Mbeya.
Pia, inakabiliwa na tatizo la kuporomoka kwa shilingi, tatizo la ukosefu wa nishati ya umeme iliyosababisha mgawo, kupanda kwa bei ya bidhaa na hali ngumu katika huduma za raia mathalani elimu na afya.
“Kama tukitaka kutazama matatizo ya viongozi, basi si Kagame (Paul), Rais wa Rwanda tu, bali hata Museveni (Yoweri), yule (Museveni) amehusika katika uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa demokrasia,” anasema Profesa Haroub Othman wa Chuo Kikuu Dar es Salaam alipofanya mahojiano maalum na gazeti hili jana.
Profesa Haroub anaungana na wasomi mbalimbali wanaoonyesha wasiwasi na hatua ya kuziruhusu Rwanda na Burundi kujiunga na jumuiya hii sasa na anaongeza kuwa; kuna matatizo yanayozikabili nchi hizi kwa kila nchi moja moja na pia ukanda huu. Matatizo anayoyabainisha yapo katika ukiukaji haki za binadamu, kujihusisha na machafuko na pia kukosa mfumo wazi wa utawala kwa viongozi wa mataifa haya.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa ambaye pia ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam, Rasul Ahmed anaeleza: "Kulipaswa kutazamwa suala la wakati kabla ya kuziruhusu nchi hizi kujiunga na jumuiya."
Anaongeza: “Sina wasiwasi na Rwanda, lakini hofu yangu ipo Burundi.
"Kihistoria, Tanzania na pengine Rais Kikwete imekuwa ikitumika kama msuluhishi wa matatizo ya nchi hiyo, lakini sasa kama Burundi atakuwa mwanachama itakuwa vigumu Tanzania kuchukua hatua ya kusawazisha machafuko Burundi kwa kuwa itaonyesha kukumbatia serikali iliyopo madarakani,” anasema.
Anaongeza: “Nadhani, sasa nafasi ya Afrika Kusini ndiyo itakayotumika katika kusuluhisha Burundi na sio Tanzania.”
Tatizo lingine analojadili Ahmed ni kuhusu bajeti ya jumuiya ambayo imekuwa ikiyumbayumba kutokana na nchi wanachama kukosa uwezo wa kumudu gharama.
Anaeleza kuwa, kuingia kwa Rwanda na Burundi kwa hivi sasa ni kuongeza tatizo katika jumuiya kuliko ufanisi wake.
Wachambuzi hao wa masuala ya siasa na utawala, waliiambia Mwananchi Jumapili kuwa kuziruhusu Rwanda na Burundi kunaonyesha kuwapo kwa uwezekano wa kuathiri azma ya kupatikana kwa umoja wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki ambao sasa uko katika nafasi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi.
Wanaonyesha wasiwasi kuwa mchakato huo utakuwa mgumu kufikiwa kufuatia kuongezeka hofu zaidi ya iliyokuwepo baina ya nchi hizi tatu baada tu ya kutangaza kuziruhusu Rwanda na Burundi kujiunga na jumuiya hii.
Baadhi yao walieleza kwamba muungano wa kisiasa ungeachwa ufanikiwe kwanza kabla ya kuingiza wanachama wapya na kueleza kuwa kitendo cha kufanyika sasa kinaongeza hofu hasa kwa Tanzania ambayo kihistoria imekuwa kimbilio la wakimbizi kutoka nchi za maziwa makuu.
Tatizo hilo, wanaeleza kuwa lilikuwa likiambatana na kuongezeka vitendo vya uhalifu, uharibifu wa mazingira na kumomonyoa uchumi wa taifa, kufuatia kutumia gharama zake ambazo zingeelekezwa katika maendeleo ya walipa kodi katika kusaka amani katika nchi hizo zinazozalisha wakimbizi na pia kuwahudumia wakimbizi hao pale misaada ya wahisani inaposhindwa kukidhi lengo.
Kuna tatizo la kiulinzi katika nchi za Rwanda na Burundi, ni Tanzania itakayokuwa kimbilio hasa sasa baada ya nchi hizo kuwa wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sababu hii inatokana na historia ya Tanzania na pia mazingira yake tofauti na ilivyo Kenya na Uganda.
Rwanda kwa hivi sasa ina mkwaruzo mkali na Ufaransa kufuatia mahakama moja ya Ufaransa chini ya Jaji Jean-Louis Bruguiere, kutoa maamuzi ya kumtaka Rais Paul Kagame kutiwa nguvuni kufuatia kuhusika na mauaji ya Rais Juvenal Habyarimana, yaliyotokea baada ya kutunguliwa ndege Aprili 6, 1994 na kumuua rais huyo sambamba na rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira. Wapenda amani mbalimbali duniani, wamekuwa wakitoa maoni ya mahakama hiyo kutoa ushahidi huo na Kagame kutiwa nguvuni na sio Kagame kutumia nafasi yake kuziba mianya ya maovu yake kama yapo kuonekana na kuadhibiwa.
Rwanda imevunja uhusiano wake wa Kibalozi na Ufaransa na mgogoro huu unaweza kuyakumba mataifa yote ya jumuiya ya Afrika Mashariki hususani baada ya kuiingiza Rwanda katika jumuiya hii.
Nchi hiyo pia imekuwa ikilalamikiwa mara kwa mara kuhusiana na kujihusisha na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Kongo DRC dai ambalo halijawahi majibu yanayithibitisha kukanushwa au kukubalika.
Mgogoro ndani ya DRC, unamkumba pia Rais Yoweri Mseveni wa Uganda. Rwanda na Uganda zimeonekana kujinufaisha na madini ya Alamsi kutoka DRC na zimekuwa zikisingia kujiingiza katika DRC kwa sababu za kiulinzi na kusema DRC inashindwa kulinda mipaka yake hali inayofanya machafuko kuingia hadi ndani ya nchi hizo.
Museveni, kwa miaka zaidi ya 20 ameshindwa kutokomeza mauaji yanayoendelea mashariki ya Uganda yakiongozwa na vikundi vya Joseph Kony na pia rais huyu amekuwa akihusishwa na uvunjaji wa haki za binadamu.