MKUU wa Mkoa wa Iringa, Halima Kasungu amewataka wakazi wa Ilula, Kata ya Mazombe Wilayani Kilolo kujitokeza kupima virusi vya ukimwi, ili wajue hali ya afya, kutokana na kasi ya maambukizo ya ugonjwa katika eneo hilo.
Takwimu za ugonjwa huo katika Tarafa ya Mazombe inaonyesha kuwa kati ya watu 2,015 waliojitokeza kupima ukimwi tangu Desemba 2005 hadi Novemba mwaka huu, watu 813 ambao ni sawa na asilimia 40.3 kati yao wamekutwa wakiwa na mambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema takwimu hizo zipo juu na kuwa endapo jamii isipokubali kupima kwa hiari ili kujua afya zao na kubadili tabia, hali itaendelea kuwa mbaya zaidi kutokana na biashara ya nyanya inayosababisha mwingiliano wa watu kwenye eneo hilo la Ilula.
"Hakuna sababu ya kulifumbia macho tatizo la ukimwi, vinginevyo tutaangamia kama hatutakubali kuacha tabia zinazochangia kasi ya maambukizi haya na kupima kwa hiari ili kujua afya zetu," alisisitiza.
Alisema watu wakijitokeza kupima afya zao na kugundulika kuwa wameambukizwa na virusi vya ugonjwa huo, wanaweza kupewa dawa za kurefusha maisha na kuendelea kuishi muda mrefu zaidi kuliko mtu ambaye hatajua kama ameambikizwa ama la.
Mkuu wa Mkoa alikipongeza Kituo cha Afya cha Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) cha Ilula kwa jitihada za kutoa huduma kwa watu wanaoishi na virusi hivyo kwenye eneo hilo, ambapo tayari wameanza huduma ya kupima chembechembe za damu (CD4) na kutoa dawa za kurefusha maisha.
Kwa upande wake Katibu Tarafa ya Mazombe, Bena Polisi, alisema sambamba na kuwepo kwa mashirika mengi yanayotoa elimu ya ukimwi katika eneo la Ilula, hali ya maambukizi ya VVU kwenye tarafa hiyo inazidi kupanda ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.