WATU Watano wamefariki dunia kutokana na maradhi ya kipindupindu na wengine 11 wamelazwa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja na kambi ya maradhi hayo iliyofunguliwa Chumbuni mjini hapa.
Kaimu Mkurugenzi wa Kinga, Juma Rajab, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wagonjwa walifariki wanatoka katika maeneo ya Draja Bovu, Pwani Mchangani, Shamba na Tomondo.
Alisema kati ya wagonjwa waliofariki, mmoja ni mwanamke na wanne ni wanaume. Wakati mtu mmoja alifariki kwenye kambi ya Chumbuni, watu wanne walifia katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Hata hivyo Rajab alisema kasi ya maradhi hayo hivi sasa inaelekea kudhibitiwa na idadi ya wagonjwa wanaoripoti kila siku hospitali imepungua.
Alisema pamoja na serikali kupiga marufuku uuzaji wa vyakula vya maji maji, ikiwemo juisi na urojo, baadhi ya wananchi wanakiuka amri hiyo na wanaendelea na kuuza vyakula hivyo.
Alionya kuwa Wizara ya Afya na Baraza la Manispaa litaanzisha operesheni maalum kwa kupitia maeneo mbalimbali kupambana na watu wanaokiuka amri ya kuuza vyakula hivyo.
Aliwataka wakuu wa wilaya, serikali za mitaa na masheha kusimamia utekelezaji wa agizo la serikali la kukata biashara ya urojo na juisi.
Jumla ya wagonjwa 69 wameripotiwa kulazwa hospitali kwa ugonjwa huo tangu Novemba 7 hadi juzi kutoka maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar.