Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa ameziagiza halmashauri za wilaya na manispaa kuwasaidia waathirika wa Ukimwi na watoto yatima badala ya kutegemea wahisani kutoka nje.
Bw. Lowassa alitoa agizo hilo jana wilayani Hai alipokuwa akizindua awamu ya tano?ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuwasaidia waathirika wa ugonjwa huo na watoto yatima ambao wazazi wao walifariki kutokana na Ukimwi.
Alisema ni wajibu wa jamii kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri kutoa huduma kwa makundi hayo hasa chakula na mahitaji mengine ya muhimu.
Bw. Lowassa alisema fedha zinazokusanywa na kampuni ya uchimbaji madini ya Geita Gold Mine ambayo ni Mdhamini Mkuu wa mradi wa kupanda mlima huo, hazitoshelezi mahitaji yanayotakiwa hivyo ni wajibu wa jamii kutoa ushirikiano wa kutosha.
Alisema, pamoja na zoezi la utoaji wa dawa za kurefusha maisha (ARV) linaloendeshwa na serikali, waathirika wa Ukimwi wanahitaji chakula cha kutosha ili kukidhi mahitaji halisi katika kutumia dawa hizo.
Bw. Lowassa alisema Ukimwi unaendelea kuiathiri jamii na kutoa mfano kuwa, wilaya ya Makete mkoani Iringa ni miongoni mwa maeneo yenye hali mbaya ikiwemo idadi kubwa ya watoto yatima ambao wazazi walifariki kutokana na Ukimwi.
’’Imefikia mahali kwa jamii ione kuwa jukumu la kuwasaidia watoto yatima na waathirika wa Ukimwi ni la kila mmoja, siyo kusubiri wahisani wawasaidie kila kitu, kwa kutumia zoezi la upandaji wa mlima pekee hatuwezi kupata fedha za kuwasaidia waathirika zaidi ya milioni mbili waliopo nchini,’’alisema.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Geita Gold Mine, Bw.Ulrich Sibilski alisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2002,?zaidi ya Sh. milioni 410 zimeshakusanywa.
Alisema, fedha zitakazopatikana kwa awamu hii zina lengo la kuwahudumia watoto yatima ambao?wazazi wao walifariki kutokana na Ukimwi.
Alisema watu 51 wakiwemo Watanzania 30, walishiriki kupanda Mlima Kilimanjaro na walitumia siku sita.
Alisema, washiriki wengine walitoka Australia, Kenya, Afrika Kusini na Ujerumani.