Na Mwandishi Wetu
JESHI la polisi likishirikiana na polisi wa kimataifa (Interpol) limewakamata wafanyabiashara maarufu 10 wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Akizungumza jijini Dar es salaam jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai Robert Manumba, alisema watu watano kati ya 10 waliokamatwa wamekwisha kufikishwa mahakamani.
Manumba alisema dawa hizo ambazo ni heroin na cocaine zinatoka katika nchi za India, Pakistan, Iran na Norway
Alisema operesheni ya kuwakamata wafanyabiashara wa dawa hizo, wakiwa ni pamoja na watumiaji na mawakala, inafanyika kwa ushirikiano wa polisi wa kimataifa (Interpol) na Jeshi la Polisi.
Manumba alisema kila kona nchi kuna mitego ambayo wameshaiweka kwa ushirikiano huo ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo wanatiwa nguvuni.
Akizungumzia bangi, alisema mikoa ya Arusha, Iringa na Mbeya imegundulika kuwa na mashamba mengi ya bangi ambayo baadhi wameweza kuyateketeza na bado wanaendelea kuyasaka mengine.
Alisema makosa ya kijinsia pia yameongezeka kwa kiasi kikubwa ambayo ni pamoja na ubakaji na ulawiti hasa watoto wadogo.
Akitoa tathimini ya hali ya uhalifu nchini, Manumba alisema kwa upande wa ujambazi, uhalifu huo umepungua lakini jeshi la polisi linaelekeza macho yake kwa na nguvu zake zote katika benki za wananchi Saccos.
Alisema lengo ni kuiweka nchi katika hali ya amani na usalama na kwamba jeshi hilo limedhamiria kuweka ulinzi wa uhakika katika benki hizo zilizopo sehemu mbalimbali nchini.
Kuhusu ajali barabarani alisema kuwa bado ni tatizo, kutokana na uzembe wa madereva, ambao wanakuwa hawajali maisha ya watu wengine.
Alisema kutokana na ongezeko la ajali Jeshi la Polisi limeunda kamati kwa kushirikiana na wamiliki wa magari, madereva, Tanroads, watumiaji wa barabara na sumtara.