Na Waandishi Wetu
KAMA walivyofanya wabunge wa Bunge la Jamhuri la kutokuzungumzia kabisa tatizo la umeme ambalo limeuporomosha uchumi wa taifa, jana Rais Jakaya Kikwete naye aliangukia kwenye mtego huo kwa kutokusema lolote kuhusu umeme katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi.
Katika hotuba hiyo ya kurasa nane aliyoitoa mjini Musoma kuadhimisha siku ya ukimwi duniani, ambayo pia ilikuwa moja ya hotuba zake za mwisho wa mwezi kwa wananchi aliyosema atazungumzia baadhi ya masuala mengine muhimu ya kitaifa, Rais Kikwete hakugusia kabisa umeme, ingawa aligusia hali ya chakula nchini.
Katika mkutano wa Bunge uliomalizika mwezi uliopita, wabunge hawakuzungumzia kabisa kero ya umeme ingawa walijuwa wazi kwamba ulikuwa umeathiri si shughuli zao binafsi tu, bali za uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kulikuwa na habari kutoka Dodoma kwamba wabunge wa CCM walifanya mkutano wao kama kamati ya chama na kukubaliana “kusitiriana” kutokana na matatizo ya umeme na hasa jinsi kampuni zilizopewa kazi ya kuzalisha umeme wa dharura zilivyokuwa zikifanya kazi.
Hotuba ya jana, Rais ameitoa baada ya kutokufanya hivyo mwishoni mwa Oktoba kutokana na kuwa nje ya nchi kikazi na kwa hali hiyo wananchi wengi walitarajia Rais angezungumzia hali ya umeme nchini kutokana na upatikanaji wa nishati hiyo kuzidi kuwa mbaya.
Aidha, hotuba ya Rais ameitoa siku ambayo kampuni iliyopewa jukumu la kuanza la kuzalisha umeme wa dharura – Richmond Development Corporation ikiwa imeshindwa kuanza kuzalisha megawati 22 kama ilivyoahidiwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.
Novemba 22, mwaka huu Tanesco walitoa tangazo kwenye vyombo vya habari wakisema kwamba Richmond ingeanza kuzalisha megawati 22 kabla ya Desemba mwaka huu, hadi jana umeme huo ulikuwa haujaanza kuzalishwa.
Hadi sasa haijajulikana ni kwa nini Rais amekwepa kuzungumzia tatizo la mgawo wa umeme kwa sababu mbali ya kuwa kero kubwa kwa wananchi kwa sasa, pia umesababisha hasara kubwa kiuchumi.
Inakadiriwa kwamba kiasi cha hasara ya Sh815 bilioni kwa uchumi wa taifa itapatikana kuanzia Januari hadi mwisho wa mwezi huu kutokana na mgawo wa umeme ambao umesababisha uzalishaji viwandani na huduma mbalimbali nchini kukwama kabisa.
Hasara hiyo ni sawa na moja ya sita ya bajeti ya taifa ya Sh 4.8 bilioni kwa mwaka.
Habari kutoka vyanzo vilivyo karibu na Ikulu jana viliiambia Mwananchi kwamba, ingawa Rais amekwepa kuzungumzia hali ya umeme nchini, lakini haridhishwi kabisa na jinsi kampuni ya Richmond inavyoshughulikia suala hilo tangu iingie mkataba wa kuzalisha megawati 100 na serikali Juni 23, mwaka huu.
Richmond wanatakiwa ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe wamekwisha kuanza kuzalisha megawati 100 za umeme na kuingizwa kwenye gridi ya taifa ili kupunguza makali ya mgawo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alisema kutokana na umeme wa Richmond, Aggreko, Songas na huo unaozalishwa na Tanesco, ifkapo mwisho wa mwezi huu mgawo utakoma kabisa. Aggreko na Songas tayari wanaendelea na uzalishaji kama kawaida, tatizo likiwa ni Richamond kwa sasa.
Vyanzo vya habari vinasema kinachompa Rais kigugumizi cha kuzungumzia umeme kwa sasa ni “urafiki” wake na watu wanaoizunguka Richmond, wengi wakiwa ni watu wake wa karibu zaidi katika serikali na kwamba alichofanya jana ni sawa na “funika kombe mwanaharamu apite.”
Tangu Richmond wapewe kazi hiyo na serikali, kumwekuwako na matatizo mengi juu ya uzingatiaji wa ratiba ya kukamilisha kazi hiyo, lakini kikubwa zaidi ikielezwa ni kukwama mara kadhaa kutokana na kukosa fedha za kutosha.
Awamu ya kwanza ya mitambo ya Richmond ya kuzalisha megawati 22 inaelezwa kuendelea kufungwa katika kituo cha Tanesco cha Ubungo, na inaelezwa kwamba mitambo iliyobaki yenye uwezo wa kuzalisha wastani wa megawati 80 ungewasili nchini wakati wowote. Hadi sasa haijawasili na ifikapo mwisho wa mwezi huu inatakiwa kukamilisha kazi ya uzalishaji wa megawati 100.
Kuhusu maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani, yenye kauli mbiu “Zuia Ukimwi timiza ahadi yako” Rais alielezea kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya NGO kutumia fedha zinazokusanywa kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa ukimwi pasipo kuzingatia makusudio yake na akazitaka zibadilike haraka.
“Natambua kuwepo maneno ya baadhi yenu kudaiwa kutokuwa waaminifu. Yaani kwamba fedha nyingi mnazopata kwa ajili ya kuhudumia waathirika au yatima haziwafikii walengwa. Zinatumika kinyume na kwa manufaa binafsi ya wenye NGO husika. Naomba wahusika waache tabia hiyo mbaya. Naomba pia mbanane wenyewe kwanza na mrudishane kwenye mstari,” alisema.
Kuhusu maambukizi ya ukimwi nchini, rais alisema yanaonekana kupungua kwa maambukizi mapya, lakini pia akaeleza kuwa, asilimia saba ya watanzania wameathirika na ukimwi, hali inayohitaji mkakati kukabiliana nayo. Watanzania 8,000 hadi 10,000 hufa kila mwezi kutokana na ukimwi, hali iliyosababisha kuongezeka kwa watoto yatima ambao wazazi wao wamefariki kwa ukimwi kufikia milioni mbili.
katika hotuba hiyo ya Rais pia alizungumzia tatizo la ukosefu wa chakula na akabainisha kuwa baadhi ya maeneo katika mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga na Mwanza hayakupata mavuno ya kutosha.
“Serikali imejiandaa vya kutosha kukabiliana na tatizo lolote la upungufu mkubwa wa chakula iwapo litajitokeza katika maeneo hayo au mengineyo nchini ambayo sasa hatuna taarifa nayo. Tumeamua kuimarisha akiba ya chakula (SGR) kwa kuhakikisha kuwa tunayo akiba ya kutosha ya chakula wakati wote,” alisema na kuongeza kuwa;
“Katika kutekeleza uamuzi huo, tayari tumeshanunua jumla ya tani 96,019 za nafaka ya mahindi na mtama ambazo zimehifadhiwa kwenye maghala ya hifadhi hiyo katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Lengo letu ni kufikisha tani 150,000 ambazo ndiyo ukomo wa SGR kwa chakula cha mahitaji ya dharura.”
Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF) kimeitaka serikali kusimamia fedha zinazotolewa na wahisani kwa ajili ya kununua dawa za kurefusha muda wa kuishi kwa waathirika na kulea watoto yatima.
Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyasema hayo katika ujumbe wake wa siku ya ukimwi duniani kwa vyombo vya habari.
Aliitaka serikali pia kutenga fedha za kodi za kutosha kwa ajili ya kupambana na ukimwi ili ziweze kusaidia watoto yatima na isiwe jukumu la taasisi binafsi na wahisani pekee.
Lipumba aliitaka serikali ihakikishe ongezeko la waathirika linapungua kwa kuhamasisha kwa nguvu zote watu kujizuia na maambukizo ya Ukimwi kwani wataalam wengi wenye uwezo mkubwa wa kujenga taifa letu wanapoteza maisha kwa ugonjwa huo.