Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Penzi lako Silitaki!
http://www.habaritanzania.com/articles/2125/1/Penzi-lako-Silitaki!
By Mzee Mwanakijiji
Published on 12/3/2006
 
Ni utenzi mfupi wa mtu aliyetamani cha mtu kumbe vyote ulaghai!

Na HabariTanzania.com

Penzi lako silitaki
Kwani halitendi haki
Limenipa taharuki
Kupenda kitu cha watu!


Cha mwingine siyo chako
Hata kama ni ukoko
Kutamani cha mwenzako
Ni kuleta utukutu!


Nitatafuta mwingine
Penzi lake nilione
Nami siku nione
Ya penzi lisilo butu!


Wewe mpe atakaye
Tena yeye ashikaye
Nakuaga kwahiriye
Mi panya, wewe chatu!


Ninajisikia homa
Kauli imenizima,
Moyo wangu waniuma
Kwa kutamani cha mtu!


Chozi limenidondoka
Pumzi yachoropoka
Nahisi kuweweseka
Sitaki yako mavitu


Kuniringishia dodo
Kwa mbwembwe na madoido
Sikujua hizo nyodo
Si moja wala si tatu!


Natamka hadharani,
Ya kwake nilitamani
Yarabi nimebaini
Kumbe roho ina kutu!


Kwa mbali nitatazama
Nitafute pangu pema
Penye penzi la adhama
Linipalo roho kwatu!


Kwa heri ninakuaga
Kwa maneno naganaga
Ngoma yako sitaiga
Nakataa katukatu


Nenda salama wendako
Kwa huyo aliyewako
Ukampe penzi lako
La kwangu simpi mtu!!