Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Kikwete kushiriki mkutano wa TNBC mara ya kwanza
http://www.habaritanzania.com/articles/2114/1/Kikwete-kushiriki-mkutano-wa-TNBC-mara-ya-kwanza
By Ramadhan Semtawa
Published on 12/1/2006
 
KWA mara ya kwanza tangu aingie madarakani, Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kushiriki katika mkutano wa nne wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) utakaofanyika Desemba 11.

Na Ramadhan Semtawa

KWA mara ya kwanza tangu aingie madarakani, Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kushiriki katika mkutano wa nne wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) utakaofanyika Desemba 11.

Atashiriki mkutano huo akiwa ni mwenyekiti wa baraza na atapata fursa ya kueleza matarajio yake katika baraza hilo na uongozi wa serikali ya awamu ya nne katika masuala ya uchumi.

Mkutano huo wa nne utakuwa ni sehemu ya maandalizi ya mikutano mingine ambayo ni pamoja na utakaohusisha wawekezaji wa ndani utakaofanyika Januari mwakani na wawekezaji wa kimataifa utakaofanyika Februari mwakani, ambayo yote itaongozwa na Rais Kikwete.

Katika awamu ya tatu chini ya uenyekiti wa Rais Benjamin Mkapa, kulifanyika mikutano mitatu ambayo moja ya mambo yaliyokuwa yamejadiliwani ni utawala bora, upatikanaji wa nishati endelevu, maji na kuondoa urasimu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dunstan Mrutu, alisema katika mkutano wa Desemba 11 kutakuwa na mada zitakowasilishwa na sekta binafsi na ya umma.

Mrutu alisema ya sekta binafsi, itakuwa ikiangalia jinsi inavyoweza kuchangia katika kufanikisha ahadi ya serikali ya awamu ya nne ya kuzalisha ajira milioni moja.

Akizungumzia mafanikio ya baraza, alisema hadi sasa limeweza kujiimarisha katika mikoa 19 na kwamba bado mitatu na kuongeza kwamba kumekuwa na mafanikio zaidi ya kuwa na ofisi hizo.