Na Midraji Ibrahim
RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amesema maskini hawezi kuendelea au kuwa na sauti bila kuwezeshwa wala mataifa tajiri kumsikiliza.
Mkapa alisema nchi haiwezi kuwa na maendeleo bila fukara kuwezeshwa na kupewa sauti na mataifa tajiri na kwamba wanachopigania sasa ni maskini kutumia fursa ya kunufaika na sheria za maendeleo ya uchumi.
"Wanaonufaika na sheria za uchumi wa maendeleo ni wachache. Fukara hawezi kuwa na sauti bila mataifa tajiri kutoa nafasi hiyo wala fukara kuendelea bila kuwezeshwa," alisema.
Tume ya Kimataifa inayohusika na masuala ya kujenga uwezo wa kisheria kwa maskini (NCCLEP), inaongozwa na wenyeviti wenza ambao ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madeleine Albright na Profesa Harnando de Soto wa Peru.
NCCLEP, ambayo Mkapa ni mjumbe wake, inatarajia kukamilisha kazi zake mwanzoni mwa mwaka 2008. Rais mstaafu, Mkapa alisema mjadala ulioibuliwa kwenye semina hiyo umebainisha sura ya fukara wa Tanzania na mataifa mengine.
Mkapa, alisema shabaha kubwa ya tume hiyo ni kuwalinda maskini kubaki ni kile walichonacho ili wasinyang'anywe, pia kuwawezesha kukilinda.
"Tuko katika kuandaa mapendekezo ya sekta mbalimbali jinsi ya kuwezesha watu wetu, tumepata mawazo katika mada zilizotolewa, lakini nao wao (kutoka nje) wamejifunza masuala mengi kutoka kwetu," alisema.
Mkapa ni muasisi wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali za Wanyonge (Mkurabita), unaoendeshwa na serikali. Aliwahi kumleta nchini Profesa de Soto kwa ajili ya kuendesha semina jinsi ya kuzigeuza rasilimali mfu kuwa hai.
Katika utekelezaji wa Mkurabita, serikali imeanza utaratibu wa kupima nyumba ambazo hazikufuata utaratibu na kutoa leseni za makazi kwa wamiliki wake, ambazo zinawawezesha kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.
Semina hiyo ya siku mbili ilikuwa chini ya Albright, lengo likiwa ni kutafuta maoni na mikakati kutoa nchi mbalimbali duniani. Albright, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, alifika Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1998 kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.