Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Ramadhan Semtawa  »  Aliyeua mtu kwa Tibaigana kizimbani
Aliyeua mtu kwa Tibaigana kizimbani
By Ramadhan Semtawa | Published  12/1/2006 | Ramadhan Semtawa | Unrated

Na Ramadhan Semtawa

RIPOTI ya uchunguzi wa kifo cha raia, Bernad Mapunda, kilichotokana na kipigo cha polisi kwa tuhuma za wizi wa makasha 27 ya marumaru katika nyumba ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, imetoka na hatua za kisheria zimekwishachukuliwa kwa askari aliyetoa kipigo hicho.

Kifo cha Mapunda kilitokea Septemba 3 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kutokana na kipigo kutoka kwa askari Godfrey Hagai (28).

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, alisema tayari polisi huyo amekwisha kufikishwa mahakamani kuhusiana na kifo hicho.

Kamishna Manumba, alisema uchunguzi ulionyesha kwamba kulikuwa na matumizi ya nguvu kutoka kwa polisi huyo dhidi ya marehemu.

"Uchunguzi umekamilika na tayari hatua za kisheria dhidi ya polisi aliyehusika zimekwisha chukuliwa kwa kufikishwa mahakamani," alifafanua Kamishna Manumba.

Kamishna Manumba, alisema kesi dhidi ya mtuhumiwa huyo imefunguliwa katika Mahakama ya Mkoa wa Pwani akwa kuwa tukio hilo lilitokea Mkuranga katika mkoa huo.

Jalada la kesi hiyo ni namba 6 ya mwaka 2006 ambayo ilifunguliwa Septemba 19, siku chache baada ya tume kumaliza kazi yake.

Manumba alifafanua kwamba, tume hiyo ya uchunguzi ya watu watatu, iliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Sydney Mkumbi.

Kipigo dhidi ya marehemu Mapunda kilitokana na tuhuma za kushirikiana na wenzake wawili ambao ni Seleman Athuman mkazi wa Kigamboni na Maganga Faida, mkazi wa Mkuranga, kuiba makasha hayo 27 yaliyokuwa na marumaru za ujenzi wa nyumba ya Tibaigana.

Taarifa kwamba marehemu Mapunda na wenzake walihusika katika tuhuma hizo za wizi zilipatikana Agosti 25 na ndipo walipokamatwa na kuwekwa mahabusu na ilipofika Agosti 28 alieleza kujisikia maumivu na kupelekwa Muhimbili ambako alifariki siku chache baadaye.

Awali, msimamizi wa nyumba hiyo, Kenny Samson, alitoa taarifa katika kituo cha polisi cha Mkuranga kuhusiana na wizi wa makasha hayo na watu 21 walikamatwa kisha baadaye kuachiwa kwa dhamana kabla ya kubainika marehemu Mapunda na wenzake.

Kufuatia utata wa kifo hicho, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, (IGP) Said Mwema, aliamua kuunda tume hiyo ili kupata undani wa kifo.

Hatua hiyo ilikumbusha tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete, kuchunguza mauji ya Sinza yaliyowahusu wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi mmoja wa Dar es Salaam.

Kwa sasa kesi hiyo ya mauji ya wafanyabiashara hao na dereva teksi inaendelea kuunguruma katika Mahakama ya Kisutu, ikimhusisha Abdallah Zombe, ambaye alikuwa ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dar es Salaam.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.