Na Claud Gwandu
SERIKALI ya Kenya imeishutumu Mahakama ya Afrika Mashariki kuwa imeingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama kinyume na uwezo wake.
Shutuma hizo zilitolewa jana na Rais wa nchi hiyo, Mwai Kibaki, Jijini Arusha, akisema mahakama hiyo imefanya jambo ambalo haina mamlaka nalo.
Akitoa hotuba yake katika mkutano wa viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Kibaki alisema mahakama hiyo haina haki ya kuingilia na kutoa maamuzi ya masuala yaliyofanyika ndani ya nchi wanachama.
Rais Kibaki ambaye pia ni mwenyekiti wa viongozi wakuu wa nchi hizo, alitoa kauli hiyo kutokana na mahakama ya Afrika Mashariki kukubali malalamiko yaliyofikishwa mahakamani hapo na watu 12 kutoka Kenya.
Walalamikaji hao wakiongozwa na Profesa Peter Anyang’ Nyong’ walidai katika malalamiko yao kwamba taratibu zilizotumika kuwapata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Kenya hazikuwa sahihi.
Walitaka, pamoja na mambo mengine, mahakama hiyo itangaze kuwa uchaguzi haukufanyika na walalamikiwa ambao walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Kenya na Makamu wa Rais wa nchi hiyo walipe gharama za kesi hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo,
Amos Wako, alisema kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kisheria na kuwataka walalamikaji kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya nchi hiyo.
Hata hivyo, katika hukumu ya kesi hiyo iliyotolewa Jumatatu iliyopita, Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Joseph Mulenga, alisema mahakama hiyo ina mamlaka kamili ya kusikiliza malalamiko yanayofikishwa hapo.
Kauli hiyo ya Rais Kibaki ilitolewa baada ya jitihada za serikali ya nchi hiyo kuwashawishi wakuu wa nchi wanachama kutengua uamuzi wa mahakama hiyo kushindikana.
Habari kutoka ndani ya vikao vya wakuu hao zinasema kuwa Kenya ilikuwa inashawishi wakuu hao watumie mamlaka waliyonayo katika mkataba wa kuundwa kwa jumuiya hiyo kutengua maamuzi ya mahakama lakini ilikwama.
“Walifikia hatua hadi wakawa wameweka pendekezo hilo katika makubaliano ambayo viongozi wakuu wangeyafikia katika mkutano wao lakini ilishindikana baada ya kuonekana kuwa kuna haja ya kuheshimu maamuzi ya mahakama,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Shinikizo hilo la Kenya kwa kiasi fulani lilifanikiwa baada ya kukubaliwa kubadilishwa kwa baadhi ya vipengele vya mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya ili kuanzisha Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki jambo ambalo viongozi hao walikubaliana nalo.
Wakati huo huo, Jaji Harold Nsekela wa Tanzania na MaryStella Arach Akomo wa Uganda, walitangazwa na kuapishwa kuwa majaji wapya wa mahakama ya Afrika Mashariki.
Majaji hao wanajaza nafasi zilizoachwa wazi tangu Novemba 29, mwaka huu na Jaji
Joseph Warioba na Salome Bosa wa Uganda ambao wamestaafu.
Wakati huo huo, Burundi na Rwanda zimekubaliwa rasmi kuwa wanachama wapya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kufanya jumuiya hiyo kuwa na nchi wanachama watano.
Hata hivyo, nchi hizo zitalazimika kusubiri hadi Julai mosi mwakani ndipo zianze kushiriki katika shughuli za jumuiya hiyo kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya masharti waliyopewa kujiunga na EAC.
Uamuzi wa nchi hizo kujiunga na EAC ulitangazwa jana mjini hapa katika kikao cha viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa viongozi hao, Rais Kibaki alisema kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya nchi hizo kutimiza masharti waliyopewa kabla ya kukubaliwa kuwa wanachama, ingawa hakutaja masharti hayo.
Kibaki alisema nchi hizo zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na nchi za Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na kufanya biashara na kutumia bandari za Dar es Salaam na Mombasa katika kupitisha mizigo yao.
“Hawa ni wenzetu kwa kuwa tumekuwa tukifanya nao biashara kwa muda mrefu hivyo tunawakaribisha katika jumuiya yetu ili tushirikiane kwa pamoja kuwaendeleza wananchi wetu,” alisema Rais Kibaki.
Aliwataka viongozi wa nchi hizo kuhakikisha kuwa lugha za Kiswahili na Kiingereza zinafundishwa katika nchi hizo kwa kuwa ndizo lugha za mawasiliano za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumzia wanachama hao wapya wa Jumuiya, Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa uamuzi huo ni wa kihistoria kwa kuwa nchi hizo zimeomba kujiunga na Jumuiya hiyo muda mrefu uliopita.
“Hawa ni jamaa zetu na kwa kweli wameomba kujiunga na Jumuiya kwa muda mrefu sasa leo ni siku ya kihistoria kwa kuwa umoja wetu umepata wanachama wengine wapya, tunawapongeza na kuwakaribisha sana,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Paul Kagame wa Rwanda alishukuru nchi yake kukubaliwa kujiunga na Jumuiya hiyo na kuahidi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha shughuli zote za jumuiya zinafanyika kama ilivyopangwa.
Alisema Rwanda iliomba kujiunga na EAC tangu mwaka 1996 na kwamba siku zote wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakisubiri kwa shauku kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
"Hiki kwa kweli ni kikao cha viongozi wakuu wa nchi wanachama cha kihistoria kwa kuwa kimekata kiu waliyokuwa nayo wananchi wa Rwanda ya kujiunga na Jumuiya hii ili washirikiane na wenzao katika kuendeleza maisha yao,” alisema.
Naye Rais Pierre Nkuruzinza wa Burundi ambaye alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa lugha ya Kiswahili, alisema kuwa nchi yake imekuwa na hamu ya kuwa mwanachama wa jumuiya kutokana na kutambua umuhimu wake.
Alisema serikali yake ilipoingia madarakani ilianza kutoa elimu ya msingi bure na kufundisha lugha za Kiswahili na Kiingereza ikiwa ni maandalizi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuingia kwa nchi hizo katika Jumuiya kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki Kuwa na watu zaidi ya milioni 100 jambo ambalo litachangia kuongeza biashara kati ya nchi hizo.
Mkutano huo pia ilihudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Amani Karume wa Zanzibar na mawaziri waandamizi kutoka serikali za nchi wanachama na wawakilishi kutoka asasi za kimataifa.