Vifo kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kutokana na sababu mbalimbali ni miongoni mwa matatizo yanayoendelea kuikabili jamii yetu wakati huu ambao dunia inazungumzia kukua kwa sayansi na teknolojia katika nyanja mbalimbali .
Miongoni mwa sababu zinazochangia vifo hivyo ni imani walizonazo baadhi ya watu kuwakataza wanawake wajawazito kwenda kliniki au kwenda kujifungulia katika vituo vya afya au hospitali zenye wataalamu na vifaa vya kutosha kuokoa maisha ya akinamama hao linapotokea tatizo wakati huo.
Imani hizo ambazo zimejikita katika maisha ya baadhi ya watu katika makabila mbalimbali zimekuwa zikichangia vifo vya akina mama hao ikiwa pamoja wakati mwingine na watoto wao.
Kwa mujibu wa takwimu kuhusu uzazi na vifo, imebainika kuwa,karibu mwanamke au msichana mmoja nchini Tanzania hufa kila saa kutokana na matatizo ya ujauzito, uzazi kabla na baada ya kujifungua.
Ili kujaribu kulitafutia ufumbuzi suala hilo hatari kwa maisha ya wanawake wengi, serikali imeweka mikakati mbadala ya kujaribu kuzuia vifo au magonjwa yatokanayo na uzazi.
Hata hivyo, mabadiliko makubwa ni kama bado hayajapatikana hata kuleta unafuu katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Hivi karibuni, Shirikisho la Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari(UTPC) ulifikia makubaliano na shirika lisilo la kiserikali liitwalo Women Dignity Project (WDP) kufanya uchunguzi ili kubaini kwa nini wanawake wanakufa wakati wa kujifungua na kuepndekeza hatua za kuchukua ili kuboresha hali hiyo na kuzuia vifo hivyo.
Mikoa mitano ilipendekezwa kufanyiwa uchunguzi wa kina na kutoa matokeo ambayo yatatoa picha halisi ya hali ilivyo.Mikoa hiyo ni Singida,Lindi, Shinyanga,Manyara, Rukwa na Lindi.
Jukumu hilo la uchunguzi kwa kuzingatia vigezo vya WDP, lilikabidhiwa kwa waandishi wa habari katika mikoa hiyo kupitia klabu zao za waandishi.
Eneo la Shinyanga mjini na wilaya ya Bukombe, waandishi waliopewa dhamana hiyo ni Suleiman Abeid ( gazeti la Majira),Shaaban Alley (Radio Free Africa/Star TV),Eunice Kanumba (Radio Faraja) na Herman Mezza (Business Times).
Waandishi hao wakitumia mbinu za utafutaji habari, walihoji watu na kufanya uchunguzi ili kupata taarifa mbalimbali muhimu.
Yaliyojitokeza katika uchunguzi huo kuwa yanachangia vifo vya akina mama wajawazito ni malaria asilimia 50, utapiamlo asilimia 13,Ukimwi asilimia 10 na magonjwa mengine asilimia 27 Ilibainika kuwa ukosefu au upungufu wa hospitali na zahanti katika mkoa huo unachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya wanawake wakati wa kujifungua hasa wale wanaoshi maeneo ya vijijini ambapo hawapati tiba sahihi na matunzo.
Sababau nyingine ni barabara mbaya zisizopitika kwa urahisi au ambazo haziamikini kupitika kwa wakati wote zinachangia vifo wakati wa kujifungua kwa sababu inakuwa vigumu kuwasafrfisha akina mama hao wajawazito hata kuwawahisha katika hospotali za mkoa au wilaya kupata matibabu muhimu na ya haraka ili kuyaokoa maisha yao.
Sababu nyingine zinazochangia vifo hivyo ni upungufu au ukosefu wa madaktari na wauguzi wenye sifa na utaalamu wa fani hiyo, hasa maeneo ya vijijini, uchache wao katika hospitali na zahanati ni tatizo ambalo linatakiwa kushughulikiwa kwa uzito unaostahili kama lengo ni kutaka kuyanusuru maisha ya akinamama na watoto wao.
Wanawake wajawazito wanaopata matatizo,hupelekwa kwa waganga wa kienyeji ambao huwatibu kwa dawa zao, ambazo hudai kuwa zitawawezesha kujifungua salama.
Lakini ukweli uko bayana kuwa, wajawazito wengi wanaotumia tiba hiyo hawaponi.
Kama hiyo haitoishi, kwa mujibu wa uchunguzi huo ni kwamba,wanawake wanaojifungulia majumbani kwao wanakufa kwa sababu hawapatiwa matunzo wanayostahili.Wakunga na waganga wa kienyeji ni kwamba hawawezi kumudu kutibu matatizo yanayojitokeza baada ya kujifungua kama vile kutokwa na damu nyingi.
Uchunguzi katika eneo hilo, pia umebaini kuwa wanawake wengi hasa wenye kipato cha chini,wanakabiliwa na utapiamlo mkali kutokana na kula lishe duni.
Wanawake wajawazito wenye matatizo hawapelekwi haraka katika hospitali za wilaya na mikoa.
Hii inasababishwa na ukosefu wa usafiri wa kuaminika kutoka vijijini na hata wanapofika katika hospitali hizo hali huwa ni mbaya na hata kusababisha kifo cha mama mjamzito.
Kama hiyo haitoshi, wauguzi na madaktari wengi hawana ujuzi wa kuwahudumia wajawazito ambao ni walemavu kama vile viziwi au mabubu na hivyo kushindwa kuwasiliana na kuwapa msaada unaohitajika kwa tatizo husika.
Kufuatia uchunguzi huo,ilipendekezwa kuwa kunahitajika kampeni maalum ya kuielimisha jamii kuachana na mila potofu ambazo zinazuia akina mama kwenda kujifungulia kliniki na kupata uangalizi makini na wa kitaalamu.
Serikali inatakiwa kuongoza kampeni hii na wadau wote kama vile viongozi wa dini,viongozi wa jamii na vyombo vya habari vishiriki kikamilifu.
Kama hiyo haitoshi,wakunga wa jadi na waganga wanatakiwa kupewa mafunzo maalum ya kitabibu ili kuinua uwezo wao katika kuwahudumia akina mama wajawazito kwa njia bora zaidi.
Kwa upande wa akina mama wajawazito, wanatakiwa kushauriwa kuhudhuria kliniki kama njia mojawapo ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Serikali kwa upande wake, inashauriwa kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini yanakuwa na zahanati zenye vifaa muhimu na vya lazima kwa ajili ya kujifungulia akina mama.
Bi Subila Mwambingu,Afisa Mradi Mwandamizi wa taasisi ya Women Dignity Project(WDP), akizungumzia suala la vifo vya uzazi na magonjwa yatokanayo na uzazi kwa waandishi wa habari hivi karibuni, aliwaambia kuwa tatizo hilo, latakiwa kuchukuliwa hatua muhimu na za makusudi katika kulidhibiti kwa sababu linaweza kuzuilika na kuokoa maisha ya wajawazito hao wakati wa kujifungua.
Baadhi ya hatua zinazopendekezwa kuzingatiwa ni, kuongeza bajeti katika sekta ya afya, ili kuhakikisha kuwa huduma muhimu na za lazima zinakuwepo.
Fedha zaidi zinahitajika kwa namna yoyote ile, zinahitajika kwa ajili ya sekta ya afya na kiasi kikubwa kiweze kuelekezwa kwenye huduma za kuzuia vifo na magonjwa yanayotokana na uzazi.
Hali hii inaashiria kuwa, fedha zaidi zinahitajika kwa ajili ya kuhudumia sekta ya afya na kiasi kikubwa kiweze kuelekezwa kwenye huduma za kuzuia vifo na magonjwa yanayotokana na uzazi badala ya mkazo mkubwa kuwekwa katika kutibu tu.
Katika kutilia mkazo uimarishaji wa huduma hiyo ni kwamba, umuhimu mkubwa uelekezwe kwenye ngazi ya chini ya huduma ya afya na kwenye jamii ambayo haina huduma.
Hatua nyingine muhimu zinazotakiwa kuchukuliwa ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa akina mama wote wajawazito, bila ya kujali kama wana uwezo wa kulipia au la.
Huduma hizo, ni pamoja na zile zinazotolewa kabla ya kujifungua,wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Sera ya kitaifa inazungumzia kuhusu huduma bure kwa akina mama wajawazito. Hivyo,wanawake wasiambiwe kupeleka chochote wakati wanapokwenda kujifungua na wasitoe hongo ili waweze kupata huduma nzuri au bora.
Huduma bora zinatakiwa ziwepo au zipatikane kwa wanawake wote, hata wale wanaoishi vijijini.
Hatua nyingine muhimu zinazotakiwa kuchukuliwa ni pamoja na kupanua huduma za dharura na upasuaji kwenye kiwango cha vituo vya afya(emergency Obstetic Centre).
Huduma hizo za dharura zihakikishwe kuwa zinapatikana kwa mwanamke kati ya mmoja hadi saba kwa wanaohitaji.
Nyingine ni kupanua huduma za dharura na upasuaji kufikia kwenye ngazi ya vituo vya afya, ili wanawake wengi zaidi waweze kuzifikia wakati wa uzazi wa dharura.
Pia inatakiwa uboreshwaji mkubwa katika swala zima la kutoa rufaa kwa akina mama, ikiwa pamoja na kuboresha barabara na usafiri wa maeneo ya vijijini, ili hata wakati wa dharura wanawake waweze kuzifikia hospitali zenye huduma inayotakiwa.
Ni muhimu ikahakikishwa kuwa, wanawake wote wanasaidiwa au kuhudumiwa na wahudumu wenye ujuzi wakati wa kujifungua na si vingnevyo.
Kulingana na utafiti wa kitaifa kuhusu masuala ya afya mwaka 2004/2005 (Tanzania Demographic and Health Survey) asilimia 40 ya wanawake walitoa taarifa kuwa,upatikanaji wa fedha kwa ajili ya matibabu ndiyo tatizo kubwa katika kupata huduma za afya.
SOURCE: Nipashe