Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), limetangaza kuwa mgao wa umeme utarejea tena kesho. Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Bw. Adrian van der Merwe kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa mgao huo utaanza Juni 8, mwaka huu.
Ilieleza kuwa ingawa mvua zilinyesha kwa wingi kwa wiki kadhaa katika mikoa mingi nchini, lakini kina cha maji kwenye bwawa la Mtera mkoani Iringa, bado kipo chini.
Aidha, taarifa hiyo ilileza kuwa kina cha maji kwenye bwawa la Mtera hadi leo (jana) kilikuwa mita 689.01 juu ya usawa wa bahari ambacho kina cha chini kabisa ni mita 690.
Ilieza zaidi kuwa kina cha juu kwenye bwawa hilo ni mita 698.50 na kwamba katika historia ya shirika hilo halijawahi kuwa na kina hicho kidogo cha maji kwenye bwawa la Mtera baada ya msimu wa mvua.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, mvua zilizonyesha ziliongeza maji kwenye mabwawa madogo ya Kidatu, Kihansi na Nyumba ya Mungu na hivyo kuwezesha kuongeza uzalishaji wa umeme kwenye vituo vyake.