Na Mwandishi Wetu
SEMINA ya siku mbili kuhusu mkakati wa kitaifa unaojadili sheria za kuwajengea uwezo maskini maskini (NCCLEP), inayohudhuriwa na watu kutoka nchi mbalimbali duniani, imeanza jana jijini Dar es Salaam.
Semina hiyo jana ilikuwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madeleine Albright, ambaye ni mwenyekiti mweza wa Tume ya Kimataifa inayohusika na masuala ya kujenga uwezo wa kisheria kwa masikini, akiwa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ambao kwa pamoja wanatafuta maoni na mikakati kutoka nchi mbalimbali duniani, safari hii ikiwa ni zamu ya Tanzania.
Katika semina ya jana, Albright, ambaye aliwahi kufika Tanzania mwaka 1998 kutokana na shambulizi la kigaidi katika ubalozi wa Marekani, na baadaye mwaka 1999 wakati wa mazishi ya kitifa ya marehemu Mwalimu Julius Nyerere, alitoa shukrani zake kwa Tanzania kuwa moja ya nchi inayothamini demokrasia na inayokua kiuchumi na akafafanua kuwa jitihada zaidi zinahitajika kuongezwa ili kuwasaidia watu masikini kunufaika.
Alisema, uchumi imara hauletwi kutoka katika mikono ya matajiri wala ile ya serikali, bali uchumi unaokua mithili ya nyumba na ambao unapaswa kujengwa kutokea chini kuelekea juu.
Akizungumza wakati wa hotuba yake ya ufunguzi, Rais Jakaya Kikwete, alisema jitihada na mafanikio yanayotokana na utawala wa sheria hazitoshelezi kuwakwamua wananchi ili kufikia maendeleo ya kiuchumi kama hakutakuwa na sheria zinazowajengea uwezo masikini.
Alifafanua kuwa wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana na serikali katika mkakati huu ili kurahisisha kufikiwa lengo la kuwakwamua masikini.
“Ni jambo lililo katika mtazamo wangu kuwa, ni vigumu kupambana na umasikini kama hakutakuwa na mkakati wa kuwajengea uwezo wa kisheria. Niliposoma malengo ya Tume ya Kimataifa inayohusika na masuala ya kujenga uwezo wa kisheria kwa masikini mapema mwaka jana, nilijiuliza maswali kuhusu kwa nini sisi nchi zinazoendelea na wenzetu katika maendeleo kwa nini hatukubaini mapema kuhusu uhusiano wa sheria na maendeleo,” alisema.
Rais Kikwete alimueleza Albright kuwa Tanzania inashukuru mchango wake na kufika kwake Tanzania.
Ujio wa Albright nchini Tanzania na mkakati wa Tume anayoiongoza unaendana na sera za chama chake cha Democrat kinachozungumzia kuwawezesha masikini kutoka katika makucha ya matajiri.
Chama hiki kimeibuka na ushindi wa Kongresi mapema mwezi huu na duru za kisiasa nchini huko zinaonyesha nafasi ya chama hicho kushinda pia nafasi ya urais mwaka 2008.
Ziara za Albright katika Tume hii anayoiongoza pamoja na Rais Mkapa, zimeshafanyika katika nchi za Brazil, Ukraine na Indonesia huku akitarajia kuelekea Kenya, Uganda na Ethiopia baadaye mwaka huu. Mwakani atazitembelea Sri Lanka, Bangladesh, Mexico na Guatemala.
“Katika ulimwengu wa sasa, watu maskini wameshindwa kulindwa na mfumo wa sheria, hali inayosababisha maisha yao kusinyaa badala ya kuchanua. Uchumi imara na unaokua hauwezi kujengwa na matajiri au kuletwa na serikali. Uchumi unaokuwa na imara ni ule unaojengwa mithili ya nyumba,” alisema Albright.
Awali akimkaribisha Katibu Albright, Rais Mkapa anayeonekana bado mkakamavu, alifafanua kuwa jitihada za kila sekta zinatakiwa katika kumuendeleza masikini.
Alisema pia kuwa mipango ya kitaifa ya kupambana na umasikini iliyopo, inapaswa kutazama mabadiliko mbalimbali yaliyopo ulimwenguni ili kuwezesha malengo kufikiwa.