Na Pendo Mtibuche
POLISI mkoani Dodoma inawashikilia wafungwa wanne wa gereza la Isanga kwa tuhuma za kumnyonga hadi kufa mfungwa mwenzao, Athumani Musa (30).
Wafungwa hao, wanadaiwa kuwa baada ya kumuua, walimwegesha pembeni ya chumba walimokuwamo ndani gereza hilo linaloaminika kuwa na ulinzi mkali nchini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Omary Mganga, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 21 majira ya saa 5:40 usiku katika gereza la Isanga mjini hapa.
Wafungwa hao wote wanatumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha.
Kamanda alisema kuwa marehemu ambaye pia alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la unyang'anyi tangu mwaka 2004, pia alikuwa anatumikia adhabu ya nyingine ya kifungo cha miezi sita kwa kosa la kuidharau mahakama.
Mussa alinyongwa kwa kutumia kamba iliyotengenezwa kwa kitambaa cha suruali ambayo inadaiwa kuwa ilichanwa na kitu chenye ncha kali.
Mganga alidai kuwa mara baada ya polisi kupata taarifa hiyo, walifika gerezani na kufanya uchunguzi ambapo waligundua kuwa ndani ya chumba aliponyongewa, pia walikuwamo wafungwa hao wanne, na baada ya kuwahoji ilionekana kuwa wamehusika na kitendo hicho.
Alisema katika uchunguzi uliofanywa, waligundua kuwa mahali aliponyongewa mfungwa huyo palikuwa ni pafupi kiasi kwamba asingeweza kujinyonga yeye mwenyewe kwa vile miguu ilikuwa inagusa chini, hivyo kuleta wasiwasi kuwa lazima wenzie wameshiriki.
Alisema kuwa wafungwa hao tayari wanatarajia kufikishwa mahakamani kesho kwa tuhuma za mauaji.
Katika tukio jingine kamanda Mganga alisema kuwa polisi inamshikilia mwanamume mmoja mkazi wa Ipagala kwa tuhuma za mauaji ya kumpa juisi inayodhaniwa kuwa na sumu mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili ambaye alikufa baada ya muda mfupi.
Akielezea mazingira ya kifo cha mtoto hiyo, Kamanda Mganga alisema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 28 mwaka huu majira ya saa 8:5 mchana maeneo ya Ipagala mjini hapa baada ya baba mzazi wa mtoto huyo kumnyweshwa juisi inayaodhaniwa kuwa ina sumu.
Alisema kuwa siku ya tukio mtoto huyo aliachwa nyumbani akiwa na baba yake mzazi wakati mama yake, alipokwenda kisimani kuchota maji na baada ya kurudi nyumbani alikuta mtoto akilia, huku akitapika na alipomuuliza mumewe kwanini mtoto yupo kwenye hali hiyo, mumewe alikimbia akiwa ameshika chupa mkononi na kwenda kuitupa sehemu isiyojulikana.
Kamanda aliongeza kuwa katika tetesi, inasemekana kuwa chanzo cha mtuhumiwa huyo kuua mwanae, ni kwa sababu ana mwanamke mwingine wa nje ambaye wanataka kuoana, na alimpa masharti kuwa ili waoane ni lazima awaondoe mke na mtoto wake katika hiyo nyumba.
Mara baada ya polisi kupata taarifa walifika sehemu ya tukio, lakini walikuta mtoto huyo tayari akiwa amekwisha kufa na kumkamata mtuhumiwa huyo, ambaye anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.